ad

ad

BEYOND LOVE- (ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA KWANZA MPAKA YA 10



Beyond love- (Zaidi ya Mapenzi -1)
Tom aliheshimika na kutisha, hakuna mtu aliyechezea shughuli zake kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao na viongozi Serikalini, akiwa mdhamini wa Chama Tawala. Hakuna mtu ambaye hakumfahamu, kila alipopita watu walionyeshana vidole, alikuwa na marafiki wengi kupita kiasi.  Ilipotokea akaa peke yake kwenye baa au hotelini,  ndani ya dakika mbili tayari alishazungukwa na watu,  kila mtu akiagiza alichotaka kutumia, kwa Tom kulipa haikuwa tatizo, fedha alikuwa nayo. Tabia hii ilimfanya awe na wapambe wengi kila alikokwenda,  akilindwa na watu ambao wala hakuwapa kazi hiyo.

Hayo ndiyo yaliwahi kuwa maisha ya Tom, lakini vitu vyote hivyo  havikuwepo tena, vilikuwa vimeyeyuka na yeye kujikuta amelala kitandani kwa miaka mitano bila kuwa na fahamu, akiwa amepooza  mwili wote isipokuwa kichwa tu! Marafiki wote aliokuwa nao walimkimbia, mwanzoni kila mtu alifikiri angekufa wiki ya kwanza lakini akaendelea kuwepo mpaka mwaka ukaisha, ukaja wa pili, hatimaye wa tatu akiwa hana fahamu.  Fedha zote alizokuwa nazo zikiwa zimetumika kumtibu kwenye hospitali mbalimbali duniani bila mafanikio yoyote,  hatimaye mke wake mrembo, Mayasa  Kamani  ambaye kwa hakika walitumbua maisha pamoja wakati wa raha, akaja kumbwaga kwenye Hospitali ya Muhimbili na yeye kuingia mitini akiwa ameuza kila kitu kilichokuwa kimebaki. 



Mama yake Tom,  mjane bibi Bhoke Wambura, ilibidi  asafiri kutoka nyumbani kwao Tarime kuja kumuuguza mwanaye, naye hakudumu sana akawa amefariki kwa ugonjwa wa shinikizo la damu mwanaye akiwa hana fahamu na kuzikwa  na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni kwani  haikuwepo hata senti moja ya kutosha kusafirisha maiti kwenda Tarime, Tom akabaki kitandani peke yake, marafiki zake wala hawakuulizia aliendeleaje na wauguzi wala hawakujishughulisha naye sana wakijua alikuwa ni mtu aliyesubiri siku yake,  kwa miaka miwili zaidi aliendelea kulala kitandani.

Ilikuwa ni asubuhi siku ya Jumapili, wodi ya Mwaisela ikiwa kimya kabisa, wagonjwa wakiwa wametulia vitandani mwao. Mwanamke mwembamba mrefu, afya yake ikiwa imedhoofika alikuwa akimgeuza Tom kitandani ili amwoshe sababu alikuwa amejisaidia kwenye mashuka,  hakuwa muuguzi bali mtu aliyejitokeza kumtunza Tom baada ya kukosa ndugu hata mmoja. Ghafla alishangaa alipomwona Tom amefumbua macho, lilikuwa ni jambo geni kabisa ambalo halikutegemewa kutokea,  akashtuka na kumuachia, Tom akazungusha macho yake huku na kule chumbani na baadaye kumkazia sana macho mwanamke huyo.

“Wee Malaya nani amekuambia uje nyumbani kwangu? Hivi wewe mwanamke husikii? Nilishakuambia sikupendi kwanini unanifuatilia? Ondoka hapa, Mayasa akikuta utasema nini? Unataka kunichonganisha na Mayasa wangu? Ondoka upesi vinginevyo nitakupiga!” Tom aliongea akijaribu kunyanyuka kitandani, akashindwa,  hapo ndipo akagundua hakuwa na hisia hata kidogo kuanzia shingoni hadi miguuni,  hakuelewa ni kitu gani kimetokea.

“Tom! Tulia kwanza, huelewi kilichotokea ndani ya miaka mitano iliyopita, niko hapa kitandani kwako kwa sababu nilichonacho moyoni juu yako ni zaidi ya neno nakupenda, zaidi ya mapenzi; This is Beyond Love!” Aliongea mwanamke huyo akibubujikwa na machozi.

Tom hakuwa na habari juu ya kilichotokea maishani mwake,   hakuelewa alikuwa amelala kitandani bila fahamu kwa muda wa miaka mitano, fikra zake zilimtuma kuhisi alikuwa amelala kitandani nyumbani kwake mahali ambako alishampiga marufuku Mariam kufika. Alipozungusha macho yake huku na kule ndani ya chumba alicholala, aliwaona watu wengine wakiwa juu ya vitanda na harufu ilikuwa mbaya tofauti kabisa na nyumbani kwake, akaelewa alipokuwa amelala ni hospitali,  mara moja akaanza kuzivuta kumbukumbu zake juu ya kilichotokea mpaka akajikuta  yuko mahali pale.

Picha iliyokuwa kichwani mwake kwa haraka, aliyoikumbuka kama kitu kilichotokea mwisho ni yeye akiwa ndani ya gari lake aina ya Vogue, akiwa amefunga vioo vyote huku akipulizwa na kiyoyozi, muziki laini  uitwao Hello wa mwanamuziki Lionel Richie ulikuwa ukipigwa taratibu kutoka kwenye spika ambazo hazikuonekana. Shingoni alikuwa amevaa mkufu  uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa dhahabu, rubi  na Almasi ambao thamani yake ilikuwa milioni ishirini na tano.

Si hivyo tu, usoni kulikuwa na miwani ya jua kutoka Kampuni ya DG, thamani yake ikiwa ni milioni  moja saa yake ilikuwa ni ya milioni   tano, nywele zake zilikuwa zimetengenezwa na kuwekewa dawa iliyozifanya zimeremete na kuwa na mawimbi, alipojiangalia kwenye kioo  kilichokuwa juu mbele yake  kwenye gari,  alitabasamu na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomuumba akiwa kijana mwenye kuvutia,  yeye mwenyewe aliamini hakuwepo mwanamke wa  kupindisha kama  angeamua kumtokea.

Akijiangalia kupitia kwenye kioo hicho, alifanikiwa kuona gari  nyeusi aina ya Rav 4  ikija nyuma yake, hakutilia maanani sana akiamini   mwenye gari alikuwa na safari zake na alipojaribu kuangalia vizuri, alimwona msichana mzuri akiwa amekaa nyuma ya usukani.

Tom alizidi kukanyanga mafuta gari hilo likimfuata  kiasi cha mita  kumi tu nyuma yake mpaka akafika kwenye lango la kuingilia kwenye jumba lake la kifahari eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam,  akakanyaga breki na kubonyeza  kitufe fulani kando ya mlango ili lango kuu lifungunge aingize gari lake, ghafla bila kutegemea kabla hajakanyaga moto, lango likiwa wazi,  alishangaa kuwaona watu wawili waliovaa kininja wakiwa wamesimama kila upande wa gari lake, mmoja akipigapiga dirishani  na kumwomba afungue,  mshtuko mkubwa ulimpata, akaanza kutetemeka akiwa hajui nini cha kufanya.

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie
Akiwa katika hali hiyo akifahamu kabisa alikuwa ametekwa, mmoja wa watu hao waliotoka kwenye gari lililokuwa nyuma yake, alikipiga kioo cha dirisha kwa kitako cha bunduki, chote kikavunjika na  Tom   kuwekewa mdomo wa bunduki aina ya SMG shingoni.

“Ndugu yangu, naomba usiniue kama ni gari chukua, niachie roho yangu niko tayari kukuongezea  na vito vyote vya thamani nilivyovaa na hata fedha ya mafuta kama utahitaji!”
“Sihitaji fedha yako, nimefuata roho yako!”
“Nani amekutuma?”
“Hilo sio swali!”

Kilichofuata baada ya hapo ni milio miwili ya risasi, moja ikazama kichwani kwa Tom na nyingine shingoni,  akaanguka kwenye kiti huku akitokwa damu nyingi.  Majambazi wakamchukua na kutupa nje ya gari, wote wawili wakaingia ndani na kuondoka na gari lake kwa kasi ya ajabu,  Tom akiachwa amelala ardhini akivuja damu nyingi bila kuwa na fahamu, wakati hayo yakitokea ilikuwa ni saa tatu na nusu ya usiku kwani  alikuwa akiwahi nyumbani kuangalia taarifa ya habari ya  ITV, saa nne kamili.

Hiyo ndiyo ilikuwa kumbukumbu ya mwisho iliyomwijia kichwani mwake baada ya kujaribu  kukumbuka ilikuwaje akawa hospitalini, kichwani mwake alifikiri  tukio  la kuvamiwa lilitokea jana yake kumbe alikuwa amelala kitandani kwa miaka mitano mfululizo bila kuwa na fahamu akiwa amezungushwa huku na kule duniani kutafuta matibabu, Uingereza, Marekani, Ujerumani,  India kote walishindwa kumsaidia ndipo akarejeshwa nyumbani Tanzania,  mkewe Mayasa akambwaga hospitali ya Muhimbili na kutokomea akiwa ameuza kila kitu na kumwacha masikini.

“Yuko wapi  mke wangu mpenzi Mayasa?”
“Mayasa hakukupenda wewe Tom,  alipenda mali zako, zilipokwisha akaamua kukukimbia, mimi niko hapa  pembeni mwa kitanda chako kwa sababu niliyokueleza, la kwangu ni zaidi ya penzi!” Aliongea Mariam akilia  kwa uchungu, kumbukumbu za mambo yote ambayo Tom alimfanyia zilimwijia, akamwangalia na hasira ikapanda, lakini akakumbuka neno la mwisho alilolisema kabla hajatoka porini kwamba “Nimemsamehe Tom!”
Je, nini kilitokea katika maisha ya watu hawa?

Beyond love -2

Hali ilikuwa ya utulivu jijini Dar es Salaam,  watu wengi walikuwa wakirejea majumbani mwao kutoka kazini,  giza lilishaanza kuingia. Katika wakati kama huo watoto wengi maeneo ya Vingunguti, Manzese, Tandika na kwingineko walikoishi watu wenye maisha ya  kawaida, walikuwa wakioshwa tayari kwa chakula cha  usiku na kwenda kulala, ndio maana vilio vya watoto wengi ambao hawakutaka kuoga vilisikika, labda siku ambayo  kwenye nyumba nyingi ulipikwa wali, siku hiyo hakuna mtoto aliyelia, akiogopa kuambiwa ‘mpelekeni akalale’

Nyumbani kwa mzee Maftah Abdallah,  aliyekuwa na nyumba kubwa yenye vyumba zaidi ya kumi na tano vilivyojaa wapangaji hali ilikuwa tofauti, watoto walikuwa bado wakicheza na kukimbizana huku na kule uwani, miongoni mwa watoto hao alikuwepo Mariam na Thomas, Mariam akiwa mtoto wa mwenye nyumba na Tom akiwa mtoto wa  bwana  Chacha, mpangaji aliyefanya kazi ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi, kilichokuwepo huko huko Vingunguti.

“Tucheze mchezo wa baba na mama, mimi mama wewe baba!” ilikuwa ni sauti ya Mariam akimwambia Tom, ambaye hakukubaliana na mchezo huo, badala yake akawaita watoto wengine wa wapangaji waungane nao kucheza mchezo wa kujificha na kutafutwa, maarufu kwa jina la kombolela, watoto wote wakakubaliana, Mariam akatakiwa kujifunika na viganja vyake machoni na watoto wengine wote wakaenda kujificha, Tom akajificha kwenye nyumba ya kuku.

“Tiari bado?” Mariam aliuliza.
“Bado” watoto wengine ambao walikuwa bado hawajajificha waliitikia.
“Tiari bado?”  Mariam akapataza sauti na kuuliza  tena mara ya pili,
“Tiari!” Sauti za watoto  zilisikika kutoka sehemu mbalimbali walizokuwa wamejificha, akaanza kuwatafuta mmoja baada ya mwingine, ndani ya  muda wa nusu saa alishawaona wote lakini akabaki Tom peke yake, Mariam hakukata tamaa akizunguka huku na kule kufunua kila sehemu  akimtafuta lakini hakumpata mwisho giza  likazidi kuingia, watoto wengine wakaanza kuchukuliwa na wazazi wao kwenda kuoshwa.

