ad

ad

MASSACRE (MAUAJI YA HALAIKI) SEHEMU 02



Judith akaanza kupiga hatua kukifuata kiti cha wageni na kisha kutulia huku kikiwa mbele ya meza ile pale ofisini. Judith hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia mchungaji kwa kutumia macho ambayo yalionyesha mshtuo mkubwa kwa mchungaji Matimya. Mchungaji Matimya akasimama na kuanza kumsogelea Judith ambaye alibaki kimya akijifikiria namna ya kufanya kile ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati ule.

   “Kuna nini tena judith?” Mchungaji Matimya alimuuliza Judith.

   “Nina kiu mchungaji” Judith alijibu.

   “Kiu ya Neno la Mungu au?”


   “Hapana. Nina kiu ya penzi lako”  Judith alijibu huku akionekana kutokujiamini.
   Mchungaji Matimya akapigwa na mshtuko, jibu ambalo lilitoka mdomoni mwa Judith lilionekana kumshtua kupita kawaida. Hakujua kama masikio yake yalikuwa yamesikia vibaya au yalikuwa yamesikia kitu halisi ambacho kilikuwa kimetoka mdomoni mwa Judith.
   Akaanza kumwangalia Judith mara mbili mbili kana kwamba hakuwa amekielewa kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka mdomoni mwa Judith. Uso wa Judith haukuonekana kutania hata kidogo, alionekana kumaanisha kile ambacho alikuwa akikiongea kwa wakati ule.
   Huku akionekana kutokujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya kwa wakati ule, akashtuka mara baada ya kumuona Judith akianza kuvua nguo zake katika kasi ambayo ilionekana kumshangaza.
    Mikono ya Judith ikapata nguvu ya ziada, akamvuta mchungaji Matimya na kisha kuanza kulivua shati lake ambapo likafunguka huku baadhi ya vifungo viking’oka. Mchungaji Matimya alijaribu kuleta purukushani za kutaka kujiondoa mikononi mwa Judith lakini hakufanikiwa.
   “Niachie…niach…..” Mchungaji Matimya alimwambia Judith lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, akasukumwa na Judith ambaye alianza kupiga kelele za kuomba msaada huku akiifungua blauzi yake na kuyaacha matiti yake nje. Judith hakuona kuridhika, akaanza kuipandisha sketi yake juu ya kuyaacha mapaja yake wazi.
   “Ananibakaaaaaa…..ananibakaaaaa…..” Judith alipiga kelele huku akimsogelea mchungaji ambaye alionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Kwa kasi kubwa Judith akamvuta mchungaji na kisha kumuweka katikati ya mapaja yake na kisha kuibana miguu yake huku kelele za kubakwa zikiendelea kusikika.
   Ghafla mlango wa ofisi ile ukafunguliwa na wazee wa kanisa kuingia. Picha ambayo ilionekana ndani ya ofisi ile ilionekana kumshtua kila mtu. Judith alikuwa amelala juu ya meza huku mchungaji Matimya akiwa katikati ya mapaja yake yaliyokuwa wazi.
   “Yesu wangu!” Mzee kiongozi wa kanisa hilo, Bwana Onesmo alijikuta akisema huku akiiweka mikono yake kichwani. Mara baada ya Judith kuona kwamba wazee wa kanisa walikuwa wamefika ndani ya ofisi ile na kuliona tukio lile, hapo hapo akajitoa na kuelekea pembeni huku akijitahidi kuyafunika matiti yake.
   “Mchungaji! Umefanya nini?” Mzee Sule aliuliza kwa mshtuko.
   Mchungaji Matimya hakutoa jibu lolote lile, alibaki kimya huku akimwangalia Judith usoni. Judith alikuwa akilia huku mashavu yake yakiwa yameloanishwa na machozi ambayo yalikuwa yakimtoka. Mchungaji Matimya hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea ili aeleweke kwa wazee wa kanisa kwamba hakuwa amefanya kile kitu ambacho Judith alikuwa akikisema kwa wakati ule.
