MASSACRE (MAUAJI YA HALAIKI) SEHEMU 03
“Upo wapi Benedict? Mbona sikuoni hapa nje?”
Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza.
“Wewe nani?” Benedict aliuliza.
“Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi”
Benedict hakutaka kuongea kitu chochote
kile, akakata simu, akainuka kitandani na kuanza kuelekea nje. Alipofika nje,
akaanza kuangalia katika kila upande. Macho yake yakatua katika uso wa mwanaume
mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi ambaye alimuonyeshea ishara ya kumuita. Benedict
akaanza kupiga hatua kumfuata mwaname yule.
“Hebu tusogee pembeni kidogo” Mwanaume yule
alimwambia Benedict na kuanza kusogea pembeni. Hata kabla mzee yule hakuongea
chochote, akatoa kitambulisho chake na kumuonyeshea Benedict.
“Uchunguzi wenu umeishia wapi?” Benedict
aliuliza.
“Kwamba baba yako hakujinyonga”
“Unasemaje?”
“Huo ndio ukweli. Hakujinyonga bali
alinyongwa”
“Umejuaje?”
“Tulipima alama za vidole katika kamba ile,
na vile vile tulikuta alama za kiganja katika shavu lake hali iliyoonyesha
kwamba alipigwa kibao kabla ya kunyongwa”
“Sawa. Kwa hiyo mmeamua nini?”
“Kumtafuta muuaji. Jambo hilo libaki kuwa
lako tu, usimpe taarifa dada yako wala mama yako katika kipindi hiki. Wape
taarifa baada ya mwezi mzima kupita” Mkuu yule wa polisi alimwambia.
Benedict akaonekana kuchanganyikiwa, maneno
ambayo aliongea mzee yule ndio ambayo yalionekana kumchanganya zaidi.
Alimwangalia mzee yule mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile
ambacho alikuwa ameambiwa. Hasira zikazidi kumpanda zaidi juu ya kanisa la
Praise And Worship kwa kuona kwamba kanisa lile pia lilikuwa limehusika katika
mauaji ya baba yake.
Unyonge ukaongezeka zaidi moyoni mwake, kiu
ya kumtafuta muuaji ikaonekana kumkamata. Maswali mengi juu ya muuaji huyo
yakaanza kumiminika kichwani mwake, mbele yake akaona giza, tumaini ndani ya
moyo wake likaonekana kupotea.
“Ni kanisa. Kanisa linamjua muuaji” Benedict
alijisemea kwa hasira.
****
Mchungaji Mwakipesile hakuonekana kuridhika
japokuwa mchungaji Matimya alikuwa amevuliwa cheo cha uchungaji na kusimamishwa
kazi ya Utumishi wa Mungu. Hakutaka mzee Matimya abaki ndani ya dunia hii kwani
kama angemuacha basi ni lazima ingetokea siku ambayo angekuja kufahamu njama
zote alizozifanya na hivyo kumuingiza katika matatizo.
Mchungaji Mwakipesile hakutaka kutulia,
akaiweka pembeni kazi yake ya Utumishi wa Mungu aliyokuwa nayo na kujiingiza
katika mambo ambayo yalikuwa kinyume na kazi yake. Akaamua kuwafuata vijana
ambao akaamini kwamba wangeweza kumfanyia kazi yake kama alivyotaka kufanyiwa.
Mchungaji Mwakipesile hakutaka kuendelea kubaki Morogoro, kitu alichokifanya ni
kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia gari lake.
“Unahitaji nini mzee?” Kijana mmoja
aliyejazia mwili alimuuliza mchungaji Mwakipesile.
“Nahitaji kuonana na kiongozi wenu”
“Unamfahamu au?”
“Hapana” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
Hapo hapo akaambiwa ateremke kutoka ndani ya
gari lake. Vijana watatu wakatokea mahali hapo kutoka katika sehemu ambayo
hakuifahamu na kuanza kumpekua. Walitumia dakika tano kumpekua yeye pamoja na
gari lake, walipomaliza wakaanza kumwangalia usoni.