“Labda kwenye nyumba ya kuku?” Alijiuliza Mariam ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka  saba, mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Vingunguti na Tom miaka kumi mwanafunzi wa darasa la pili katika shule hiyo hiyo.

Taratibu akaanza kuisogelea nyumba ya kuku, ndani yake hapakuwa na kuku hata mmoja, wote walishakufa, akapiga magoti chini na kuanza kutambaa akiingia ndani yake, macho yake hayakuamini alipomwona Tom amelala kwenye kona,  akataka kupiga kelele kuashiria kwamba amemwona, kabla hajafanya hivyo kiganja cha Tom tayari kilishaufunika mdomo wake kuzuia asiseme chochote.

“Mimi baba wewe mama, sawa?”
“Sawa!”
“Tulale kama vile baba na mama!”
“Sawa!”

Karibu wapangaji wote wa mzee Maftah walikuwa na chumba kimoja,  wakiwa wamegawa katikati kwa pazia  ili watoto walale upande wa pili, kwa wenye mtoto mmoja kama ilivyokuwa kwa  Chacha na mkewe,  hawakuona sababu ya kufanya hivyo, walilala na mtoto wao chumba kimoja wakijidanganya kwamba walikuwa ni watoto wadogo wasioelewa chochote, jambo ambalo halikuwa na ukweli, katika umri wa miaka kumi, Tom aliona kila kitu ambacho wazazi wake walifanya usiku wakiamini yuko usingizini na  hicho ndicho alitaka kukifanya na Mariam. Akapanda juu yake.

“Mariaaam!Mariaaaam!Mariaaaam!” ilikuwa ni sauti ya Bi.  Mwamtumu Maftah, mke wa baba mwenye nyumba akimtafuta mwanae wa mwisho ili aoge,  Mariam hakuitika, aliendelea kubaki kimya Tom akiwa juu ya kifua chake, bila kuelewa jambo alilokuwa akifanya, kwao kilichokuwa kikitokea ni kuwaigiza baba na mama bila kuelewa maana  yake.
“Mariaam!” aliendelea kuita lakini sauti ya mtoto wake haikusikika.

Ghafla akipita kando ya  kibanda cha kuku alisikia minong’ono ya watoto “baba Khadija, niachie mwenzio watoto hawajalala” moyo wake ukashtuka, akarudi kinyumenyume mpaka kwenye kibanda hicho, akasikia sauti ya mtoto wa kiume “Wewe mama Tom, ritomu rimesharara, sogea huku” hiyo ilikuwa ni sauti ya Tom akimwigiza baba yake, mama yake Mariam hakuyaamini masikio yake baada ya kuhakikisha kabisa kwamba ni binti yake mdogo wa miaka sita na mtoto wa mpangaji wake walikuwa ndani ya kibanda cha kuku wakifanya mambo  yasiyolingana na umri wao, akakimbia mbio hadi ndani kumwita mume wake.

“Hebu sikiliza mwenyewe kinachoendelea ndani ya hiki kibanda!” alimwambia mume wake ambaye baada ya kutega sikio, naye pia hakuamini, lilikuwa ni jambo la ajabu mno, hasira zikampanda.
“Hebu  kawaite wazazi wa Tom, huyu mtoto wao atatuharibia mwanetu, mtoto ana miaka kumi keshaanza mambo haya? Wallah hatumtaki ndani ya nyumba yetu, lazima wahame!”

Mzee Chacha  na mkewe walipoitwa hata wao hawakuamini  walichokiona, walishindwa kuelewa ni lini  Tom alikuwa amejifunza jambo la hatari kiasi hicho,  alikuwa mdogo mno kuelewa mambo ya watu wakubwa,  hawakuwa na habari kwamba kila kitu walichokifanya chumbani wakidhani amelala yeye alikiona na ndicho alichokuwa akikifanyia kazi.

“Hizi nyumba zetu za kupanga hizi? Kulala chumba kimoja na watoto ni balaa,  inaleta shida sana kwenye  malezi!”
“Unaongea kitu gani wewe Chacha,  kwa hiyo unataka kutoa kisingizio kwamba nyumba ya kupanga ndio imefanya mwanao atake kuniharibia binti yangu? Usinitanie, jiandaeni kuhama, siwataki tena kwenye nyumba yangu!”  mzee Maftah alifoka,  Chacha na mkewe wakaweka mikono yao midomoni kwa mshangao, hakuamini kauli waliyoisikia kama kweli ililingana na kosa lililofanywa na watoto.

 Maneno hayo hayakuwa utani,  mzee Maftah aliandika notisi na kuwakabidhi siku hiyo hiyo akiwataka wahame ndani ya nyumba yake. Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali suala likawa ni wapi wangehamia, miezi mitatu baadaye notisi yao  ilipokwisha walihamia kwenye nyumba nyingine jirani kabisa na shule ya msingi Vingunguti, mwendo wa  dakika tano tu kufika shuleni, Tom akafurahi lakini akiwa na masikitiko mengi moyoni mwake sababu ya kutenganishwa na Mariam, alikuwa amezoea sana kucheza naye.

Mzee Maftah na mkewe walifikiri kuwatenganisha Tom na Mariam ingesaidia, jambo ambalo halikuwa kweli, ukaribu wao uliendelea kama kawaida wakiwa shuleni! Waliongea,  walicheza na kufurahi pamoja lakini hawakudiriki tena kufanya mambo yaliyowasababisha wachapwe,  Tom aliogopa mno, alama za fimbo bado zilikuwepo mwilini mwake na kila siku aliporejea  nyumbani alionywa na wazazi wake kutojishughulisha na mambo hayo tena, akipewa kila aina ya vitisho ili aogope tendo la ndoa, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mariam, naye alitishwa kupita kiasi.

Kwa miaka mitano   iliyofuata  mpaka Tom anamaliza darasa la saba, hawakuwahi kabisa kuongelea suala la mapenzi. Akafaulu kuendelea kidato cha kwanza kwenye shule ya sekondari Ukonga, hapakuwahi kutokea mwanafunzi mwingine aliyefaulu vizuri kiasi hicho,  alisifiwa na kila mwalimu, alipewa zawadi mbele ya wazazi na wanafunzi wote na wakatakiwa waige mfano wake! Ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa mzee Chacha na mkewe  kusimamishwa mbele ya wageni wote waalikwa   siku  ya  kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu.
“Hongera sana Tom!” Mariam alimwambia baada ya sherehe hiyo.

“Ahsante! Inabidi pia wewe uongeze bidii, una uwezo wa kufanya vizuri, jiepushe na mambo  yaliyosababisha tukachapwa  baada ya kufumwa kwenye nyumba ya kuku, si unakumbuka?”
Badala ya kujibu Mariam alitabasamu na uzuri wote wa sura yake ukaonekana, kimoyomoyo Tom akakiri kwamba Mariam alikuwa msichana mzuri na kuweka ahadi kwamba kama akifanikiwa kufanya vizuri katika masomo yake na kufika Chuo Kikuu hatimaye kupata kazi nzuri angemuoa, hakutaka kuyaweka maneno hayo wazi, alitaka kila kitu kibaki siri mpaka wakati muafaka ufike.

“Nitajitahidi sana kufuata nyayo zako Tom!”
Sababu ya umasikini hata kutimiza mahitaji ya shule, ilikuwa ni kazi ngumu kwa Tom,baba yake alijitahidi kufanya mpaka kazi za kuzibua mitaro  akafanikiwa kupata ada peke yake, mpaka zikiwa zimebaki siku nne shule ifunguliwe, Tom alikuwa hajapata sare za shule na godoro. Hakuwa na mahali pa kukimbilia, ikabidi amfuate Mariam na kumwelezea kilichotokea, msichana huyo akamchukua mpaka kwa baba yake na kulia akiomba amsaidie, kwa kumwonea huruma mtoto wake, mzee Maftah alimnunulia Tom mahitaji yote yaliyobaki na kuondoka kwenda shule siku  nne baadaye.

“Nakushukuru sana Mariam, bila wewe sijui kama ningekwenda shule, nitaukumbuka sana mchango wako maisha yangu yote!”
“Usijali, nahisi moyoni mwangu kuna upendo wa aina fulani kwako Tom!”
“Kweli?”
“Kabisa”
“Basi tuangalie kitu gani Mungu ataleta  mbele ya safari”
Je, nini kitaendelea?

Beyond  Love -3

Mariam alikuwa amefanya ndoto yake itimie, kwa Tom alionekana  ni malaika mkombozi kwani bila yeye asingeweza kuendelea na masomo ya sekondari. Akamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, nyumbani aliwasimulia wazazi wake jinsi alivyopata msaada, hata wao hawakuwa tayari kuamini kama baba yake Mariam aliyewafukuza kwenye nyumba sababu Tom na Mariam walikutwa ndani ya nyumba ya kuku wakicheza mchezo wa baba na mama ndiye aliyempa fedha mtoto wao  kukamilisha   mahitaji yote ya shule.

Tom alisindikizwa na wazazi wake hadi Ukonga na kukabidhiwa  kwa walimu wake,  ulikuwa ni mwanzo mpya wa maisha. Kwa alivyokuwa amevaa, haikuhitaji maelezo yoyote kuelewa alikuwa ni mtoto wa masikini. Alibezwa na kupuuzwa na wanafunzi wenzake wengi wao wakiwa ni watoto wa matajiri jijini Dar es Salaam,  hii ilimtia Tom hasira na uchungu lakini hakutaka kulipiza kwa mtu yeyote, nguvu zake zote zikaishia kwenye masomo ingawa alitengwa na wanafunzi wenzake.

Miezi mitatu baadaye  walipofanya mitihani ya majaribio,  matokeo aliyopata Tom yaliwashangaza walimu mpaka wanafunzi, alishika namba moja, akiwa amepata alama mia moja katika kila somo! Heshima ikaanza kupanda, wanafunzi wakaanza kumsogelea na kumfanya rafiki wakimtaka msaada. Hakuwa na kinyongo,  alikuwa tayari kumsaidia kila  mwanafunzi aliyemwomba kitu bila masharti yoyote, idadi ya marafiki ikaongezeka na  Tom akazoea shule ingawa hakumwondoa Mariam katika akili yake, kila siku alikuwemo, alimuwaza wakati wa kula, kunywa na kulala! Alikuwa ni mtu muhimu sana kwake.

 Shule ilipofungwa alirejea nyumbani kwa wazazi wake, baba yake alikuwa  bado akiendelea na kazi ile ile ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi na  mama yake alifanya kazi ya kuponda kokoto, hiyo ndiyo kazi ambayo Tom alichagua kufanya ili kupata fedha za matumizi shule ikifunguliwa. Kila siku asubuhi aliondoka nyumbani na mama  yake kwenda  sehemu  ilipokuwa ikijengwa barabara na kuchukua mawe kisha kuyasomba hadi karibu na nyumbani kwao ambako walianza kuyaponda kwa kutumia nyundo,   kila siku Tom alifanya kazi hiyo na mama yake bila kuchoka.

“Mama kazi hii mpaka lini?”
“Hatuna jinsi mwanangu!”
“Lakini nitakuja kuwapumzisha wazazi wangu,  kwani mmehangaika muda mrefu sana!”
“Jitahidi tu kusoma mwanangu!”
“Nitafanya hivyo mama!”

Alitamani sana kumwona Mariam lakini akaogopa kwenda kwao, kumbukumbu za kusababisha wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba bado ziliendelea kuishi akilini mwake,  lakini mwisho alipokumbuka wema wa Mariam na wazazi wake walipompa fedha za mahitaji ya shule, aliamua kuweka hofu pembeni na kumuaga mama yake asubuhi moja  na kutembea kwa miguu hadi nyumbani kwao, ilikuwa siku ya  Jumapili, ambaye hapakuwa na uwezekano wa Mariam kutokuwepo nyumbani.
“Shikamoo mama!” alimwamkia mama yake.
“Marahabaaaa…nani huyu? Tom?”
“Ndio mama”
“Karibu mwanangu habari za shule?”
“Nzuri tu mama”
“Umeongezeka urefu!”
“Ahsante mama! Hamjambo hapa nyumbani?”
“Hatujambo!”
“Mama nimekuja kuwapeni shukrani zangu kwa wema mlionitendea! Sijui baba yupo?”
“Hapana ametoka asubuhi, usijali sana, tulikuwa tukitimiza wajibu, mbona sisi tulishasahau?”
“Mimi nakumbuka mama,  nimemkuta Mariam?”
“Yupo…Mariaam!” alijibu mama huyo na kuanza kuita.
“Bee mama!” sauti ya Mariam ilisikika kutoka ndani.
“Njoo huku nje una mgeni!”