   Muonekano wa Judith ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa ukiwahakikishia wazee wa kanisa kwamba mchungaji Matimya alikuwa amefanya kile ambacho Judith alikuwa akikisema kwa wakati huo.
   Sketi yake ilikuwa imechanika na kuyafanya mapaja yake kuwa nje. Blauzi yake ambayo alikuwa ameivaa ilikuwa imeng’olewa vifungo na kuyafanya matiti yake kuwa nje. Kila mtu alimwamini Judith juu ya kile ambacho alikuwa akikisema kwa wakati ule.
   Muda wote huo mchungaji Matimya alibaki kimya huku akiwa hafahamu ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya. Alionekana kuchanganyikiwa.
****
   Katika kipindi chote mchungaji Matimya hakuonekana kuwa na furaha, kila wakati alikuwa mtu wa majonzi tu. Skendo ya kutaka kubaka ambayo ilikuwa imemkuta ndio ambayo ilichangia kuwa katika hali hiyo ya majonzi. Katika vipindi vyote ambavyo alipitia katika maisha yake, kipindi hicho ndicho kilionekana kuwa kuwa kipindi kigumu kuliko vipindi vyote maishani mwake.
   Mara kwa mara alikuwa akijifungua chumbani akisali, alijiona kuwa kama mtu mwenye dhambi mbele za Mungu. Shetani alionekana kupewa nafasi ya kumjaribu.  Kila wakati alikuwa akisali huku machozi yakimtiririka, alilia kupita kiasi, hakuona msaada wowote mbele yake, alijiona kuwa kama mtu aliyetengwa pasipo msaada wowote ule.
   Marafiki zake wote aliokuwa nao walionekana kuwa kama kumtenga. Familia yake ndio ambayo ilionekana kuwa kila kitu katika maisha yake, hiyo ndio ilikuwa furaha yake, upendo wake na faraja yake kuu. Mchungaji Matimya hakupewa nafasi yoyote ya kujitetea, kila mtu alimuona kuwa mtu maalum ambaye aliitwa kanisani kwa ajili ya kuliharibu kanisa.
   Kanisani akawa akikaa katika viti vya nyuma pamoja na familia yake. Washirika wa kanisa hilo hawakuwaonyeshea upendo tena, kila mtu alionekana kuichukia familia hiyo. Tukio ambalo lilikuwa limetokea katika maisha yake lilionekana kutaka kuiyumbisha imani yake siku za usoni.
   Kila ibada ilipokuwa ikiisha, hakutaka kubaki kanisani hapo zaidi ya kuingia ndani ya gari na kuondoka pamoja na familia yake.
   Kila siku moyo wake ulikuwa na majonzi, furaha kwake ikapotea, majonzi yakautawala moyo wake. Mara kwa mara alikuwa akifikiria sababu zilizompelekea Judith kufanya kitendo kama kle ndani ya ofisi yake. Hakufikiria hata mara moja kama mchungaji Mwakipesile alikuwa nyuma ya tukio zima.
   Ndani ya gari kila mtu alikuwa kimya huku wote wakionekana kuwa na mawazo vichwani mwao. Vitendo ambavyo vilikuwa vikifanywa na washirika wa kanisa lile ndivyo ambavyo vilikuwa vikiwaumiza. Ukaribu ambao ulikuwepo kati yao na washirika wa kanisa lile ukaonekana kupotea. Familia nzima ilionekana kutenda dhambi isiyoweza kusameheka mbele za Mungu.
   “Siamini kama kanisa linaweza kufanya kitu kama hiki, yaani upendo wao wote umepotea, upendo ambao walikuwa nao kabla umepotea kabisa” Mzee Matimya alisema huku akionekana kuwa na majonzi.
   “Nafikiri Mungu anataka kuipima imani y….” Bi Meriana alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, Benedict akaingilia.
