She is too young to die -12
Alikuwa mmoja wa chokoraa hao, akamtaka Salome ampe shilingi elfu moja ya Kenya vinginevyo angewaita Mungiki waje wamuue. Kwa sababu hakuwa na fedha za Kenya, Salome alitoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpa mtoto huyo ambaye aliikataa na kudai asingeifanyia kitu, hapo hapo alipiga kelele na kuwaita Mungiki kwa sauti ya juu.
Je, nini kitafuata? Atawapata Gilbert na Faith? SONGA NAYO…
“Mungikiiiiiiii!” mtoto huyo aliita kwa sauti ya juu, Salome akitetemeka mwili mzima, alijua ni kitu gani kingetokea kama watu hao wangerejea mpaka mahali sauti ilipotokea. Alipotupa macho yake mbele aliwaona watu wote waliopita wakiimba wamesimama na kuangalia nyuma, kisha kuanza kutembea kurudi mahali sauti ilipotokea, Salome akajua kifo chake kimefika kabla hajamwona Gilbert na mwanae Faith. Akatamani sana kukimbia lakini alijua kufanya hivyo kusingemsaidia chochote, Mungiki wangemwona na hakuwa na uwezo wa kuwaacha kwa kukimbia, lazima wangemkamata na kumkatakata kwa mapanga hadi kifo.
“Nipe soo nisiwaonyeshe pale uko!” mtoto huyo alisema tena.
“Sina fedha za Kenya mdogo wangu, hizi nilizonazo ni sawa na dola elfu saba za Kimarekani kama zikibadilishwa, tafadhali chukua zote lakini usinitie mikononi mwa watu hawa wauaji!”
“Sitaki pesa za Tanzania!” alijibu mtoto huyo huku kundi la Mungiki likizidi kukaribia
Ghafla Salome alipata wazo la kupekua vizuri ndani ya mkoba wake kwani mara kadhaa siku za nyuma alikuwa na tabia za kusahau fedha za aina tofauti tofauti hasa akirejea kutoka safarini nchi za nje, kwa kasi ya ajabu alianza kupekua mkoba wake na kuzama hadi chini! Bila kutegemea alishtuka alipoiona noti ya dola hamsini ya Kimarekani, ambako kwa kumbukumbu zake haikuwa halisi, aliwahi kubadilisha mtaani na kupewa noti hiyo ya bandia, akiwa na uhakika asingeitambua akaichomoa haraka na kumpatia mtoto huyo.
“Hii poa!”
“Nisaidie sasa!” alisema Salome akiwashuhudia Mungiki wakiwa kama mita sabini tu kutoka mahali alipojificha wakiimba nyimbo za mauaji, ndani ya dakika mbili kama kisingefanyika kitu mwili wake ungekuwa ukigawanywa na mapanga! Alihisi ganzi.
Baada ya kupokea noti hiyo chokoraa alichomoka kutoka nyuma ya mti na kwenda kusimama mbele ya kundi la Mungiki akivuta nta yake, walipomwona wote walisonya na baadaye kuanza kumuuliza kama kuna watu waliokuwa wamejificha mahali popote! Akawaeleza hajamwona yeyote lakini ikitokea akamwona basi atawajulisha ili wammalizie, jibu hilo liliwafanya Mungiki wageuke na kuanza kuondoka zao, Salome akashusha pumzi akiwa haamini kama amenusurika! Walipopotea gizani, mtoto alirejea nyuma ya mti na kumkuta Salome akitetemeka, akamuuliza alikuwa akifanya nini mjini Nairobi wakati huo wa hatari, ikiwa wakazi wote walikuwa wameukimbia mji kwa sababu ya machafuko.
“Namfuatilia mume na mtoto wangu!”
“Walikuwa wakiishi hapa?”
“Hapana!”
“Sasa?”
“Mtoto wangu alikuwa anaumwa moyo, hivyo walikuwa safarini kuelekea India na hapa Nairobi ni lazima kubadilisha ndege, walifika hapa jana na kukuta hali imekuwa mbaya, uwanja wa ndege umetekwa na Mungiki, nao nafikiri watakuwa wametekwa…!”
“Pole sana!”
“Ahsante!”
“Sasa sikiliza, mimi nakushauri kitu kimoja, usijaribu kuzunguka mtaani kwa sasa, Mungiki watakuua, ni bora ujifiche mahali fulani mpaka hali itulie ndipo uanze kuwatafuta, ukifanya sasa hivi utaingia katika hatari, unasikia?”