Ukimya ukatokea, baadaye Mariam akatokeza nje,  alipomwona Tom furaha ilimjaa, akaruka juu na kushangilia huku akimkimbilia lakini alipomfikia alishindwa kumkumbatia baada ya kuona macho ya mama yake yakimwangalia kama vile alitaka kujifunza kitu! Wakashikana mikono na kusalimiana kwa heshima,  kama alivyofanya kwa mama yake, Tom pia akamshukuru Mariam kwa wema aliomtendea na kumtaarifu kwamba alikuwa amefunga shule  lakini alikuwa akiendelea vizuri, pia akachukua kadi yake ya matokeo na kumwonyesha.

“Umekuwa wa kwanza?”
“Ndio!”
“Amekuwa wa ngapi?” mama aliuliza.
“Wa kwanza mama,  Tom ana akili sana, hongera!”
“Ahsante,  wewe unaendeleaje?”
“Vizuri ingawa sikuwa wa kwanza, nilishika nafasi ya kumi!”
“Hongera pia, jitahidi mpaka uende sekondari!”
Waliongea mengi lakini mama hakutaka kuondoka, alikuwepo kusikiliza kila kitu kilichotoka midomoni mwao, Tom alipoaga mama  hakumruhusu Mariam kumsindikiza, wakashikana mkono na akaondoka kurudi ndani huku akimshuhudia Tom akitembea kwenda nyumbani kwao, fikra  za mapenzi zilikuwa zikijengeka ndani ya mioyo ya watoto hao, hakuna kilichokuwa kimebadilika siku walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku, pamoja na   kuwatenganisha baada ya   wazazi wa Tom kufukuzwa nyumbani kwa baba yake Mariam walipokuwa wamepanga, bado waliendelea kupendana.

Nyumbani Tom alimsimulia mama yake kila kitu wakiponda kokoto,  siku hiyo kazi hazikufanyika sawasawa, akili  yote ikiwa kwa Mariam. Alimfikiria kila aliponyanyua nyundo juu na alimfikiria kila aliposhusha chini na kuvunja jiwe, ubongo wake ulijaa neno “Mariam!Mariam!Mariam” aliamini kwa upendo aliokuwa nao,  huyo ndiye msichana aliyemfaa hata baadaye katika maisha yake, ingawa alikuwa bado ni mtoto mdogo alijikuta akifikiria hivyo akiamini upendo aliokuwa nao Mariam ulikuwa ni wa kweli, mtoto wa tajiri kumpenda masikini halikuwa jambo rahisi kukutana nalo.

Maisha yakaendelea, mara kwa mara Mariam akielekea  kwenye masomo ya ziada alipita sehemu ambapo Tom na mama yake waliponda kokoto, alimwonea huruma lakini hakuwa na jinsi ya kumsaidia zaidi ya kuchukua sehemu ya nauli yake na kumwachia ili yeye na mama waitumie kununua chakula au maji. Ulikuwa ni upendo wa ajabu,  hata mama yake Tom alikiri kwamba Mariam alikuwa na moyo tofauti kabisa na watoto wengine wa matajiri aliowafahamu.
“Kwa jinsi baba yake alivyo na majumba mengi hapa Dar es Salaam, lazima angekuwa na  maringo ya kutisha!”
“Hayuko hivyo mama, ana moyo wa huruma sana Mariam!”
“Basi endeleeni na uhusiano huo huo, msigombane wala usije ukamuudhi!”
“Sawa mama!”

Shule zilipofunguliwa Tom aliagana na Mariam na kurejea shule ambako kazi ilikuwa  ni moja tu; kusoma ili kulinda heshima aliyokuwa nayo  na pia aliamini hiyo ndiyo njia pekee ya kumfikisha juu na kuendelea kuheshimiwa  zaidi na jamii iliyomzunguka hata akiwa mkubwa, hakutaka maisha kama ambayo yeye na wazazi wake waliishi,  alipenda sana kubadili historia, awe mtoto wa masikini aliyefanikiwa na kuwatia moyo watoto wengine ambao wangekuwa katika maisha kama ya kwake ili kuonyesha kwamba mafanikio ni ya kila mtu.

Utaratibu uliendelea kuwa ule ule,   nafasi ya kwanza ilikuwa ni ya  kwake mpaka anamaliza kidato cha kwanza na kuingia cha pili, kila mtu alimpenda, walimu walimfurahia na waliamini kabisa  ni yeye ndiye angeweza kuiletea heshima shule yao kwenye mitihani ya kidato cha nne kama angeendelea na kasi hiyo hiyo. Kidato cha pili kilikuwa kizuri sana kwake, hasa kwa kuwa pia Mariam alikuwa amefaulu na kujiunga na shule hiyo hiyo kwa kidato cha kwanza, yeye ndiye akawa mwenyeji wake. Furaha ikawa imeongezeka, wasichana wote walioonekana kuwa karibu naye wakimtaka mapenzi, hakusita kuwatambulisha kwa Mariam ili wajue  Paka alikuwa ameingia, Panya wote waondoke.
“Huyu ndiye Mariam uliyekuwa  ukimwongelea?” wasichana waliuliza.
“Ndio”
“Ni mzuri!”
“Ahsante, hata mimi najua” Tom alitania.



Urafiki wao ulizidi kukomaa na matatizo ya Tom  kiuchumi yakapungua kwani Mariam alimsaidia kwa kila kitu,  kila alichotumiwa iwe ni chakula, dawa ya meno  ama fedha waligawana na kutumia pamoja. Shukrani zake kwa Mariam alizitoa kwa njia ya kumfundisha masomo aliyoyapitia kidato cha kwanza, yeye pia akaanza kufanya vizuri akashika namba moja kwenye kila mtihani, hii iliwafurahisha sana wazazi wa Mariam kiasi kwamba  kila walipokuja shuleni kuwatembelea ilikuwa ni lazima waonane na Tom kumpa shukrani zao.
“Tunakushukuru sana Tom na  tunaomba utusamehe kwa yote yaliyotokea ukiwa mtoto mdogo nafikiri wazazi wako huwa wanaliongelea sana suala hili nyumbani!”
“Yalishapita wazazi, ulikuwa utoto tu ule!”
“Basi ni vyema endeleeni hivyo hivyo, kila tutakachomtumia Mariam pia kitakuwa cha kwako!”
“Ahsante mama!”

Hiyo ikawa kama ni ruhusa kwao,  mapenzi yakaongezeka ingawa hawakudiriki hata siku moja kubusiana wala kufanya ngono na  hakuna kati yao aliyewahi kumwambia mwenzake anampenda kingono! Walikuwa  marafiki wa kweli ambao kwao neno “Mapenzi” lilikuwa ni zaidi ya kufanya tendo la ndoa, mwaka wa kwanza ukapita wakiwa pamoja, hatimaye ukaja wa pili, Tom akaingia kidato cha nne na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yake kuliko  ilivyokuwa kwenye vidato vilivyotangulia,  walimu wote walimtegemea yeye kupeperusha bendera ya shule ya sekondari Ukonga Kitaifa, nafasi ya kwanza Tanzania nzima iliaminika kuwa yake.
“Tom!”
“Yeah!”
“I am so proud of your success!” (Najivunia mafanikio yako!)
“Thanks!” (Ahsante)
“And I know you are going to perform well in your final exams!” (Na ninajua utafanya vizuri kwenye mitihani yako ya mwisho!)
“I know! My mind is  stronger than any challenge ahead” (Najua, akili yangu ni imara kuliko changamoto yoyote mbele yangu!)
“Today I want to tell something!” (Leo nataka kukuambia kitu)
“What is it girl?” (Nini hicho?)
“NAKUPENDA!”
“Najua unanipenda na mimi nakupenda pia!”
“Sikupendi kama tunavyopendana!”
“Unanipendaje?”
“Vile kivingine!”
“Kivingine aje?”
“Tom!”
“Sijakuelewa!”
Je, nini kitaendelea?

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Beyond Love -4

Mariam alitumia uwezo wake wote wa kujieleza akijaribu kukitoa kilichokuwemo ndani ya moyo wake ili Tom aweze kuelewa ni  kiasi gani alimpenda na alihitaji nini kutoka kwake lakini bado Tom alimkatalia, hakuwa tayari kabisa kujiingiza katika uhusiano zaidi ya uliokuwepo, bado aliikumbuka picha ya tukio la utotoni  walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku wakiigiza kufanya mapenzi, jambo lililosababisha yeye na wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba ya wazazi wa Mariam kwenda kupanga sehemu nyingine, bado taswira ilikuwemo kichwani na ilimfanya amwogope Mariam, hakuwa tayari kukororofishana tena na wazazi wake waliojitolea kuwa wafadhili wa masomo yake kwa miaka yote aliyokaa shuleni.

“No!No Mariam, we cant be more than this!” (Hapana! Hapana Mariam,  hatuwezi kuwa zaidi ya hapa)
“Think twise darling!” (Fikiria mara mbili mpenzi)
“Even if I think about it a dozen times it won’t change a thing!” (Hata nikifikiria mara kumi na mbili, bado haitabadilisha chochote!)
“I love  you Tom, with all my heart, please accept me as your lover!” (Nakupenda Tom,  kwa moyo wangu wote,  tafadhali nipokee kama mpenzi wako!)
“It is not possible darling, let’s just remain good friends, helping one another to achieve our dreams!” (Haiwezekani mpenzi,  tuendelee kuwa marafiki,  tukisaidiana kutimiza ndoto zetu!)
“I know, but …!(Najua lakini…)
“That is the truth!” ( Huo ndio ukweli) Tom alisisitiza.

Wote wawili walikuwa bado bikra, mpaka wakati huo Tom akiwa kidato cha nne na Mariam cha tatu, walikuwa bado hawajakutana na mtu  yeyote kimwili! Halikuwa jambo rahisi sana kwa mtu kuamini, lakini huo ndio ulikuwa ukweli, Tom alikuwa amedhamiria kuutunza mwili wake kama ilivyokuwa kwa Mariam mpaka watakapomaliza Chuo Kikuu,  wote wawili wakiwa wamesahau kwamba miili yao ilikuwa ikikua na mihemko kuongezeka,  kilichokuwa kikimtokea Mariam hakikuwa ridhaa yake ni  mabadiliko ya mwili  yaliyokuwa yakimsukuma, alihitaji sana kufanya tendo la ndoa na mtu pekee wa kufanya naye hakuwa mwingine isipokuwa Tom, alimpenda kwa moyo wake wote.

Kumkatalia msichana mwenye umbile na sura nzuri kama Mariam ilihitaji moyo, haikuwa rahisi sana kwa vijana wengi  hasa wa umri kama aliokuwa nao Tom, yeye pia mwili wake ulikuwa ukichemka ni kweli alivutiwa na Mariam kwa kila kitu lakini alijitahidi kadri ya uwezo wake kupambana na hisia zote zilizokuwa zikimpata, Mariam alikuwa mzuri, kuanzia juu hadi chini hapakuwa na mahali pa kumkosoa na  kila alipopita mbele ya kundi la wavulana walionekana kupagawa, hakika alikuwa na mvuto wa kutisha, huo ndio ambao Tom alikuwa akipambana nao.

Hakustahimili sana jambo hilo, mwezi mmoja baadaye alijikuta amepunguza msimamo na kuruhusu angalau kuwa wanabusu kwenye kona usiku baada ya  kujisomea, hii ilikuwa ni faraja tosha kwa Mariam aliyeamini lazima nia aliyokuwa nayo ingetimia! Kila siku usiku ilikuwa ni lazima wafanye jambo hilo kabla ya kwenda kulala,  jambo pekee ambalo Tom hakuwa tayari kulitenda ni ngono.

“Siwezi Mariam, nilishaweka nadhiri ya kutokukutana na mwanamke mpaka niingie Chuo Kikuu!” alimwambia Mariam siku moja wakiwa gizani kabla ya kwenda kulala,  alikuwa akishinikiza wakutane kwenye choo cha shule na kufanya tendo hilo.