“Wewe ni polisi?” Kijana mmoja aliuliza.
“Hapana”
“Unahitaji nini?”
“Nataka kuonana na mkuu wenu” Mchungaji
Mwakipesile aliwaambia.
Hapo hapo akafungwa kitambaa usoni na kisha
kupakizwa ndani ya gari nyingine na safari ya kuelekea asipopafahamu kuanza.
Muda wote mchungaji Mwakipesile alikuwa akitetemeka kwa woga. Imani aliyokuwa
nayo juu ya vijana wale ikaanza kupotea, kitu alichokifanya katika kipindi
hicho ni kutulia ili kuona ni mahali gani ambapo angefikishwa.
Safari ilitumia dakika kumi huku kitamba
kikiendelea kuwa usoni mwa Mchungaji Mwakipesile. Mara baada ya dakika chache
gari likasimama nje ya jengo moja ambapo geti likafunguliwa na gari kuingizwa
ndani. Mchungaji Mwakipesile akateremshwa na moja kwa moja kupelekwa ndani ya
nyumba hiyo. Kitambaa kile alichokuwa amefungwa usoni kikafunguliwa na
kuamrishwa kukaa kochini.
Macho ya mchungaji Mwakipesile hayakutulia
sehemu moja, yalikuwa yakiangalia kila kona sebuleni pale ambapo alikuwa
ameachwa peke yake. Wala hazikupita dakika nyingi, mzee mmoja mnene akafika
mahali hapo na kutulia katika kochi jingine huku mkoni akiwa na chupa ya
kinywaji cha Heineken.
“Nasikia unanihitaji” Mzee yule alimwambia
mchungaji Mwakipesile.
“Ndio”
“Una shida gani?”
Mchungaji Matimya akaanza kuelezea shida
zake huku mzee yule akiwa kimya kumsikiliza. Mchungaji alitumia dakika tano
kuelekezea kila kitu ambacho alitaka kifayike kwa wakati huo. Mara baada ya
kumaliza maelezo yake, mzee yule akachukua kinywaji chake kile na kupiga funda
moja.
“Una kiasi gani?” Mzee yule alimuuliza.
“Milioni mbili” Mchungaji alijibu
lililomfanya mzee yule kuanza kucheka.
“Unataka tumuue mtu au kuku?” Mzee yule
aliuliza.
Tayari muonekano wa mzee yule ukaonekana
kuwa tofauti na jinsi alivyokuwa kabla, ndita zikaanza kuonekana usoni mwake
hali ambayo ilimuongezea wasiwasi mchungaji. Mchungaji Mwakipesile akashindwa
kutoa jibu, alibaki akimwangalia usoni mzee yule kana kwamba hakulisikia lile
swali aliloulizwa.
“Acha utani na kazi yetu” Mzee yule
alimwambia.
“Milioni tatu” Mchungaji Mwakipesile
alimwambia.
“Nimekwambia acha utani”
“Milioni nne. Naomba unisaidie”
“Utani wako umezidi”
“Milioni tano. Please, naomba unisaidie”
“Sawa. Nitafanya hivyo kwa kiasi hicho kwa
sababu tu umeniomba” Mzee yule alimwambia Mchungaji Mwakipesile.
Mchungaji akaanza kutoa maelekezo kama njia
ambazo zingewezesha kupatikana kwa mzee Matimya. Akatoa picha yake na yule mzee
kuanza kuiangalia kwa makini. Alieleza kila kitu ambacho kilionekana kuwa
muhimu kuhitajika na watu hao.
“Utafurahia kifo gani?” Mzee yule
alimuuliza.
“Chochote kile ili mladi aonekane amejiua”
Mchungaji Mwakipesile alijibu.