“Sawa! Lakini nilitaka kwanza nifike uwanja wa ndege!”
“Hauwezi kufika dada yangu ni mbali mno kutoka hapa na hakuna usafiri wa matatuu tangu jana, watu wameficha magari yao na Mungiki wako kila mahali lazima utakutana nao na watakuua kifo kibaya!”
Salome alitulia kwa muda wa kama dakika tano akitafakari mambo ambayo mtoto huyo alimwambia, ni wazi alikuwa hamdanganyi maana yeye tangu machafuko yatokee alikuwepo mtaani! Kulikuwa na mambo mawili ya kufanya, atafute mahali alijifiche kwanza mpaka hali itulie au awe jasiri na kuyatoa maisha yake lakini aendelee kuwatafuta Gilbert na Faith, ndani ya moyo wake aliamini walikuwepo mahali fulani wakihitaji msaada wake, kitendo cha kujificha alikitafsiri kama woga na usaliti wa hali ya juu ambao hakuwa tayari kuufanya.
“Hapana, siwezi!”
“Huwezi nini?”
“Siwezi kujificha, nimetokea Tanzania kwa kazi moja ya kuwaokoa mume na mtoto wangu!”
“Dada! Dada! Dada! Utayakumbuka maneno yangu!”
“Acha niende, nielekeze njia ya kwenda uwanja wa ndege kutokea hapa!”
“Sawa…mimi simo…hii barabara ni Mombasa road, sasa nenda nayo moja kwa moja hapana kukatisha mahali, mbele utakuta kuna njia panda kubwa, ya kulia itakuwa inakwenda Mombasa usifuate hiyo, nenda kushoto mbele yako utaona uwanja kama stima iko utaona maandishi yanawaka juu yameandikwa JKIA, yaani Jomo Kenyatta International Airport, lakini sidhani kama utafika ni mbali mno halafu Mungiki wametawala, utakufa dada!”
“Ahsante wacha mimi niende, nashukuru kwa msaada wako!”
Huku akitetemeka Salome alijikakamua na kusimama wima kisha kuanza kutembea kusonga mbele akipita kando kando ya barabara kwenye nyumba za watu, kulikuwa na giza nene kiasi cha kushindwa kuona mbele, hakuwa na uhakika hata kidogo wa kufika alikokuwa akienda lakini alikuwa ameamua kujaribu kwa ajili ya mume na mtoto wake.
“Woooh!Woooh!Wooooh!” lilikuwa ni kundi la mbwa likija mbio kumfuata yeye, akainama chini na kuchota mchanga mbwa wote wakafunga breki na kurudi nyuma na yeye akasonga mbele.
Kwa masaa mawili alitembea bila kukutana na watu na bila kufikia njia panda aliyoelezwa, alikuwa amechoka na alisikia kizunguzungu lakini hakutaka kukata tamaa, kila alipoifikiria taswira ya mtoto akiteseka na mume wake amelala katikati ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta roho ilimuuma, akakosa sababu ya kutamani kuendelea kuishi, kwake ilikuwa ni bora afe akijaribu kuokoa aliowapenda kuliko kukaa mahali akiamini yuko salama na kifo kikamkuta mbele ya safari.
“Kila mwanadamu atakufa, watu wa mwaka 1700 wako wapi? Ni bora nife nikijaribu kumwokoa Gilbert na mwanangu Fait…!” aliwaza akizidi kutembea kupita chini ya miti iliyopandwa kando ya barabara, hakuwahi kuwa katika giza la namna hiyo kwa kipindi kirefu, sentensi yake hakuimaliza akawaona vijana watatu wakimfuata kwa kasi wote wakiwa na mapanga, akajua tayari aliyoelezwa yamefika.
“Weee! Wee manzii, unafanya nini huku?” mmoja wao aliuliza lakini Salome hakujibu.
“Mazee, huyu mwanamke mzuri kweli kweli ni lazima tumfaidi!” aliongea mwingine akimmulika Salome kwa tochi usoni na wakazidi kumsogelea, lengo lao lilikuwa kumkamata kisha kumwingilia kwa zamu, Salome alilifahamu jambo hilo mapema na hakuwa tayari. Akirudi kinyumenyume, ghafla alijikwaa na kuangukia mgongo, wakawa wamekwishafika na kusimama juu yake wakimwangalia.