“Kidogo tu! Wala haitachukua muda, nakupenda Tom tafadhali kubali!”
“Unaweza kupata mimba halafu wazazi wako wakanichukia tena! Huyo ni shetani Mariam lazima upambane naye, ukimruhusu sana hutamaliza masomo yako, ni afadhali umekutana na mimi ninayeweza kukupa ushauri!”
“Nina kondomu, tutaitumia!”
“Umeitoa wapi?”
“Nilipewa na msichana mmoja darasani kwetu!”
“Hata kama una kondomu siwezi kukubali,  tendo la ndoa kabla ya ndoa ni dhambi!”
“Tom utabaki kwenye msimamo huo  mpaka lini? Mbona wenzetu wanafanya na wanafunzi wengi pia wananifuata mimi nakataa?”
“Naomba uendelee kukataa hivyo hivyo, hiyo ni kwa faida yako!”

Msimamo wa Tom uliendelea kubaki huo huo mpaka mwisho wa muhula ukafika, shule ikafungwa na wote wakarejea nyumbani. Alijisikia mshindi moyoni mwake baada ya majaribu makubwa ya Mariam ambaye tayari alishaanza kuonyesha chuki kwa sababu ya kukataliwa. Wakiwa nyumbani waliendelea kuwasiliana kama kawaida,  wakienda kwenye masomo ya ziada pamoja, wazazi wa Mariam walimfurahia na Tom, hawakuwa na wasiwasi naye kwa kitu chochote, wakiamini  angemsaidia mtoto wao kutimiza ndoto bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea kichwani mwa Mariam.

Usiku wa manane wiki moja kabla shule haijafunguliwa, Tom alizinduliwa usingizini na kelele za mlango ukigongwa, aliposikiliza vizuri ilikuwa ni sauti ya mama yake.  Halikuwa jambo la kawaida mama  yake kumgongea usiku,  ilipotokea kuna shida ni baba aliyekwenda chumbani kwa Tom kumwamsha, hii ilimshtua na kumfanya anyanyuke haraka kwenda kufungua mlango akiwa amevaa bukta tu.
“Vipi mama?”
“Imebidi tu nikuamshe!”
“Kwani kuna nini?”
“Baba yako!”
“Kawaje? Kalewa halafu anakupiga?” Tom aliuliza kwa mshangao, mara kadhaa huko nyuma ilipotokea baba yake akanywa pombe nyingi alimfanyia fujo mama na hata kufikia hatua ya kumpiga jambo ambalo Tom hakulipenda hata kidogo.
“Hapana anaumwa!”
“Anaumwa?”
“Ndio!”
“Nini?”
“Mkojo umekataa kutoka  anasema tangu jana  mchana, walinzi wenzake wamemrudisha kutoka kazini!”

Tom hakuongea zaidi, wala kuuliza chochote alichokifanya ni kuchomoka chumbani na kupita sebuleni akielekea chumbani kwa wazazi wake, nyumba yao ilikuwa ni ya vyumba viwili na sebule. Halikuwa jambo la kawaida kwake kuingia chumbani kwa wazazi wake lakini siku hiyo alilazimika kufanya hivyo, akamkuta baba yake amelala sakafuni akitupa miguu huku na kule na kulalamika maumivu ya tumbo,  mwili wote ulikuwa umelowa jasho, akitua harufu kali ya mkojo! Ingawa alijua kabisa  Tom hakuwa na uwezo wa kumsaidia alianza kulia akiomba ampunguzie maumivu, hali ilimchanganya Tom, akamgeukia mama yake aliyekuwa akilia.
“Mama tufanyeje?”
“Twende hospitali!”
“Tutapata wapi daladala saa hizi?”
“Sijui!”
“Tusaidiane kumbeba mpaka stendi, Mungu atajua huko huko!”
“Sawa mwanangu!”

Wakakubaliana, mzee Chacha alikuwa mzito sana kwao lakini walijitahidi kadri ya uwezo wao na kumbeba juu juu wakipita kwenye madimbwi ya maji sababu mvua kubwa ilikuwa imenyesha jijini Dar es Salaam siku hiyo. Njia nzima  mzee Chacha alikuwa akilia kama mtoto mdogo, hata hivyo wakafanikiwa kufika stendi na kumlaza chini, tayari ilikuwa saa tisa na nusu za usiku kwa mujibu wa saa ya plastiki ambayo Tom alikuwa amevaa mkononi, kila gari lililopita walijaribu kulisimamisha lakini hakuna lililosimama, wote wawili wakachanganyikiwa.
“Mama!”
“Naam mwanangu”
“Acha nikimbie nyumbani kwa akina Mariam nikamwombe baba yake atusaidie gari!”
“Wazo zuri sana,  laiti ungekuwa umesema mwanzo,  hivi sasa tungekuwa hospitali!”
“Nilipitiwa!”

Pamoja na giza lote lililokuwepo Vingunguti sababu ya mawingu ya mvua angani, Tom hakuogopa, ni kweli hakuzoea kutembea usiku kwa kuogopa vibaka lakini siku hiyo aliweza. Akakimbia moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Mariam na kuanza kugonga kwenye lango kuu la kuingilia lakini hakuna mtu aliyemsikia wala kufungua,  akalazimika kuzunguka nyuma ya nyumba na kugonga kwenye dirisha la kwanza alilokutana nalo bila kujua nani aliyelala ndani ya chumba hicho.
“Nani?” ilikuwa ni sauti ya Mariam.
“Mariam?”
“Ndio!”
“Mimi  ni Tom!”
“Tom?”
“Ndio!”
“Unafanya nini saa hivi nje?”
“Baba yangu anaumwa!”
“Anaumwa nini?”
“Ameshindwa kukojoa!”
“Mungu wangu! Sasa?”
“Nimekuja kuomba msaada wa gari!”
“Baba amesafiri, tutafanyaje sasa?”
Je, nini kitaendelea?

Beyond Love -5

Tom alikuwa gizani akijaribu kutafakari juu ya nini cha kufanya ili kuhakikisha kwamba baba yake  anapelekwa hospitali   baada ya kuambiwa na Mariam kuwa  gari lilikuwepo lakini baba yake  ambaye dereva alikuwa amesafiri,  hivyo  hapakuwa na dereva wa kuifanya kazi hiyo. Akamwomba Mariam atoke nje ili wapate kushauriana  kwa sababu akili yake yeye ilikuwa imekoma kufanya kazi.
“Sidhani kama mama atakubali nitoke nje!”
“Sasa?”
‘Tuongelee hapa hapa!”
“Hakuna njia yoyote unayoweza kuitumia kunisaidia?”
“Nakuhurumia sana Tom lakini sidhani kama naweza, mimi najua kuendesha gari lakini sio sana, hata mara moja sijawahi kuendesha gari mbali na hapa nyumbani tena baba akiwa hayupo!”
“Kwa hiyo unaweza kuendesha?”
“Kidogo naweza!”
“Sasa kwanini usijaribu?”
“Naogopa kugongana na magari barabarani!”
“Lakini hakuna magari mengi hivi sasa!”
“Mh! Tom unanishawishi kufanya jambo la hatari sana”
“Mariam take risk for me!” (Mariam thubutu kwa ajili yangu)
“Hebu subiri!” Mariam aliongea akishuka kitandani kisha kunyata hadi sebuleni ambako aligusa juu ya kabati mahali ambako  siku zote ufunguo wa gari  ulihifadhiwa na kukuta upo, akauchukua na kunyata tena hadi chumbani ambako alimwomba Tom amsubiri nje ya lango.
“Sawa!”

Baada ya kuvaa nguo zake, Mariam alinyata  kwa mara nyingine akitumia ustadi wa paka mpaka akaufikia mlango na kuufungua bila kelele  yoyote kisha kutembea hadi kwenye lango la kutokea nje, pia akalifungua na kutoka. Tom alikuwa akimsubiri, akamsogelea na wakakumbatiana, Mariam alipomwangalia vizuri aligundua machozi yalikuwa yakimtoka.
“Usilie Tom!”
“Nampenda sana baba yangu!”
“Najua!”
“Naomba unisaidie baba afike hospitali, nakufanyisha kosa lakini sina jinsi, wewe peke yake ndiye  msaada ninaoutegemea, tafadhali nisaidie ili baba yangu apone, Mariam unataka niendelee na shule?”
“Ndio!”
“Basi nisaidie ili baba yangu apone, akifa  sina uhakika kama naweza kuendelea kusoma!” aliongea Tom akilia, maneno hayo yakauchoma moyo wa Mariam mpaka ndani kama vile mkuki wa moto, naye akalengwalwengwa na machozi..
“Sasa sikiliza!” Mariam alisema.
“Ndio!”
“Nafungua lango kuu,  kwa sababu  sitaki kuliwasha gari likiwa  mahali lilipo, mama atasikia muungurumo, hivyo basi  itabidi tulisukume sisi wenyewe  kulitoa ndani mpaka pale mbele kwenye mteremko ndipo tuliwashe,  huo ndio mtihani tulionao,  tukifanikiwa  basi  mimi niko tayari kuthubutu kuendesha gari kwenda hospitali, si ni Amana Ilala?”
“Ndio!’
“Uko tayari kusukuma gari?”
“Natamani lingekuwa limeshafika nje” Tom aliongea akionyesha utayari wake.

Bila woga  Mariam akanyata tena na kuingia ndani ambako kwa  taratibu sana alizungusha komeo la lango na kufanikiwa kufungua bila kelele ndipo akamwita Tom aingie ndani, wote wawili kwa nguvu zao zote walizokuwa nazo na hata za akiba, walishirikiana na kufanikiwa kusukuma gari hilo dogo aina ya Nissan Datsun  hadi nje ambako waliendelea kusukuma mpaka mbele mita kama  hamsini hivi,  kilichowasaidia ni mteremko, ndipo Mariam akaingia na kuketi kwenye usukani,  mara moja akawasha na gari likaitika. Tom alibaki mdomo wazi, hata siku moja hakuwahi kufahamu kwamba msichana huyo alikuwa na uwezo wa kuendesha.

“Nani alikufundisha kuendesha gari Mariam?”
“Ni baba,  lakini hajawahi hata siku moja kuniruhusu niendeshe peke yangu!”
“Haya twende basi!”
“Umesema wako sehemu gani?”
“Stendi”

Mariam aliendesha gari kwa ustadi mkubwa, wakipita kwenye barabara zenye madimbwi mpaka wakafanikiwa kufika stendi na  kuwakuta  wazazi wa Tom wakisubiri, wote wamelowa na mvua, baba  akiendelea kulia  kwa maumivu makali aliyokuwa nayo  yaliyosababishwa na mkojo uliogoma kutoka! Mama yake Tom hakuamini alipoona gari linasimama na mwanae kushuka, macho yake alipoyatupa kwenye usukani alimwona Mariam ameketi, hakutaka hata kuuliza swali lolote,  alichokihitaji wakati huo ni kufika hospitali tu.

Baada ya kuegesha gari Mariam alishuka, wote wakasaidiana kumpandisha mgonjwa garini, zoezi lilipokamilika wote wakapanda, gari likawashwa tena na safari kwenda hospitali ya Amana ikaanza. Akiwa nyuma ya usukani Mariam alitetemeka lakini hakutaka kuionyesha hali hiyo, mpaka wakafika Tazara ambako alikata kushoto kuelekea Buguruni ambako alikata kulia kuingia barabara ya Uhuru bila kukutana hata na gari moja barabarani, akanyoosha moja kwa moja hadi hospitali  ya Ilala Amana, yeye mwenyewe hakuamini kama alikuwa amewafikisha.

“Nakushukuru Mungu!” alitamka maneno hayo kimoyomoyo alipoegesha gari mbele ya jengo lililoandikwa OPD na  wauguzi wakafika wakiwa na machela.
“Vipi?” mmoja wao akauliza.
“Tuna mgonjwa!”
“Anaumwa nini?”
“Ameshindwa kukojoa!”
“Poleni!”

Wauguzi wakapanda ndani ya gari na kwa kusaidiana na Tom pamoja na  Mariam walimshusha  mgonjwa na kumlaza juu ya machela ambayo ilisukumwa moja kwa moja hadi kwenye chumba cha daktari, akalazwa kitandani na daktari kuanza kumchunguza kwa makini, alishangazwa na jinsi mfuko wa mkojo ulivyokuwa umetuna.
“Mzee hujakojoa tangu saa ngapi?”
“Tangu  juzi!”
“Pole sana…masista hebu nileteeni  Catheter na vifaa vyote vya  Catheterization haraka”  Daktari aliagiza.
“Sawa daktari!” Mmoja wao aliitikia na kuondoka mbio  aliporejea  alikuwa amebeba sinia lenye vifaa  pamoja na  mpira wa kutolea mkojo,  vyote akaviweka kwenye meza iliyokuwa kando ya kitanda, daktari akawaomba ndugu wa mgonjwa watoke nje ili apate kufanya kazi yake.