****
Saa kumi na mbili, vijana watatu walikuwa
wamelipaki gari lao dogo mita hamsini kutoka katika geti la nyumba ya mzee
Matimya iliyokuwa Mwenge. Vijana wale hawakutoka nje ya gari lao, waliendelea
kumsubiri mzee Matimya ambapo lengo lao lilikuwa moja tu, kumuua. Waliendelea
kusubiri zaidi na zaidi lakini wala mzee Matimya hakutoka ndani.
Mara baada ya kuona kwamba wamesubiri muda
mrefu pasipo mzee Matimya kutoka ndani ya nyumba yake, kijana mmoja kati yao
akachukua simu yake na kupiga namba ya mzee Matimya ambayo walikuwa wamepewa na
mchungaji Mwakipesile. Simu ikaanza kuita, iliendelea kuita kwa sekunde chache,
ikapokelewa.
“Mungu wangu! Umerudi lini kutoka Marekani?”
Sauti ya mzee Matimya ilisikika ikiuliza mara baada ya maongezi mengine.
Maongezi kati ya mchungaji Matimya na kijana
yule aliyejiita Zolaya yaliendelea zaidi na zaidi. Vijana wale wengine wala
hawakuongea kitu chochote kile, walibaki kimya wakimsikiliza Zolaya. Maongezi
hayo yalichukua dakika mbili nzima, simu ikakatwa, uso wa Zolaya ukajaa
tabasamu hali ambayo iliwaonyeshea matumaini fulani.
“Vipi?” The Killer aliuliza.
“Anatoka. Jiandaeni, wekeni silaha zenu
vizuri” Zolaya aliwaambia.
Hawakutaka kusubiri chochote kile, silaha
zikawekwa tayari. Kila mtu akabaki kimya huku macho yakiwa getini kwa mzee
Matimya. Zilipita dakika tano, geti likafunguliwana gari aina ya Vitara kutoka.
Wakayapeleka macho yao ndani ya gari lile, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya mzee
Matimya. Walipoona kuwa mzee Matimya ameanza safari ya kuelekea uwanja wa
ndege, hapo hapo Zolaya akawasha gari na kuanza kumfuatilia mzee Matimya.
Hawakutaka kuwa karibu na gari la mzee
Matimya, waliacha umbali wa hatua thelathini kati yao. Mara baada ya gari la
mzee Matimya kuchukua barabara ya Sam Nujoma, nao wakachukua barabara hiyo na
kuanza kuelekea Mwenge kituoni.
“Unafikiri atatumia njia gani kwenda uwanja
wa ndege?” The Killer aliuliza.
“Labda atakwenda kuingilia pale Sayansi.
Njia ya kule Ubungo hakutaka kuitumia kwa sababu ya foleni” Zolaya alijibu.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kama kutakuwa na foleni kidogo pale Sayansi
itakayomfanya kusimama. Shukeni na mkamuingilie. Hakikisheni mnampa amri ya
kuelekea Mbezi, hasa katika msitu wa Pande” Zolaya aliwaambia.
“Sawa”
Bado waliendelea kumfuatilia zaidi na zaidi
huku wakiwa wametenganishwa na magari mawili kati yao. Mzee Matimya akakata
kona na kuchukua barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Kila mmoja garini alikuwa na
shauku ya kutaka kufanya kile ambacho walikuwa wameagizwa. Kama walivyotaka
ndivyo ilivyokuwa, walipofika Sayansi, magari yakasimama kutokana na foleni
iliyokuwa mahali hapo.
“Fanyeni haraka. Mfuateni, mtekeni na kuanza
kuelekea Mbezi” Zolaya aliwaambia.
Kwa haraka sana bila kupoteza muda, The
Killer na Zinja wakateremka na kuanza kulifuata gari alilokuwa mzee
Matimya.Walipolifikia, wakaingiza mikono yao katika madirisha yale ambayo
hayakuwa yamefungwa vioo na kisha kutoa loki za milango ile. Mzee Matimya
akapigwa na mshtuko mara baada ya kuona vijana wawili wakiingia ndani ya gari
lake.