   “Silifikirii hilo mama. Hapa kuna kitu, ni lazima kutakuwa na mtu aliyefanya mpango huu” Benedict alisema huku mikono yake ikiwa imeshikiria usukani.
   “Hakuna mpango wowote Bened…..”
   “Usiseme hivyo baba. Sisi kama binadamu tuna udhaifu. Unaweza kukuta hata wachungaji wengine wamehusika katika hili” Benedict alisema huku akionekana kukasirika.
   “Usiseme maneno hayo juu ya watumishi wa Mungu, Benedict”
   Benedict hakutaka kuendelea kuongea kitu chochote kile kwani kila alipokuwa akiongea na ndivyo ambavyo hasira zilivyozidi kumpanda. Hakutaka kuwa na mapenzi yoyote na washirika wa kanisa la Praise And Worship. Alimchukia kila mtu kanisani. Akili yake haikukubaliana na kanisa kama kweli baba yake aliweza kufanya kitu kama kile. Alijua fika kwamba Judith alikuwa amefanya kitu kile kwa sababu ya kitu fulani.
   “Kuna mtu nyuma ya Judith” Benedict alisema mara baada ya ukimya kutawala kwa muda mrefu garini mule.
   Kila mtu akabaki akimwangalia Benedict ambaye alikuwa akitingisha kichwa chake juu na chini kuashiria kwamba alikuwa na uhakika juu ya kile ambacho alikuwa akikiongea katika kipindi kile.
   “Kuna mtu? Mtu gani?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kushangaa.
   “Simfahamu ni mtu gani lakini nafikiri mtu huyo atakuwa miongoni mwa wachun…”
   “Benedict…..” Mzee Matimya aliita kwa sauti iliyojaa hasira ambayo ilimfanya Benedict kunyamaza.
*****
   Mzee Matimya alibaki katika chumba chake cha kusalia. Macho yake yalikuwa yakiiangalia Biblia yake iliyokuwa juu ya meza. Aliiangalia kwa kipindi kirefu bila kufanya kitu chochote kile. Alitamani kuanza sala yake kama siku nyingine ambavyo alivyokuwa akifanya lakini kila alipojaribu kupiga magoti chini, aliiona miguu yake ikiishiwa nguvu.
   Aliendelea kutulia juu ya kiti ndani ya chumba kile. Alijikuta akipata nguvu mpya, akaipeleka mikono juu ya meza ile, akaichukua Biblia ile na kuifungua. Akaanza kusoma baadhi ya maandiko ambayo aliyaona yakimfariji. Ghafla macho yake yakaanza kujaa machozi ambayo baada ya muda fulani yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
   Nguvu za kuendelea kusoma Biblia zikatoweka. Akaifunika Biblia na kuyaelekeza macho yake darini. Alijiona kuwa peke yake, tumaini lote likatoweka, hasira zikaanza kumpanda kila kila alipokuwa akimfikiria Judith.
   Aliendelea kubaki katika hali ile kwa dakika kadhaa, mara akashtuka baada ya simu yake kuanza kuita. Akaupeleka mkono wake mfukoni na kuitoa simu ile na kuanza kukiangalia kioo cha simu ile. Namba ambazo zilionekana katika kioo cha simu ile zilikuwa ngeni machoni mwake. Hakutaka kujali sana, alichoifanya ni kuipeleka simu ile sikioni na kuanza kuongea.
   “Bwana Yesu Asifiwe mchungaji” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
   Mzee Matimya hakuitikia chochote kile. Kichwa chake kikaanza kujaza maswali juu ya mpigaji wa simu ile. Taarifa zilijulikana  Tanzania nzima kama katika kipindi hicho hakuwa mchungaji tena mara baada ya kuvuliwa uongozi huo. Ni nani alikuwa akiongea upande wa pili? Je alikuwa ni rafiki yake ambaye walipotezana kipindi kirefu kilichopita au alikwa mtu mwingine?