 Tom, Mariam na mama yake wakatoka nje. Alichokifanya daktari ni kuchukua mpira na kuuingiza kwenye uume wa mzee Chacha na kuusukuma moja kwa moja mpaka kwenye mfuko wa mkojo, ilikuwa ni kazi ngumu kidogo kuliko alivyofanya kwa wagonjwa wengine lakini ulipoingia mkojo mwingi ukatoka  kwa nguvu na kuanza kujaa kwenye mfuko wa  plastiki ambao mpira wa kutolea mkojo ulikuwa umeunganishwa nao. Mzee Chacha akashusha pumzi na maumivu yote yakaisha.

Nje ya chumba cha daktari, Mariam na Tom waliendelea kuongea mama akiwa kimya, fikra zote zikiwa zimetekwa na  tatizo la mume wake. Hakuwa na uhakika kama angeweza kupona, ilikuwa ni mara ya kwanza kushuhudia binadamu ameshindwa kukojoa,  hakuna kitu alichotamani kama mume wake kupona kwani maisha katika jiji la Dar es Salaam yasingewezekana bila yeye kuwepo,  mshahara wake wa ulinzi ulikuwa mdogo lakini uliweza kuitunza familia yao.
“Tom!”
“Naam”
“Acha mimi nirudishe gari la wao kabla hakujakucha, mama yangu huwa ana kawaida ya kuamka saa kumi na mbili kamili, hivi sasa ndio nasikia Adhana inalia, acha nirudi, ili mradi nimeshakufikisha hapa, endeleeni na matibabu nitakuja kukuona asubuhi!”
“Nakushukuru sana Mariam, msaada ulioutoa ni mkubwa sitausahau, nakupenda kuliko unavyofikiria!”
“Nakupenda pia na ndio sababu nayafanya yote haya!”
“Endesha vizuri njiani, naomba Mungu asaidie ufike nyumbani salama!”
“Amina!”
Wote wakasimama na kukumbatiana, walipoachiana ndipo Mariam alimfuata mama yake Tom na kumuaga, yeye pia alitoa shukrani nyingi na kumtaka pia afikishe shukrani hizo kwa wazazi, hakuwa na habari kabisa kwamba gari liliibiwa. Mariam akashukuru na kuingia ndani ya gari, kuwasha na kuondoka kwa mwendo wa kawaida.

Mbele aliingia barabara kuu ya Uhuru na kunyoosha kama alivyokuja mpaka akafika Tazara kwenye mataa,  macho alipoyatupa mbele aliona taa za kijani zikiwaka,  akawa na uhakika  ilikuwa ni zamu yake, kwa haraka aliyokuwa nayo wala hakutaka kuangalia upande mwingine wowote, akakata kona  kuelekea  uwanja wa ndege, hakujua kama kulikuwa na  daladala la kutokea Mbagala likija kwa kasi bila kujali taa alishtuka,  aliona mwanga mkali machoni.
“Mamaaaaaaa! Nakufa!” ndio maneno pekee aliyoyasema ukatokea ukimya.

***
“Tumeutoa mkojo  sasa hivi anajisikia vizuri, lakini ni lazima tufanye uchunguzi ili kufahamu ni kwanini alishindwa kukojoa, hapa kuna uwezekano kukawa na  moja  kati ya matatizo mawili, aidha ana Stricture au Benign Prostatic Hypertrophy!” daktari aliongea  baada ya  kuwaita  Tom na mama yake kutoka nje.
“Sijakuelewa daktari” Tom alisema, maneno yaliyokuwa yametolea yalikuwa ni mazito sana kwa elimu yake ya kidato cha nne.
“Inawezekana kuna kovu ambalo limeziba njia ya mkojo, hii inaitwa Stricture  au Tezi ya Prosteti imepanuka sababu ya uzee na kuuziba mrija wa kutoa mkojo nje sababu unapita ndani yake!”
“Mungu wangu si ni magonjwa makubwa sana hayo?”
“Hapana, yanaweza kutibika kwa njia ya upasuaji lakini ni lazima tufanye kwanza uchunguzi kupata uhakika! Subiri kuche, ili  afanyiwe vipimo vya Ultra-sound ili tuone kama kuna  tatizo lolote tumboni, sawa?”
“Sawa daktari!”
“Kwa hivi sasa naandika cheti akalazwe wodi ya wanaume!”
“Ahsante daktari!” mama yake Tom aliitikia.
Je, nini kitaendelea? Ajali  iliyompata Mariam imemwacha salama?

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Beyond Love -6

Kulipokucha hapakuwa na kazi nyingine iliyofanyika hospitali kwa mzee Chacha zaidi ya vipimo, daktari aliandika kwenye faili lake afanyiwe  kipimo cha  kupiga picha tumboni kilichoitwa kwa kimombo Ultra-sound,  saa  tatu kamili  wauguzi walifika na kumbeba kwenye machela kumpeleka kwenye chumba cha kipimo hicho, mrija wa  mkojo ukiwa mahali pake. Kila kitu kikafanyika na  akarejeshwa wodini baada ya dakika arobaini na tano, Tom na mama yake walikuwepo kusubiri, mioyo yao ikiwa na hamu kubwa ya kujua tatizo lililokuwa likimsumbua mgonjwa wao.

“Tom!” Dk. Magesa alifika na kumwita nusu saa baadaye,  mkononi akiwa ameshikilia faili juu yake likiwa limeandikwa Chacha Mitiro, Tom akaelewa lilikuwa ni faili la baba yake.
“Naam daktari”
“Njoo wewe na mama tuongee!”

Akamgusa  begani mama yake alikuwa akisinzia  kwenye msingi  nje ya wodi na kumwomba anyanyuke wafuatane, wakaingia  wodini ambako  wauguzi walikuwa bado wakimsaidia mzee Chacha  kupanda kitandani. Daktari  akaanza kufungua faili lililokuwa mikononi mwake,  wakati anamaliza wauguzi  nao walishamaliza kumlaza mgonjwa kitandani ndipo daktari akaanza kulielezea vizuri tatizo lililokuwa likimsumbua mzee Chacha.
“Mzee anaumwa, ana uvimbe tumboni!”
“Uvimbe wa nini?” mama yake Tom aliuliza.

“Tezi ya Prostate,  kwa  ilivyovimba nahisi  atakuwa na Saratani, kwani uvimbaji wake sio wa kawaida, nahitaji kumchukua kwenda chumba cha upasuaji leo mchana ili nipate kuchukua kipande cha nyama kwenye tezi hiyo  nikipeleke hospitali ya Ocean Road  kuhakikisha ninachokiwaza!”
“Sawa tu daktari!”

“Kwa hiyo naomba muwe wavumilivu,  kwa hivi sasa atatumia dawa za kuzuia maambukizi lakini pia atakojoa kwa kutumia mpira, tukishapata majibu ndio tutajua sasa ni nini  kifanyi…!” daktari hakuimaliza sentensi yake hadi mwisho akashangaa kuona mzee Chacha akikakamaa kitandani kama mtu mwenye degedege kali, lilikuwa jambo la ajabu sana kulishuhudia kwani mara nyingi waliopatwa na tatizo hilo walikuwa ni watoto wadogo.

“Mungu wangu baba kawaje tena?” Tom aliongea akimwangalia daktari.
“Hebu nipeni sindano ya Valium!” daktari aliwaeleza wauguzi huku akimlaza mzee Chacha vizuri kitandani kuhakikisha haumi ulimi wake, muda mfupi baadaye muuguzi alirejea na chupa ya dawa pamoja na bomba la sindano, akamkabidhi daktari ambaye aliivunja na kuinyonya dawa yote kwa kutumia bomba kisha kumchoma mzee Chacha,  muda mfupi baadaye akatulia na kulala usingizi.
“Sijui ni kwanini anapatwa degedege? Nahitaji kujua hili suala, sijawahi kuona mtu aliyeshindwa kukojoa akapatwa na hali hii,  lazima kuna tatizo jingine hapa!”
“Tusaidie kumchunguza vizuri daktari, huyu ni baba yangu ndiye anayenisomesha, akifa  mimi nitakuwa nimekwama moja kwa moja!”

“Unasoma darasa la ngapi Tom?”
“Kidato cha nne!”
“Ulikuwa wa ngapi kwenye mtihani wako?”
“ Wa kwanza!”
“Hongera, unataka kuwa nani ukimaliza masomo  yako?”
“Kama wewe”
“Daktari?”
“Ndio!’
“Kazi ya  wito hii mwanangu!”
“Nafahamu lakini nataka kusaidia watu, kuna masikini wengi kama mimi!”
“Nakutakia kila la kheri, sasa saa tano kamili watakuja kumchukua wamlete chumba cha upasuaji nichukue  hicho kipimo, sawa?”
“Sawa daktari!”

Kama ilivyopangwa saa tano kamili  machela iliingizwa wodini na mzee Chacha akapandishwa juu yake kisha kupelekwa moja kwa moja hadi chumba cha upasuaji Tom na mama yake wakifuata nyuma na kusubiri nje ya chumba hicho wakiwa na wasiwasi mwingi!  Ndani   akaingizwa kwenye chumba kimoja kidogo kwa ajili ya kazi hiyo ambako alimkuta Dk. Magesa akimsubiri, kazi ikaanza kufanyika na kukamilika ndani ya kipindi cha nusu saa,  haukuwa upasuaji kama ambavyo Tom na mama  yake walifikiri bali kifaa fulani kiliingizwa kwa kutumia mashine mpaka kwenye tezi hiyo na kuchukua kipande cha nyama,  kikawekwa ndani ya chupa tayari kwa kupelekewa hospitali ya Ocean Road.

Mgonjwa aliporudishwa wodini, mawazo ya Tom yalirejea tena kwa  Mariam akaanza kufikiria juu ya wema wote alimtendea, hakujua kabisa angefanya kitu gani ili  msichana huyo  apate kuzielewa shukrani zake! Hakuwa na jinsi zaidi ya kumpenda,  tayari alishaanza kumkubali na kuona kama ingewezekana  baadaye katika maisha yao,  alikuwa  tayari  hata kubadili dini yake lakini amuoe Mariam kuwa mke wake wa maisha, mambo aliyomtendea yalikuwa makubwa mno.
“Ananipenda kwa ukweli kabisa!” aliwaza.

Baadaye mama yake aliondoka na kumwacha Tom  wodini,  kama kawaida aliendelea kumuwaza Mariam akimsubiri kwa hamu, alijua mchana huo ni lazima angefika sababu  aliahidi  siku hiyo badala ya kwenda kwenye masomo ya ziada angerudi wodini  kumwona  baba yake Tom. Mpaka saa kumi na moja wakati mama analeta chakula cha jioni, Mariam alikuwa hajaonekana, Tom akahisi labda wazazi wake hawakumruhusu kwani isingekuwa kawaida  asifike kabisa kwa upendo  aliokuwa nao moyoni mwake.
“Mariam amekuja?”
“Bado”
“Kwanini?”
“Sifahamu mama,  lakini atakuja tu!
Walikaa na mama  yake mpaka muda wa kuona wagonjwa  ukapita bila Mariam kuonekana, mama akaondoka  kurudi nyumbani akimwacha Tom mwenye mawazo mengi kichwani mwake,  si kwa sababu baba yake alikuwa akiumwa peke yake bali kwa sababu pia Mariam alikuwa hajaonekana,  alimpenda mno, alitamani kuwasiliana naye angalau kwa simu lakini hakuwa na namba, matumaini akayahamishia siku iliyofuata ambayo pia Mariam hakuonekana, wasiwasi wake ukazidi kuongezeka.
“Haiwezekani, au kwa sababu kaona baba yangu kaugua? Ndio maana ananitelekeza?  Lakini Mariam hawezi kufanya hivyo, ana upendo wa kweli, sijui tu ni kitu gani kimempata!”

Siku tatu baadaye alizobaki wodini akimwangalia baba yake  kuanzia   sababu  mama hakuruhusiwa  kulala kwenye wodi ya wanaume, Mariam alikuwa hajaonekana!  Badala ya huzuni  hisia za chuki zikaanza kumwingia Tom,  moyoni  akajua alikuwa ametelekezwa kwa sababu  baba yake alikuwa mgonjwa.  Siku hiyo  ndiyo majibu kutoka Ocean Road yalikuja na kuthibitisha kabisa kwamba baba yake Tom  alikuwa na Saratani iliyocheleweshwa kupata matibabu na kusambaa karibu kwenye viongo vyote muhimu vya mwili ukiwemo ubongo.