“Mbona mnaingia nd….?” Mzee Matimya aliuliza
lakini hata kabla hajamalizia swali lake, The Killer akatoa bunduki yake
iliyokuwa kiunoni.
Mara baada ya mzee Matimya kuiona bunduki
ile, hapo hapo akatulia, mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda kwa kasi kubwa
huku woga ukianza kumuingia. Hakutakiwa kuongea kitu chochote kile katika
kipindi hicho. Kitu walichokifanya ni kumuamuru mzee Matimya kutoka katika
usukani na kuelekea katika kiti cha nyuma huku Zinja akishikilia usukani na
safari ya kuelekea Mbezi kuanza.
Walitumia dakika sabini kutoka Kijitonyama
mpaka Mbezi Mwisho huku Zolaya akiwafuatilia kwa nyuma. Hawakutaka kuishia
Mbezi Mwisho, kitu kilichowapelekea kuendelea mbele. Kutokana na kasi ambayo
walikuwa wakiitumia, walichukua dakika tano mpaka kufika katika msitu wa Pande.
“Hapa hapa panatosha” The Killer alimwambia Zinja.
Wote wakateremka kutoka ndani ya gari,
wakamshusha mzee Matimya na kuanza kusogea nae katika sehemu iliyokuwa na miti
mingi zaidi. Zolaya akafika mahali hapo, akateremka huku mkononi akiwa na kamba
ngumu na kisha kuanza kuwasogelea.
Kutokana na giza nene lilikuwa mahali hapo,
wakawasha tochi zao na kuanza kuelekea mbele zaidi. Mzee Matimya bado alikuwa
akitetemeka, moyoni alikuwa akiendelea kusali kwa kumtaka Mungu amnusuru na kumlinda
na chochote ambacho kilitakiwa kufanyika. Hali haikuonekana kuwa na usalama wa
hali yoyote ile kwa mzee Matimya, kadri walivyozidi kusonga mbela na ndivyo
ambavyo woga ulivyozidi kumshika zaidi.
“Panatosha” Zolaya aliwaambia huku akiwa
amemaliza kufunga kamba katika mtindo wa kitanzi.
“Jamani vipi tena?” Mzee Matimya aliuliza
mara baada ya kuona akivalishwa shingoni kamba ile ambayo Zolaya alikuwa
amekwishaifunga mtini. Hakukuwa na mtu aliyejibu chochote zaidi ya Zolaya
kumpiga kofi moja shavuni ambalo lilimfanya kulewa.
Kutokana na ubishi ambao alikuwa akiuleta
mzee Matimya, iliwachukua nusu saa mpaka kukiingiza kichwa chake katika tundu
la kamba na kumnyonga huko porini. Hakukuwa na mtu aliyeonyesha roho yoyote ya
huzuni, kila mtu alikiona kitendo kile kuwa cha maana kwake. Huo ndio ukawa
mwisho wa maisha ya mzee Matimya.
Kazi yake kubwa ya kumtumikia Mungu katika
kipindi kilichopita ikabaki kuwa kama historia. Alinyongwa porini siku hiyo
baada ya wiki mbili ndani ya skendo yake ya kutaka kubaka ambayo ilikuwa
imevuma sana nchini Tanzania. Zolaya alipohakikisha kwamba mzee Matimya
amefariki, akaondoka pamoja na wenzake huku wakiuacha mwili ule mtini.
*****
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na
ndivyo ambavyo hasira za Benedict juu ya kanisa la Praise and Worship lililoko
Mwenge zilivyozidi kuongezeka. Hakuonekana kumpenda mtu yeyote ndani ya kanisa
lile, kila mtu kwake alionekana kuwa adui wake. Kila alipokuwa akielekea
kanisani pamoja na mama yake, Bi Meriana na Angelina, Benedict hakutaka kuongea
na mtu yeyote kanisani hapo.