“Ya!Ya!Yaaaa! leo tutafaidi kweli, mwanamuke murembo kama nini, vua!” mmoja wa Mungiki alipaza sauti akiwa ameshikilia panga lake juu, tayari Salome alikuwa ameingia kwenye tatizo jingine.
“Subiri kwanza, subiri niwape kondom, wala msiwe na shaka naweza kuwaridhisha wote!”
“Kweli?”
“Kabisa vueni tu nguo zenu, wala msiniue!”
“Wewe Mtz?”
“Ndio!”
“Hakyanani leo na mimi nimepata Mtz, wacha nivue, naanza mimi!” aliongea mwanaume mrefu mweusi mwenye misuli iliyotuna na kujaa mwili mzima huku akitupa panga lake chini na kuanza kufungua zipu ya kaptura yake, dakika chache tu wote walikuwa utupu wakisubiri kuanza kumwingilia Salome kwa zamu ambaye mkono wake ulikuwa ndani ya mkoba akitafuta kitu ambacho Mungiki waliamini kilikuwa ni kondomu.
“Paaaaa!Paaaa!Paaaa!” ilikuwa ni milio ya risasi, mkono wa Salome ukiwa umenyooka kuwalenga watu hao na wote wakaanguka chini, akanyanyuka mara moja na kusimama wima juu yao kisha kuwaongezea kila mmoja wao risasi nyingine moja.
Bastola ya Gilbert ambayo Salome aliichukua na kuidumbukiza ndani ya mkoba wake kabla ya kuondoka Dar es Salaam ilikuwa imemsaidia! Alimshukuru Gilbert kwa kumfundisha kuitumia kila walipokwenda kuwinda porini.
Mara moja bila kupoteza wakati akaanza kukimbia kwenda mbele, hatua kadhaa tu alishangaa kuona kikundi kingine cha watu wakija nyuma yake tena wakipiga makelele ya mwizi. Moyo wa Salome ulikwenda kwa kasi kuliko mbio alizokuwa akikimbia, jasho jembamba likamtoka na hofu ya kifo ikiwa imemtanda maana alijua kama angeingia mikononi mwa watu hao angegawanywa vipande vipande, kwa sababu walikuwa na hasira ya kuuawa kwa ndugu zao.
Mbele kidogo aliamua kukata kulia baada ya kuona barabara ikishuka chini mahali asikokufahamu, alikuwa katika jiji geni kabisa kwake lakini alilazimika kuwa mwenyeji akijaribu kuokoa maisha. Muda wote akikimbia bastola ilikuwa mkononi akiwa tayari kumshambulia mtu yeyote ambaye angejitokeza mbele yake, tofauti na alivyotegemea kwamba watu waliokuwa wakimkimbiza wangepotea na kuendelea mbele, nao walikatisha kwenye kona hiyo hiyo na kuzidi kumfuata! Ghafla akafika sehemu ambayo macho yake yalikutana na ukuta mrefu, hapo ndipo palikuwa mwisho wa barabara.
“Mungu wangu, nifanye nini hapa? Sitaki kuingia mikononi mwa hawa watu, au nijipige risasi nife badala ya kukamatwa? Kwanini nisife kama Mkwawa?” Salome alijiuliza maswali mengi huku sauti za watu hao zikizidi kukaribia.
“Manzii!” ghafla alisikia sauti ikimwita kutoka nyuma yake, kwa sababu alikuwa peke yake eneo hilo alimanusra azimie sababu ya mshtuko alioupata, alipogeuza shingo yake alikutana na mtu wa ajabu, alionekana kuwa mtoto lakini sauti yake ya mtu mzima.
“Naomba msaada wako, wanataka kuniua!” aliongea Salome akitetemeka baada ya kuwa ameizamisha bastola yake ndani ya mkoba bila kugundulika sababu ya giza.
“Akina nani wanataka kukuua?”
“Mungiki!”
“Mungiki watu mbaya sana, wameua watu mingi sana, kuja huku!” aliongea mtu huyo.
Waliposimama mtu huyo alimfikia Salome chini ya kiuno akamshika mkono na wote wakaanza kutembea kuelekea kwenye ukuta wa pembeni ambapo mtu huyo alishika bati lililoegeshwa ukutani likatokea tundu, akapenya na kuingia ndani kisha kumtaka Salome afanye hivyo, moyo wake ukasita lakini alipozisikia sauti za watu waliokuwa wakimkimbiza zikikaribia, akajikuta amechagua kupenya kwenye tundu hilo na kuanza kumfuata mtu huyo wakiteremka chini kulikokuwa na giza nene.