“Ndio maana anapatwa  na degedege kumbe ubongo wake umekwishashambuliwa na  Saratani!” Dk Magesa aliongea na Tom pamoja na mama yake ofisini.
“Atapona?” Tom aliuliza.
“Kwa kweli ni kazi ngumu kidogo, kwanza itabidi ahamishwe hapa kupelekewa hospitali ya Ocean Road ambako watamwanzishia matibabu ya Saratani, Mungu akisaidia anaweza kupona!”
“Tunashukuru daktari!”

Maelezo hayo baadaye yalitolewa kwa mzee Chacha katika lugha ya kumpa matumaini na wakapakiwa ndani ya gari kwenda hospitali ya Ocean Road,  Tom akiwa ameacha maagizo kwa wauguzi kwamba ikitokea Mariam akaonekana na kuulizia basi aelekezwe mahali walikokuwa, wauguzi wakaahidi kumsaidia kufanya hivyo. Safari  ya hospitali ya Ocean Road ikaanza, siku zote Tom alipita nje ya hospitali  hiyo akielekea feri lakini hakuwahi kuwaza kwamba siku moja angeingia humo akiuguliwa na baba yake, hakuamini kama  Saratani ingeweza kuingia ndani ya familia yake, aliuona ugonjwa wa watu wengine.

Matibabu yalianza siku hiyo hiyo kwa njia ya vidonge,  mionzi na dawa za sindano ambazo badala ya kuonekana kumsaidia mzee Chacha zilimdhoofisha zaidi, afya yake ikaharibika kabisa na kupoteza uzito mwingi ndani ya muda mfupi! Nywele zote zikanyonyoka kichwani sababu ya ukali wa dawa alizokuwa akipewa.

Kila mara Tom alipomwangalia  baba yake  alishindwa kuvumilia na kutoka nje ambako  alibubujikwa na machozi akitamani angalau Mariam angeonekana na kumpa maneno ya faraja lakini haikuwa hivyo, hatimaye wiki  mbili zikakatika hali ya mzee Chacha ikizidi kuwa mbaya, madaktari wakashauri mgonjwa arudishwe nyumbani hasa baada ya kugundua alikuwa ni mtu wa Tarime na mke wake hakuwa tayari azikwe jijini Dar es Salaam kama kingetokea kifo jambo ambalo kila mtu alikuwa akilitarajia.
“Sawa tu daktari nimekubali,  tatizo letu kubwa ni nauli,  hatuna fedha kabisa!”
“Mimi na wafanyakazi wenzangu tutawachangia fedha kidogo lakini pia ninyi mnaweza mkajitahidi kutafuta kwa ndugu jamaa na marafiki!”
“Tutajitahidi!”

Alichokifanya mama yake Tom ni kuuza vyombo vyote vya ndani,  akaenda  Pepsi kazini  kwa mume wake  na kuomba msaada, Mkurugenzi wa kiwanda hicho akampa shilingi laki moja na nusu na kuja nazo hadi hospitali ya Ocean Road ambako wafanyakazi walimkabidhi shilingi laki moja, jumla akawa na shilingi  laki sita pamoja na zilizopatikana kwa kuuza vyombo, mipango ya safari ikaanza kuandaliwa.

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Siku mbili tu baadaye bila Tom kuonana na Mariam, moyo wake ukiwa umejaa hasira, walipanda daraja la tatu  la treni  kuelekea Mwanza ambako wangeunganisha kwa basi hadi Tarime, kwa jinsi hali ya mzee Chacha ilivyokuwa mbaya ilibidi  abiria wote waliokuwa naye kwenye kiti, wanyanyuke kumpisha alale, hakuna aliyekuwa na uhakika angefika mzee huyo  angefika Mwanza siku tatu baadaye akipumua.
Je, nini kitatokea? Nini kilimpata Mariam?

Beyond Love -7
Ulikuwa ni mlio mkubwa mno kwa mtu yeyote aliyekuwa jirani na eneo hilo kutosikia,  watu wengi waliokuwa jirani walianza kukimbia kwenda mahali magari yalipogongana, baadhi wakiwa na nia   ya kuokoa lakini wengine wakifikiria kuiba mali yoyote ambayo wangeikuta. Magari yaliyokuwa yakipita  kwenye Barabara ya Nyerere kwenda au kutoka Uwanja wa Ndege yalishindwa kuendelea na safari sababu barabara ilikuwa imezibwa na magari mawili yaliyogongana uso kwa uso katikati ya barabara, hii iliwafanya abiria wote waliokuwa kwenye magari washuke kwenda kutoa  msaada.
Kwenye daladala kulikuwa na abiria wengi walioumia, dereva wake akiwa amelaza kichwa kwenye usukani, damu zikimtoka puani na mdomoni, tayari alishakufa! Taratibu wakamwondoa na kumlaza chini. Sababu tairi za mbele  za daladala zilikuwa zimesimama juu ya gari dogo lililogongwa, ilibidi watu wajitolee kulisukuma  kurudi nyuma ili kutoa nafasi ya kuangalia  kama kulikuwa na watu wengine ndani ya gari dogo. Hayo yalifanyika wakati abiria waliojeruhiwa wakipakiwa ndani ya magari mengine tayari kwa kupelekwa hospitali ikiwa ni pamoja na dereva wa daladala aliyekufa.
“Mungu wangu kuna mtoto mdogo, tena kwenye usukani, sijui ndiye aliyekuwa akiendesha? Mbona mdogo sana?” Mtu mmoja aliuliza baada ya daladala kuondolewa juu ya gari dogo.
“Ni mdogo mno huyu, hawezi kuwa dereva kama ni hivyo basi itakuwa aliiba gari, hawa watoto wa matajiri ndio wanasababisha sana ajali barabarani, si ajabu alikuwa ametoka zake disko akiwa amelewa!” Mwingine  aliitikia.
Mariam alikuwa amelala ndani ya gari lililogongwa, akiwa kimya kabisa huku damu nyingi zikimtoka hasa kwenye paji la uso palipoonekana  kuvimba, damu nyingine ilikuwa ikimtoka puani na masikioni. Kwa jinsi alivyokuwa amebanwa ilikuwa kazi ngumu kidogo kumtoa, hata hivyo baada ya muda si mrefu walifanikiwa na kumlaza chini kisha kuanza kumgusa kifuani kuona kama alikuwa na uzima.
“Anahema!” Aliongea mwanaume aliyekuwa akimgusa kifuani.
“Basi hajafa, tumkimbizeni hospitali!”
“Ni jambo jema, mleteni huku kwenye gari yangu nimpeleke mara moja Muhimbili!” Mwananchi mmoja alijitolea, Mariam akabebwa juu juu na kwenda kupakiwa kwenye gari dogo aina ya Mark II,  safari kwenda hospitali ikaanza ambako walikuta pia majeruhi wengine wamekwishawasili.
Mapokezi hawakuona sababu ya kuuliza maswali mengi kwa jinsi hali ya mgonjwa ilivyokuwa mbaya, haraka akakimbizwa mpaka kwenye chumba cha daktari ambaye baada ya kumwona aliamuru akimbizwe haraka sana Chumba cha Upasuaji, kisha yeye kuwasiliana na madaktari wengine ambao walikutana  kwenye chumba hicho na Mariam kuwekewa Mashine ya Hewa ya Oksijeni  kisha kupandishwa kitandani ambako kazi ya kwanza iliyofanyika ni kuziba mishipa yote iliyokuwa  ikivuja damu kuzuia upotevu mkubwa.
“Haraka sana mfanyieni  CT-Scan!” Dk. Majaliwa, Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, alisema.
“Sawa daktari, acha tuwapigie simu hawa  watu waje kuifanya kazi hiyo mara moja!”
“Fanyeni hivyo haraka kwani  kwa dalili ninazoziona  nahisi  kuna tatizo kwenye  ubongo wake!”
“Sawa daktari!”
Dakika ishirini baadaye Bingwa wa Kipimo cha CT-Scan alifika kwenye Chumba cha Upasuaji cha Hospitali ya Muhimbili na vifaa vyake na kumfunga Mariam kichwani, kisha yeye na madaktari wote wakaanza kuangalia,  haikuhitaji muda mrefu sana kugundua kilichokuwa kikiendelea chini ya fuvu la Mariam; damu nyingi ilikuwa imevuja chini ya fuvu,  kichwa chacke kilijipiga kwenye chuma sehemu ya paji la uso na   ubongo kuumia kwa ndani.
“She has  a subdural  haemorrhrage!” (Anavuja damu chini ya fuvu!) Dk. Majaliwa aliongea baada ya kuitazama picha kwenye kompyuta.
“So?” (Kwahiyo?)
“She needs an urgent operation!” (Anahitaji upasuaji wa haraka)
“Are we ready?” (Tuko tayari?)
“Yes!” (Ndiyo)
“Can the people from laboratory do  urgent blood grouping and  cross matching check? As well as HB level?” (Watu wa maabara wanaweza kupima kundi lake la damu na anaweza kuongezewa na kundi gani? Pia  kiasi cha damu alichobakiza?) Dk. Majaliwa alisema na wote wakakubaliana,  watu wa maabara wakaitwa haraka na kuifanya kazi hiyo.
Hapakuwa na mtu wa kujiuliza mtu waliyekuwa wakimshughulikia aliitwa nani, mtoto wa nani na alitokea wapi. Kwao  alikuwa ni mgonjwa na kazi yao kubwa ilikuwa ni  kuokoa maisha yake, hilo ndilo madaktari walilotaka kulifanya. Damu ilipopatikana, vipimo vya moyo wake vikawa viko sawa, Mariam aliingizwa kwenye chumba kingine kikubwa cha upasuaji ambako kazi ya kupasua kichwa chake,  kuufikia ubongo na kuiondoa damu yote iliyoganda chini ya fuvu ilifanyika na kukamilika ndani ya masaa  sita, madaktari wakiwa wamesimama wima!
Baada ya hapo Mariam aliondolewa Chumba cha Upasuaji na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, hali yake ilikuwa mbaya, hakuna aliyekuwa na matumaini kwamba  angeweza kupona kwani mapigo yake ya moyo yalikuwa yakipanda na kushuka. Kwenye chumba hicho alilazwa na kuwekewa mashine ya hewa ya oksijeni, damu ikiendelea kudondoka kuingia kwenye mishipa yake huku  vipimo vyote vikifuatiliwa kila baada ya nusu saa kuona namna alivyoendelea, kadri muda ulivyozidi kusonga ndivyo mapigo yalivyozidi kuporomoka.
“I don’t know  if she will make it!” (Sijui  kama atapona!) Muuguzi mmoja alimwambia mwenzake baada ya kusoma majibu ya mwenendo wa moyo kwenye mashine.
“Hivi ni mtoto wa nani kwanza?”
“Mpaka sasa haijajulikana!”
“Mh! Wazazi wake wakijua watachanganyikiwa!”
****
Saa kumi na mbili  kamili alfajiri mama yake Mariam alizinduka usingizini na kuketi kitandani, siku hiyo kilikuwa kimetokea kitu cha ajabu ambacho kwa muda mrefu hakuwahi kukiona kwa mtoto wake. Ilikuwa ni kawaida ya Mariam kuamka asubuhi kabla ya wazazi wake kwenda kuamkia, baada ya hapo alirejea kitandani kulala,  siku hiyo ilikuwa tofauti na siku nyingine zote; mpaka muda huo Mariam alikuwa hajagonga mlango kusalimia, mama yake akaingiwa na wasiwasi na kufikiri pengine alikuwa mgonjwa.
Alichokifanya ilipotimu saa moja kamili ni kutoka chumbani kwake na kunyoosha moja kwa moja chumbani kwa Mariam; mlango ulikuwa wazi!  Jambo jingine ambalo halikuwa kawaida, hakutaka kusita, akaingia  ndani na kusimama katikati ya chumba, Mariam hakuwepo! Moyo wake ukaanza kudunda kwa nguvu,  badala ya kutembea akatoka akikimbia hadi nje ambako alianza kuita jina la mtoto wake lakini hakuitikiwa, hali hiyo iliwafanya wapangaji wengine watoke nje kwenda kuuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
“Sio kawaida ya Mariam kutokuwepo nyumbani asubuhi,  simwoni!”
“Labda amekwenda kufanya mazoezi?”
“Angeaga,  mwanangu namfahamu sana tabia zake!”
“Sasa atakuwa wapi? Labda huku nje?” Mmoja wa wapangaji  alisema akitembea kwenda nje, nyuma yake akifuata mama yake Mariam na wapangaji wengine watatu.
“Mungu wangu hata gari halipo, huyu mtoto kaenda wapi na gari?”
“Mimi nilisikia usiku lango la kuingilia likifunguliwa na  kitu kama gari likisukumwa, sikutia mashaka sana kwani mawazo  yangu yalinituma kuamini baba alikuwa amerudi labda alikuwa akitoka kwenda mahali fulani!”
“Basi huyo atakuwa ni Mariam, alikuwa anatoroka usiku, lakini kwenda wapi?” Mama yake Mariam alizidi  kuuliza, tayari machozi yalishaanza kumbubujika.
“Watoto wa kike mama,  huwezi jua labda yeye na wenzake walikuwa wanatoka!”
“Nitamwambia nini baba yake akirudi?” Mama huyo alisema akizidi kulia.
Je, nini kitaendelea? Tom na mama  yake walifanikiwa kufika Mwanza baba yake Tom akiwa hai? Je,

Beyond Love 8

Baada ya safari ya siku mbili, hatimaye siku ya tatu treni ilipiga honi eneo la Mwanza South,  watoto wakatoka ndani ya nyumba  kushangilia,  hiyo ndiyo hali iliyojitokeza kila treni ilipoingia mjini Mwanza! Hawakujua kilichokuwemo katika moja ya mabehewa ya daraja la tatu yaliyojaza watu, wengi wakichungulia madirishani, huku wakivuja jasho jingi miilini mwao.