Moyo wake aliuona kuwa kanisa lilihusika na
kifo cha baba yake, mzee Matimya. Kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika
kanisani kama mahubiri ya Neno la Mungu kilionekana kuwa kama unafiki. Mauaji
ndicho kitu ambacho kilikuwa kimeutawala moyo wake katika kipindi hicho, hakutaka
kuliacha kanisa hivi hivi, alitamani kuliangamiza kanisa.
Ibada ya mwisho ya Jumapili ya mwisho katika
mwaka huo ndio ambayo ilikuwa ikiendelea ndani ya kanisa hilo. Kila mtu
alionekana kuwa uso ulioonyesha furaha. Wanakwaya walikuwa wakiimba kwa furaha,
yaani kila kitu katika kipindi hicho kilikuwa kikifanyika katika hali ya
furaha. Watu wote walikuwa wakiimba kwa furaha kwani zilikuwa zimebakia siku
mbili kabla ya kumaliza kwa mwaka huo wa 2007.
“Funguo ziko wapi?” Sauti ya shemasi
ilisikika ikiuliza.
Kila mtu aliyekuwa amekaa katika viti vya
nyuma kanisani pale aligeuka na kuwaangalia mashemasi ambao walikuwa
wakizitafuta funguo ambazo zilikuwa mlangoni katika kipindi kichache
kilichopita. Ingawa ibada ilikuwa ikiendelea huku mchungaji mpya wa kanisa
hilo, Munisi akiendelea kuhubiri, mashemasi hawakuwa wakisikiliza mahubiri hayo
zaidi ya kuendelea kuzitafuta funguo za milango ya kanisa.
“Kwani zilikuwa wapi?” Shemasi mwingine
aliuliza.
”Zilikuwa hapa. Tena muda mchache uliopita”
“Hebu angalia chini ya viti, labda kuna
mtoto alizichukua”
Hapo hapo Shemasi mmoja akaanza kuangalia
angalia chini ya viti lakini funguo wala hazikuonekana. Tayari wasiwasi ukaanza
kuwaingia, akili zao zikaanza kuchanganyikiwa. Hawakujua ni nani ambaye alizichukua
funguo zile kutoka katika msumali uliochomekwa ukutani, wakazidi kuangalia
katika kila sehemu huku mchungaji Munisi akiendelea kuhubiri.
“Zile kule”
“Ziko wapi?”
“Kazishika yule mtoto” Shemasi alijibu.
Kwa haraka haraka akaanza kupiga hatua
kumfuata mtoto yule aliyezishika funguo zile ambazo alikuwa nazo, mtoto yule
ambaye alikuwa pembeni mwa Benedict. Mara baada ya kumfikia mtoto yule, shemasi
akazichukua funguo zile.
“Mmechelewa sana” Benedict alijisemea moyoni
huku akionekana kuwa katika utulivu mkubwa kumsikiliza mchungaji.
Mara baada ya ibada kumalizika, moja kwa
moja Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya kanisa lile huku furaha
ikiongezeka maradufu moyoni mwake. Kitendo cha kuzipata funguo za milango ya
kanisa lile kilionekana kumfurahisha kupita kiasi. Hakutaka kuliona kanisa
likiendelea kumtumikia Mungu kwani kitendo kile kilionekana kuwa kama unafiki
mbele ya macho yake.
Mara baada ya kufika Kariakoo, akateremka na
kuanza kuelekea katika kibanda ambacho kilikuwa na tangazo la kuchongesha
funguo. Alipokifikia, akamuita mchonga funguo ambaye mara moja akafika mahali
hapo. Akachukua kipande cha sabuni ambacho kilikuwa na alama tatu za funguo na
kisha kumgawia.
“Elfu moja kila moja”
“Sawa” Benedict alisema na kisha kumgawia
noti ya shilingi elfu kumi mchongaji yule.