Alipofikiria maisha ya aliyoishi Dar es Salaam na mahali alipokuwa siku hiyo, akagundua maisha yake yalikuwa katika hatari kubwa kiasi gani, lakini alikuwa tayari kuichukua sababu ya Gilbert na mwanae Faith. Walitokeza kwenye uwanja mkubwa wa wazi, mtu huyo akaketi kwenye tofali kisha kumtaka Salome naye afanye hivyo kwenye tofali jingine ndipo akaanza kumuuliza yeye alikuwa ni nani, kwa jinsi maswali yake yalivyokuwa ya kiutu uzima, Salome alielewa mtu huyo hakuwa mtoto bali mbilikimo.
“Naitwa Salome!”
“Hapa Nairobi watafuta nini?”
“Namtafuta mume na mtoto wangu!”
“Alikuwa akifanya kazi hapa?”
“Hapana!”
“Sasa?”
“Walikuwa safarini kuelekea India kwa matibabu ni mtoto wangu, ndege ilipotua Jomo Kenyatta akitokea Nairobi wakatekwa na Mungiki, hivi sasa sijui walipo na kama wako hai au wamekufa!”
“Mtoto wako alikuwa anaumwa nini?”
“Tundu kwenye moyo, alikuwa akipelekwa India kwa upasuaji!”
“Pole sana dada yangu, nimekuonea huruma sana, mimi pia familia yangu yote imechinjwa na Mungiki, nimekuja hapa kujificha! Sitaki mtu akuue kama ilivyotokea kwa mke na watoto wangu, wameuawa vibaya mno Mungiki waliwakata vipande vidogovidogo kama nyama choma lakini Mungu atawahukumu siku ya mwisho! Sipendi ukutane na hali hiyo” aliongea mtu huyo, kwa sauti yake tu alionekana ni mtu muungwana na mcha Mungu, Salome akawa na imani naye, akaona kweli ameingia mikononi mwa mtu wa Mungu, akahisi usalama.
“Nifuate!” alisema mtu huyo akinyanyuka na Salome akaanza kumfuata kwa nyuma wakizidi kusonga mbele, wakauvuka uwanja wa wazi na kutokea tundu jingine lililokuwepo upande wa pili kwenda nje ambako Salome alishangaa kuona mwanga wa vibatari vingi na sauti za watu wakiongea kwa sauti ya juu na wengine wakiimba nyimbo kama zile alizozisikia wakiimba Mungiki barabarani.
“Nifuate!” akasema tena mtu huyo lakini taa za hatari zilishaanza kuwaka kichwani kwa Salome.
“Tunakwenda wapi?”
“Dada njoo nataka nikakufiche mahali ambako utakuwa salama lakini usijaribu kutoka nje!”
Maneno hayo yalimwondolea Salome wasiwasi na kujikuta akimfuata mtu huyo mgongoni huku wakizidi kusogea mahali kulipokuwa na kelele, ghafla bila kutegemea watu watano wakajitokeza kutoka kwenye nyasi wote wakiwa na mapanga mikononi mwao na kumwamuru Salome akae chini, mtu mfupi aliyekuwa naye akaangua kicheko.
“Ureeee!Ulifikiri wewe ni mjanja? Huwezi kukwepa Mungiki, damu yako ni halali yetu!” akasema mtu huyo na kuukwapua mkoba wa Salome, alipoufungua aliikuta bastola.
“Mama yanguu, kumbe wewe muuaji kama sisi? Sasa leo utakufa kwa mapanga, kwanini hukuitumia hii kuniua mimi badala yake ukakubali kuja huku?”
“Jamani nawaomba msiniue, kama mnataka kufanya hivyo basi nionyesheni mume na mtoto wangu kwanz…!” Salome alisema maneno hayo akibubujikwa na machozi, lakini kabla sentensi yake haijafika mwisho, kibao kizito kikaanguka shavuni mwake, giza likatua machoni na kujikuta akienda moja kwa moja ardhini.
Je, nini kitafuata? Fuatilia siku ya KESHO HAPA HAPA
ENDELEA USHARE NA KUTEMBELEA HAPA KWA SIMULIZI ZOTE UTAZIKUTA HAPA >>www.2jiachie.com/search/label/Simulizi?max-results=7

Post a Comment