Mzee Chacha alikuwa katika hali mbaya mno, tangu waondoke Dar es Salaam alikuwa akihangaika njia nzima na kudai hewa ilikuwa haimtoshi,  kazi ya Tom na mama yake ilikuwa ni kumpepea kwenye kiti alicholala! Zaidi ya mara tano alishapoteza fahamu na kuzinduka, kila mtu alimwonea huruma. Hatimaye walikuwa wakiingia Mwanza, mzee Chacha akipumua jambo ambalo hakuna aliyekuwa amelitegemea kwa jinsi hali yake ilivyokuwa mbaya.
“Afadhali!” Mama yake Tom aliongea treni iliposimama.
“Namshukuru Mungu!” Tom alijibu.
Kilichofanyika  abiria wote walipoisha ndani ya behewa ni kumshusha Mzee Chacha na kumlaza  chini wakifikiria nini cha kufanya. Jesica Makanyaga, msichana  waliyesafiri naye  akiwapa  kila aina ya msaada   njiani  aliwauliza ni wapi walikotaka kwenda  baada ya  kutoka stesheni, Tom akamsimulia  kila kitu juu ya baba yake  kisha kumwomba msaada wa usafiri mpaka stendi ya mabasi.
“Lakini mimi nafikiri  msiunganishe na safari kwenda Tarime!”
“Tufanye nini sasa mwanangu?”
“Mgonjwa  wenu anaumwa sana,  yafaa apelekwe kwanza hospitali!”
“Wazo lako ni zuri lakini sisi ni wageni kabisa hapa Mwanza,  hatumfahamu mtu yeyote na hatuna fedha kabisa!”
“Nitawasaidia, kumpakia huyu mzee ndani ya gari kwa kweli ni kumtesa kwanza nashukuru Mungu  tumefika Mwanza salama, naomba mnisubiri!” Alisema msichana huyo na kuanza kutembea kwenda nje, aliporejea muda mfupi baadaye aliongozana na kijana mrefu mwenye mzuzu.
“Huyu ni kaka yangu, anaitwa James,  yeye ana gari hapo nje tutamchukua mgonjwa kumpeleka Hospitali ya Sekou Toure atibiwe kwanza!”
“ Mungu awabariki sana, sijui jinsi ya kuwashukuru!” Tom aliongea huku akimwangalia Jesica usoni, msaada wa gari aliopewa ukamkumbusha  Mariam, chuki zikaongezeka.
“Hakuna shida, twendeni tu!”

Wakasaidiana kumbeba mgonjwa hadi nje ambako mlango wa gari aina ya  Landcruiser ulifunguliwa na mzee Chacha akaingizwa ndani akiwa hajitambui,  safari kwenda hospitalini ilianza. Dakika  ishirini na tano baadaye walishafika na mgonjwa kupokelewa kisha kuonwa na daktari ambaye alipopewa historia yake alishauri aongezewe chupa kadhaa za maji ya glukosi ili mwili wake upate nguvu, baada ya hapo wangeendelea na safari yao. Wakalazwa kwa siku mbili,  ndipo hali ya mzee Chacha ikatengemaa kidogo.

Hawakuwa na  jambo lolote la kusubiri mjini Mwanza, ikabidi  waunganishe safari yao  kuelekea Tarime, Jesica na James kama walivyofanya mwanzo,  waliwasaidia kutoka wodini mpaka stendi ya basi na kuwapandisha kwenye basi liitwalo Tanganyika Bus service, wakaagana kwa huzuni huku Tom akiwapa shukrani nyingi kwa msaada waliompa na kuahidi kuwakumbuka katika maisha yake  yote, saa moja baadaye safari ilianza mzee Chacha akiwa amelala peke yake kwenye kiti cha watu watatu.
Njiani hali yake ilikuwa mbaya, nafuu yote  iliyopatikana iliondoka,  alilalamika maumivu makali sababu ya kurushwarushwa na basi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kukimbizana na basi jingine kuwahi abiria mbele, hata hivyo walifanikiwa kuingia Tarime saa kumi jioni,  mzee Chacha akiwa hoi, hakuwepo ndugu  yeyote wa kuwapokea stendi ya basi kwani hakuna taarifa iliyotangulia,   lakini wasamaria wema waliomfahamu mzee Chacha walijitolea kutafuta kitanda na kukifanya machela,  kisha wakambeba moja kwa moja hadi kijijini.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tom kufika kijijini kwao, hata mara moja tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kukanyaga Kijiji cha Nyamongo ambako wazazi wake walitokea! Kitu cha kwanza kilichomshangaza ni maisha, yalikuwa duni mno, hapo ndipo akafuta kichwani  ufahamu aliokuwa nao kwamba maisha yake jijini Dar es Salaam yalikuwa mabaya kuliko binadamu mwingine yeyote.
“Kumbe  kuna watu wanaoishi maisha magumu kuliko mimi, kifupi Dar es Salaam kwa watu wa  hapa ni kama mbinguni!” Aliwaza.
“Tom mbona umebadilika?”
“Kwanini hamkuwahi kunileta nyumbani mama?”
“Tusa..mehe…ane mwa…nangu! Ni mak..osa ya..ngu,” baba yake aliongea kwa taabu kubwa.

Hakuwepo mtu mwingine nyumbani, bibi na babu wa Tom walishafariki miaka mingi na kuacha nyumba peke yake, hapo ndipo  ambako pangekuwa  nyumbani kwa mzee Chacha, mke wake na Tom tangu siku hiyo. Hivyo ndivyo ilivyotokea,  Tom na mama yake ndio wakawa watafutaji wa mahitaji yote, wazo la shule likafutika kabisa kichwani. Kila siku aliamka asubuhi na kwenda kwenye mgodi wa dhahabu wa Nyamongo,  ambako alifanya kazi ya kuosha mchanga wa dhahabu uitwao Marudio kwa kutumia Zebaki, kiasi kidogo cha dhahabu alichopata aliuza na fedha kumpelekea mama yake, ikatumika kununua chakula pamoja na dawa.

Mara chache alifikiria shule na kutamani kuendelea kwani alikuwa na uwezo wa kusoma mpaka Chuo Kikuu lakini fikra za  kuwaacha wazazi wake katika hali waliyokuwa nayo zilimfanya aamue kuchagua maisha tofauti na kusoma,  siku zikazidi kusonga baba yake akiteseka kitandani bila msaada wowote zaidi ya dawa ya maumivu,  hatimaye miezi sita baadaye Tom akiwa amezoea maisha ya mgodini, bila taarifa yoyote ya Mariam, BABA YAKE ALIKATA ROHO USIKU WA MANANE NA KUIACHA DUNIA, Tom hakuamini.
Je, nini kitaendelea katika maisha ya kijana huyu? Je,  watakuja kukutana na Mariam?

Beyond Love -9
Katika maisha yake yote Tom hakuwahi kufikiria dunia bila baba yake, lilikuwa ni jambo lisilowezekana. Mara nyingi alisikia watu wamefiwa na wazazi wao,  au wengine yatima kabisa lakini aliamini hayo yalikuwa matatizo ya watu wengine, yeye akijiweka kando. Lakini  usiku huo alimshuhudia baba yake akiwa amelala kwenye jamvi, mwili umebaki mifupa  na ngozi, mama yake alikuwa kando akilia kwa uchungu  huku akiliita  jina la mume wake, picha hiyo ilimuumiza sana Tom ambaye macho yake bado yalikuwa yameangalia kifuani kwa baba yake akiamini lazima kifua kingenyanyuka na kupanda tena, kuashiria kwamba baba yake alikuwa bado akipumua.
“Haiwezekani! Baba hajafa!” Alijikuta akitamka maneno hayo huku akimgusa kifuani na kumwita kwa jina, baba yake hakuitika.
“Ni kweli amekufa! Baba yako hayupo nasi tena  tumebaki peke yetu, huu ndio mwisho wake mwanangu ametangulia mbele ya haki!” Mama aliongea akimtengeneza mzee Chacha  mdomo na macho.

Mzee Chacha alipokata roho ilikuwa katikati ya usiku, wakiwa wawili peke yao ndani ya nyumba, lakini walipoanza kulia kwa sauti majirani walianza kufika kutaka kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Walipoambiwa  mzee alikuwa amefariki wengi walisikitika lakini wakashauri  mambo yote yaachwe mpaka asubuhi ya siku iliyofuata ndipo taarifa zisambazwe kijijini.

Hilo ndilo lililofanyika, Tom na mama yake wakilia kwa uchungu, majirani wakakusanyika kwa wingi na uamuzi wa kuzika ukafikiwa kwenye majira ya saa nne asubuhi,  kaburi likachimbwa na  saa kumi jioni mzee Chacha akalazwa shimoni na mchanga kufukiwa juu yake, baada ya hapo majirani wengi walisambaa kurejea majumbani mwao wakiwaacha Tom na mama yake peke yao.
“Mama mbona wameondoka wote?”
“Hatuna ng’ombe!”
“Za nini?”
“Tungekuwa na ng’ombe wangebaki, umasikini mbaya mwanangu,  ukikua  hakikisha unapata fedha na kutajirika, binadamu wana tabia ya kuwaheshimu wenye nacho, mimi na wewe hatuna kitu ndio sababu tumeachwa peke yetu!” Mama yake  Tom  aliongea akijifuta machozi, maneno hayo yakapenya moja kwa moja  kichwani mwa Tom na kuhifadhiwa.

Hakuna mtu aliyekuja kuwaona tena baada ya  hapo, walikuwa wao wawili wakifarijiana, kila siku alfajiri ilikuwa ni lazima wanyanyuke kwenda kwenye kaburi la mzee Chacha na kusujudu wakimwomba Mungu amrehemu kule alikokuwa! Siku zikazidi kusonga, hatimaye wakaizoea hali na miili yao kupata nguvu, Tom akatamani  kurejea tena machimboni  kuendelea na kazi yake ya kuosha mchanga wa Dhahabu, tayari alishazoea kazi hiyo na aliridhika kabisa na kipato kidogo alichopata, hakufikiria shule hata kidogo, wala Mariam, alikuwa kwenye ulimwengu mwingine ambako Mbinu ya kupata mafanikio haikuwa elimu peke yake.

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

“Mwanangu usiniache peke yangu?”
“Sina jinsi mama, wewe mwenyewe umesema umasikini mbaya, kama nimeshindwa kusoma basi  acha nitafute utajiri kwa njia nyingine! Naomba baraka zako”
“Hapana Tom! Huwezi kuondoka, wewe peke yako ndiye niliyebakiza hapa Duniani,  wewe ukifa huko machimboni nitafanya nini mimi?”
“Mama,  unamwamini Mungu?”
“Ndio!’