“Rudi saa kumi, kila kitu kitakuwa tayari”
“Hakuna tatizo” Benedict alisema na kisha
kuondoka mahali hapo.
****
Masaa manne yalikuwa yamebaki kabla ya
kuuingia mwaka ambao ulikuwa ukiitwa ‘Mwaka wa Baraka’, mwaka wa 2008. Kila mtu
alionekana kuwa na furaha, waumini mbalimbali wa dini ya kikristo wakaanza
kujiandaa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea makanisani mwao. Vijana mitaani
wakaziweka ngoma zao vizuri huku mafataki ya aina mbalimbali yakiwa yamewekwa
vizuri.
Japokuwa waumini wa Kikristo walikuwa
wakitaka mwaka uingie na kuwakuta wakifanya maombi ya kumshukuru Mungu kanisani
lakini hali ilionekana kuwa tofauti kwa watu wengine. Walevi walitamani mwaka
uingie huku wakiwa na vinywaji midomoni mwao, kwa wale ambao walikuwa wazinzi,
walitamani mwaka uingie na kuwakuta wakifanya ngono na watu wawapendao.
Benedict hakutulia, muda wote alikuwa
akifikiria kufanya mauaji. Huruma ilitoweka moyoni mwake, hasira kali na roho
ya kulipa kisasi ndio ambayo ilikuwa imeutawala moyo wake kwa wakati huo. Mara
kwa mara macho yake yalikuwa yakiiangalia saa yake, dakika zilionekana kwenda taratibu
tofauti na siku nyingine.
“Jiandae twende kwenye mkesha kanisani” Bi
Meriana alimwambia Benedict.
Mishipa ya fahamu ya Benedict ikawa kama
imezibuka, kitendo cha mama yake na dada yake, Angelina kwenda kanisani
kingeweza kumzuia katika kufanya kile ambacho alitaka kukianya. Akili yake
ikafanya kazi ya haraka haraka, akainuka na kuanza kuelekea chumbani kwake. Akaiangalia
saa yake ya ukutani, masaa mawili ndio ambayo yalikuwa yamebaki kabla ya
kuingia mwaka mpya wa 2008.
Hakutaka kuendelea kukaa chumbani, hapo hapo
akainuka na kuanza kuelekea sebuleni. Alichokifanya ni kuchomoa funguo za
kuingilia mlango wa sebuleni na mlango wa nyuma. Akatoka nje na kisha kuifunga
milango yote kwa nje. Hakutaka kubaki mahali hapo, akaingia garini na kisha
kuanza kuelekea kanisani huku akiwa na funguo za kanisa lile ambazo alikuwa
amezichonga Kariakoo.
Hakutaka kuelekea kanisani moja kwa moja,
akaanza kuelekea Sinza huku lengo lake likiwa ni kutaka kupata madumu ambayo
angefanya nayo kazi. Mara baada ya kuliona duka la jumla maeneo ya Sinza
Makaburini, hapo hapo akasimamisha gari, akateremka na kuanza kupiga hatua
kulifuata duka lile.
“Nahitaji madumu matatu ya lita ishirini” Benedict
alimwambia muuzaji mara baada ya salamu.
“Yenye mafuta?”
“Hapana. Matupu”
“Elfu tatu moja”
Benedict akaingiza mkono mfukoni na kutoa
kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kinatosha kwa madumu yote hayo matatu. Mara
baada ya kumgawia muuzaji kiasi kile cha fedha, akapewa madumu ambayo
akayapakiza ndani ya gari na kuondoka katika eneo hilo.