   “Mchungaji……” Sauti ya upande wa pili iliita mara baada ya kuona ukimya umetawala kwa kipindi kirefu.
   “Amen….Amen…Nani anaongea?” Mchungaji aliitikia na kuuliza swali huku akionekana dhahiri kutokumjua mpigaji wa simu ile.
   “Ni mimi Patrick. Patrick Chonya. Umenisahau mchungaji?”Sauti ya upande wa pili ilisikika
   Mzee Matimya akaonekana kupatwa na mshtuko, ghafla tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake. Kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yak kilionekana kusahaulika kwa muda. Alimfahamu sana Patrick, kijana ambaye alikuwa mshirika wake kabla ya kuhamia jijini Mwanza. Alisafiri miaka miwili iliyopita kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kusomea udaktari wa mifupa.
   “Mungu wangu! Umerudi lini kutoka Marekani?” Mzee Matimya aliuliza huku akionekana tabasamu likiendelea kuwepo usoni mwake.
   “Leo hii ndio nimekanyaga ardhi ya Tanzania. Njoo hapa uwanja wa ndege mchungaji. Nataka kukuachia mizigo yako kutoka kwa mchungaji Macbeth Lewis. Nataka kuchukua ndege kuelekea Mwanza” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
   Tabasamu likaongezeka zaidi na zaidi usoni mwa mzee Matimya. Hakuamini kama mchungaji Macbeth kutoka nchini Marekani ndani ya jiji la Atlanta angeweza kumkumbuka kwa kumletea zawadi kwani kilipita kipindi kirefu sana tangu mchungaji Macbeth aje nchini Tanzania na kuhubiri ndani ya kanisa lake.
   Kwa haraka haraka akakata simu na kuanza kujiandaa. Moyo wake ulirejewa na furaha, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea katika maisha yake alikiona kuwa kama mpango wa Mungu katika kudhihirisha kwamba bado alikuwa pamoja nae. Mara baada ya kumaliza kujiandaa, akatoka na kuanza kuelekea uwanja wa ndege huku tayari ikiwa imetimia saa kumi na mbili jioni.
*****
   Muda ulizidi kwenda mbele lakini wala mchungaji Matimya hakurudi nyumbani. Kila mtu alionekana kuwa na wasiwasi kwani hali ile haikuonekana kuwa ya kawaida kutokea. Mara kwa mara Bi Meriana alijaribu kumpigia simu mchungaji Matimya lakini simu haikupatikana.
   Bi Meriana hakukata tamaa, bado aliendelea kumpigia simu mume wake lakini majibu yalikuwa yale yale, simu haikupatikana. Amani ikatoweka moyoni mwake, mashaka yakaanza kumjaa, mara kwa mara Bi Meriana alikuwa akiikodolea macho saa yake, masaa yalikuwa yakiendelea kusonga mbele lakini wala mzee Matimya hakurudi nyumbani.
   Bi Meriana akashindwa kuvumilia, akasimama na kuanza kuelekea sebuleni, alipofika, akatulia kochini huku macho yake yakiangalia darini hali iliyoonyesha kwamba alikuwa na mawazo katika kipindi hicho. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kuwa na wasiwasi zaidi.
   “Mungu wangu! Saa sita!” Bi Meriana aliasema hali iliyofanya Benedict ambaye alikuwa sebuleni pale kushtuka.
   “Mbona umeshtuka hivyo?” Benedict alimuuliza.
   “Baba yako”
   “Amefanya nini?”
   “Hajarudi”
   “Toka aliyoondoka saa kumi na mbili?”
   “Ndio”
   Benedict akaacha kufanya kazi ambayo alikuwa akiifanya na kisha kuanza kumsogelea mama yake. Alipomfikia, akajiweka karibu nae na kuchomoa simu yake na kisha kuanza kumpigia baba yake, mzee Matimya. Simu ilikuwa vile vile, mawasiliano hayakupatikana kabisa hali ambayo ikaanza kuibua wasiwasi moyoni mwa Benedict.