“Basi yeye ndiye atakayenilinda na kama kuna maisha mbele basi yatakuwepo na kama kuna kifo basi sitakikwepa!” Tom aliongea maneno mazito akimwangalia mama yake usoni ambaye alionekana kutoamini kama maneno hayo yalitoka mdomoni mwa Tom, kwake alikuwa mtoto mdogo mno kuongea mambo mazito kiasi hicho.

“Hapana, sikubali mwanangu, kaa tu hapa hapa tufe na umasikini wetu!”
Tom hakuwa na la kufanya, asingeweza kumkatalia mtu aliyemleta duniani. Siku zote alifundishwa kuwaheshimu wazazi hivyo akabaki kimya  kufuata maelekezo ambayo  mama yake alitoa,  kamwe asingeweza kuyakiuka, aliamini kufanya hivyo ingekuwa kupoteza baraka za wazazi ambazo zilikuwa muhimu sana katika ya mwanadamu,  ingawa aliyafanya yote hayo kwa shingo upande hakutaka kumwonyesha mama yake, siku zote aliendelea kutabasamu akimbembeleza amruhusu kwa hiari yake lakini  mama hakukubali.

Siku zikazidi kusonga  kazi yao  ya kuwapatia riziki ikiwa ni kufanya vibarua kwenye mashamba ya  majirani wenye uwezo, malipo yakiwa ni chakula. Tom hakuipenda kazi hiyo, hakumaanishwa kufanya hivyo siku zote za maisha yake,  alikuwa na akili nyingi ambazo zingemwezesha kupata fedha badala ya kuendelea kufanya vibarua vya kulima. Mara  kadhaa alitamani kutoroka aende machimboni bila ridhaa ya mama yake lakini aliogopa, mwisho akaamua kuwa anajifungia chumbani kila siku jioni na kuanza kulia.
“Mbona unalia Tom?”

“Mama ninao uwezo wa kubadilisha maisha yako, ukaishi kitajiri kuliko  mzee Wambura na  Magige tunaowalimia kwenye mashamba  yao!”
“Sasa hiyo ndiyo sababu unalia mwanangu?”
“Ndio! Naomba uniache niende machimboni, ipo siku  utakuja kufurahi kwa sababu uliniruhusu!”
“Utajitunza?”
“Ndio mama!”
“Utaendelea kumcha Mungu?”
“Ndio mama!”
“Hutawaonea watu wengine?”
“Ndio mama!”
“Hutaiba?”
“Ndio mama!”
“Kweli?”
“Kabisa mama yangu, hata mimi nasikitika kukuacha, nakupenda mno lakini sina jinsi inabidi nitakafute maisha!”
“Basi mwanangu,   hebu nipe mikono yako yote miwili!” Mama aliongea na Tom akanyoosha mikono yake  yote miwili na  kuviweka viganja vyake mbele ya mama ambaye alivishika na kuanza kuvitemea mate.
“Mungu akutangulie popote utakapokwenda mwanangu!”
“Amina mama!”
“Kila utakachokigusa kiwe chako!”
“Amina mama!”
“Watu wakusifu na kukuheshimu!”
“Amina mama!”
“Uwe na maisha marefu na Mungu akukinge na maovu!”
“Amina mama!”
“Ahsante mwanangu,  sasa unaweza kwenda una baraka zangu zote!”
“Ahsante mama yangu, sitakuangusha!”
“Sawa!”
Walipomaliza maongezi hayo ilikuwa saa saba za usiku wakiwa wameketi kando ya moto ndani ya  nyumba yao,  Tom  akamshuhudia mama yake akiingia chumbani na  yeye kutandika jamvi sebuleni, haukupita muda mrefu sana usingizi ukampitia na kuamka saa  kumi na nusu  za usiku, mara moja akaanza kugonga chumbani kwa mama  yake na kumuaga, mama akatoka nje na kumsindikiza mpaka mita kama mia moja hivi kutoka nyumbani, akamshuhudia Tom akipita katikati ya vichaka na kupotea.
Je, nini kitatokea? Je, Mariam yu hai au amekufa? Je, mama yake  atampata? Je,  nini kitampata Tom machimboni? Fuatilia

Beyond Love -10

Tukio la kupotea kwa Mariam pamoja na gari lilikuwa limemchanganya mama  yake  kupita kiasi, hakujua nini cha kumwambia mume wake akirejea  kutoka safarini  Mwanza alikokuwa amekwenda kibiashara kwani alielewa ni kiasi gani alimpenda mtoto wake Mariam, asingekubali  jibu jingine lolote zaidi ya mwanae kuwa mzima! Akili yake ilikuwa imesimama kufanya kazi, majirani pamoja na wapangaji walikuwa wamemzunguka wakimtuliza huku wakijadili juu ya nini cha kufanya, hatimaye walifikia uamuzi  wa kuondoka nyumbani kwenda kituo cha polisi cha Vingunguti kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Mariam pamoja na gari.

“Anajua kuendesha?” Mkuu wa kituo aliwauliza.
“Hapana! Alijaribu kujifunza kidogo lakini hakufuzu, hivyo siwezi kusema anajua kuendesha” mama yake alijibu huku akibubujikwa na machozi,
“Ana mpenzi?”
“Hapana,  yupo kijana mmoja wanasoma naye lakini ni rafiki wa kawaida, angekuwa mpenzi wake lazima angeniambia maana mimi na yeye huwa hatufichani  kitu, ni marafiki! Jamani mwanangu Mariam uko wapi? Naomba uwe hai…” mama huyo alimalizia kwa kilio huku majirani wakizidi kumtuliza.
“Gari lilikuwa nyumbani jana jioni wakati wa kulala?”
“Ndio”
“Yeye mwenyewe mtoto?”
“Alikuwepo, tuliingia naye ndani kulala na mlango ukafungwa!”
“Huwa ana tabia ya kutoka nje usiku,  tuseme kwenda muziki au kitu cha kufanana na hicho?”
“Hapana, ni mtoto wa ndani tu, kitu anachopenda kufanya ni kusoma!”
“Sawa, kaeni hapo kwenye kiti  mniache nifanye mawasiliano na Makao Makuu  ili niulize kama kuna tukio lolote la wizi au utekaji lililotolewa taarifa,  lakini nionavyo mimi huyu binti atakuwa aliiba gari kama wanavyofanya watoto wengine wengi wa matajiri akaenda zake muziki,  si ajabu  yuko kwa mpenzi wake amepitiwa na usingizi, usiwe na wasiwasi wowote mama atapatikana tu!”
“Hajawahi kufanya jambo la aina hii, kamwe hawezi kuanza leo, mwanangu Mariam hana tabia hiyo, niambieni tu kama amekufa!”

“Hapana mama Mariam, usiseme hivyo,  unamwom bea mtoto mabalaa,  waache maaskari wafanye kazi yao” Mmoja wa majirani aliongea akimpigapiga mama Mariam mgongoni na kumsaidia kuketi kwenye benchi, wote wakimsikiliza askari  akiongea  na Makao Makuu kwa simu ya upepo,  bahati nzuri sana sauti  ya upande wa pili pia ilikuwa ikisikika.

“Kuna ajali ilitokea…ova…jana usiku…maeneo ya Tazara…ova… binti mmoja alikuwa akiendesha gari hilo…akagongana uso kwa uso na daladala lililokuwa likitokea Mbagala…ova…akaumia vibaya sana…gari hilo hivi sasa limeegeshwa kituo cha polisi Buguruni…ova! Sijui kama unayemtafuta ndiye huyo?”
“Namba za gari afande”
“Ni TZ 22210!”
“Uwiiiii!Mwanangu! mwanangu Mariam! Amepata ajali…afande…afande…muulize kama yupo hai au amekufa, gari hilo ni la kwetu!” tayari mama  yake Mariam alishanyanyuka kwenye benchi na kusogea  kaunta ambako aliongea na askari  aliyekuwa akiwasiliana.
“Afande huyo binti alikuwa na hali gani?”
“Kwa   taarifa nilizopewa, matumaini ni kidogo na  kuna uwezekano atakuwa alikufa pale pale!”
“Mungu wangu! Muulize yuko hospitali gani?”
“Eti afande yupo hospitali gani?”
“Alikimbizwa Muhimbili”
“Ahsante afande,  acha niende huko huko Muhimbili” Mama yake Mariam aliongea na kuanza kukimbia kutoka kituoni,  hakwenda hatua nyingi sana majirani wakawa wamemkamata na kuanza kutembea naye taratibu hadi nje ya kituo ambako waliingia ndani ya gari na safari kwenda Muhimbili ikaanza mama Mariam akilia na kutamka maneno kwamba hakujua nini cha kumweleza baba wa mtoto akirejea kutoka safari, alijisikia mzembe kupita kiasi, yeye mwenyewe akawa anamatani kufa.

Muhimbili waliegesha gari lao  mbele ya  Idara ya wagonjwa wa nje na kuanza kukimbia kwenda Idara ya wagonjwa mahututi, hawakuhitaji kuuliza chochote mapokezi, walikuwa na uhakika kwa jinsi hali ilivyokuwa lazima alikuwa amelazwa kwenye wodi hiyo na si mahali pengine popote.  Maandishi “USIINGIE NDANI BILA RUHUSA” yaliwafanya wote wabaki wamesimama nje ya wodi hiyo bila kujua la kufanya ingawa walikuwa na uhakika kabisa Mariam alikuwemo ndani, dakika kumi na tano baadaye  walishuhudia mwanaume mfupi mwenye mvi  akitembea haraka sana kuelekea kwenye wodi hiyo, nyuma yake akiwepo mwanamke mwingine, wote walionekana kuwa na wasiwasi.
“Habari za leo kaka?” Mama yake Mariam aliuliza.
“Nzuri tu habari zako?”
“Sio nzuri”
“Kuna nini?”
“Namtafuta binti yangu, alipatwa na ajali  alfajiri ya leo na kukimbizwa hapa Muhimbili!”
“Anaitwa nani?”
“Mariam!”
“Kuna binti mmoja yuko ndani lakini sifahamu jina lake maana hana uwezo wa kuongea,  aliletwa  alfajiri baada ya gari lake kugongana na gari jingine, sasa sina uhakika kama ndio huyo! Nimepigiwa simu sasa hivi kwamba hali yake ni mbaya sana, imebadilika ghafla” mzee huyo  aliyetambulika kama daktari bila kujieleza sababu ya kifaa cha kupimia  mapafu na moyo alichokuwa amekivaa shingoni alimjibu  mama yake Mariam huku uso wake ukionyesha wasiwasi.
“Ni huyo hu…!” mama yake Mariam aliongea lakini kabla hajaendelea sana mlango ulifunguliwa, muuguzi aliyevaa nguo nyeupe akachungulia nje macho yake yakionyesha wasiwasi mwingi.
“Dk.Mbise!” Akaita.
“Yes Aminata!”
“Mgonjwa amekufa!” ilikuwa ni sauti ya muuguzi akimwita  daktari aingie ndani haraka.

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Dk.Mbise  hakuongea chochote  zaidi ya kuanza kukimbia kuingia ndani ya wodi akimwacha mama yake Mariam taaban,  mwili wake ukaishiwa nguvu, giza likayafunika macho yake na taratibu akaporomoka sakafuni! Majirani na wapangaji wake alioongozana nao kwenda polisi na baadaye hospitali ndio waliombeba tena kumkimbiza idara ya wagonjwa wa nje kwenda kumwona daktari ambaye baada ya kumpima kifuani na mashine ya kusikilizia mapigo ya Moyo,  alionyesha wasiwasi.
“Mh!”
“Mbona unaguna daktari?”
“Huyu mgonjwa huwa anashinikizo la damu?”
“Hajawahi kusema,  labda mume wake angekuwepo swali hilo lingepata jibu, kwani vipi daktari? Moyo haupigi?”

Daktari hakuongea chochote,   alibaki kimya akimwangalia mgonjwa machoni kwa wasiwasi mwingi, alionekana mwenye siri moyoni ambaye hakutaka kuwashirikisha watu waliokuwemo ndani ya chumba, mwisho akawaamuru wote watoke nje yeye abaki na wauguzi peke yao.
Je,  nini kitaendelea? Mariam amekufa? Mama yake je? Maisha ya Tom yataendeleaje 


machimboni? kuendelea kusoma sehemu ofya >>BEYOND LOVE- (ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA 11 MPAKA YA 20

 

 KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

No comments

Powered by Blogger.