Safari ya kuelekea katika kituo cha mafuta
ikaanza. Akili yake ilikuwa ikicheza na muda tu, dakika tisini ambazo zilikuwa
zimebaki kabla ya mwaka mpya kuingia zikaonekana kumtosha kabisa kwa kufanya
kile ambacho alipanga kukifanya. Mara baada ya kufika katika eneo la kituo cha
mafuta, akayatoa madumu yale na kuanza kujaziwa mafuta aina ya petroli. Yalipojaa
yote, akalipa fedha na kisha kuyapakiza garini na kuondoka eneo hilo kuelekea
kanisani.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo
ambavyo hasira zake juu ya kanisa lile zilivyozidi kukaba kiasi ambacho
kiliyafanya machozi kutiririka mashavuni mwake. Kila wakati ambao picha ya
marehemu baba yake ilivyokuwa ikimjia kichwani na ndivyo ambavyo hasira juu ya
kanisa lile ilivyozidi kumpanda. Hakulipenda kanisa, alilichukia kanisa hilo,
mbaya zaidi alimchukia kila mtu kaisani mule.
Ibada ilikuwa ikiendelea kanisani, idadi
kubwa ya washirika zaidi ya mia mbili hamsini ilikuwa ndani ya kanisa hilo.
Nyimbo mbalimbali za dini zilikuwa zikiendelea huku watu wakiimba kwa furaha. Benedict
akayapeleka macho yake katika saa yake ya mkononi, dakika arobaini na tano
ndizo ambazo zilikuwa zimebaki kabla ya mwaka mpya kuingia. Benedict hakutaka
kuteremka kutoka garini, aliendelea kubaki mule mule huku macho yake
yakiendelea kuangalia mishale ya saa yake.
“Mnahitajika kanisani” Shemasi Mjuni
alimwambia Benedict huku akigongagonga katika kioo cha mlango wa mbele wa gari
lile. Benedict akashtuka kutoka katika lindi la mawazo, akayapeleka macho yake
katika kioo cha saa yake ya mkononi, dakika tano ndizo ambazo zilikuwa
zimebakia kabla ya kuingia kwa mwaka mpya.
Benedict
hakutaka kuteremka japokuwa alikuwa amesikia kwamba washirika wote walikuwa
wakihitajika kaisani, washirika ambao walikuwa nje ya kanisa wakaanza kuingia
kanisani. Ndani ya dakika mbili tu, hakukuwa na mtu yeyote nje ya kanisa zaidi
ya Benedict ambaye alikuwa ndani ya gari.
“Tunataka kuukaribisha mwaka kwa maombi ya
shukrani” Sauti ya mchungaji Munisi ilisikika na mashemasi kuanza kufunga
milango. Kitendo kile kilionekana kuwa kama kosa, kwani kwa haraka haraka, Benedict
akateremka kutoka garini na kuanza kuufuata mlango mkuu wa kuingilia kanisani
mule. Akaanza kuchungulia ndani kwa kupitia katika vitundu vya ufunguo
kitasani, hakukuonekana kuwa na ufunguo wowote kwa ndani. Benedict akauchukua
ufunguo wake ambao aliuchongesha kwa fundi na kisha kuuingiza katika tundu lile
na kisha kuufunga mlango ule.
Akaanza kupiga hatua kuelekea katika milango
mingine midogo, napo huko akafunga milango ile kwa funguo alizokuwa nazo.
Hakutaka kuzitoa funguo zile katika vitasa, aliziacha pale pale ili kama watu
waliokuwa kanisani watakapojaribu kuziingiza funguo zao basi zisiweze kuingia.
Kwa wakati huo Benedict alionekana kuwa na
haraka kupita kawaida. Akaanza kurudi garini ambapo akachukua dumu moja
lililokuwa na mafuta ya petroli na kisha kuanza kuyamwaga mafuta yale kupitia
katika nafasi ndogo chini ya mlango.
Unataka niwe nakutumia CHOMEZO watu 200 wa kwanza kulike PAGE YA 2JIACHIE Mtatumiwa imbox chomezo LIKE PAGE YETU HAPA ==>www.facebook.com/2jiachie
ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA
Post a Comment