   Simu mbalimbali zikaanza kupigwa kwenda kwa ndugu, jamaa na marafiki ili kujua kama mzee Matimya alikuwa huko lakini hawakufanikiwa kumpata. Wasiwasi ukaongezeka maradufu mioyoni mwao, kitu cha hatari kilionekana kumtokea mzee Matimya kwani halikuwa jambo la kawaida kitu kama hicho kutokea.
   “Kwa hiyo tufanye nini?” Benedict alimuuliza mama yake.
   “Labda tupige simu pol….” Bi Meriana alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Kwa haraka haraka akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile. Mara ya kwanza alifikiri kwamba mpigaji wa simu ile alikuwa mumewe, lakini mara baada ya kuangalia kioo cha simu yake, namba ilikuwa ngeni.
   “Hallooo…! Wewe ni mke wa mchungaji?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza swali kwa sauti ya juu hata kabla ya salamu. Bi Meriana hakujibu chochote kile, alibaki kimya kwa muda kama mtu ambaye alikuwa akijifikiria namna ya kulijibu swali lile.
   “Haloo..! Upo hewani?”
   “Ndio”
   “Basi njoo hapa kituo cha polisi haraka iwezekanavyo”
   “Kituo gani?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
   “Mbezi kwa Yusufu” Sauti ya upande wa pili ilijibu na simu kukatwa.
   Bi Meriana akabaki kimya huku simu ikiendelea kuwa masikioni mwake japokuwa simu ile ilikuwa imekatwa. Mwili wake ukaanza kumtetemeka huku miguu yake akiiona ikifa ganzi. Hakuendelea kubaki katika hali hiyo zaidi, machozi yakaanza kumtoka.
   “Mama. Nini tena?” Benedict aliuliza mara baada ya kumuona mama yake akiwa kimya muda mrefu.
   “Kituo cha polisi Mbezi kwa Yusufu”
   “Kimefanya nini?” Benedict aliuliza huku akionekana kushangaa.
   “Twende” Bi Meriana alisema.
   Hakukuwa na sababu yoote kubaki mahali hapo, kwa haraka haraka wakachomoka kutoka ndani na moja kwa moja kuelekea nje ambako wakaingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea katika kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu. Machozi yakaanza kumtoka Bi Meriana huku sauti ya kilio cha chini chini kikianza kusikikika.
   Simu ile ambayo aliipokea muda mchache uliopita ilionekana kumchanganya, tayari alikwishajua kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Maswali mfululizo yakaanza kumiminika kichwani mwake. Katika kipindi cha nyuma mzee Matimya aliaga kwamba alikuwa akielekea uwanja wa ndege ambako alikuwa akihitajika, kwa nini simu ilipigwa kutoka Mbezi? Tena mbaya zaidi katika kituo cha polisi.
   Kutokana na kutokuwa na foleni ya magari, walitumia dakika thelathini mpaka kufika Mbezi kwa Yusufu. Moja kwa moja wasimamisha gari lao nje ya kituo kile cha polisi na kisha kuelekea katika kituo hicho.
   “Karibuni” Polisi mmoja ambaye alikuwa zamu aliwakaribisha mara baada ya kuwaona.
   “Kuna nini afande?” Mume wangu yuko wapi?” Bi Meriana aliuliza maswali mawili mfululizo hata kabla ya salamu. Sauti ya kilio cha chini ikaanza kusikika kutoka kwa Bi Meriana. Kitendo cha swali lake kutokujibiwa ndicho ambacho kilionekana kumtia wasiwasi.
   “Nini kinaendelea?” Benedict alivunja ukimya kwa kuuliza swali.
   “Ni taarifa za masikitiko sana. Kitu ambacho kimetokea kimeonekana kumshangaza kila mtu” Polisi alisema mara baada ya kuchukua maelezo ya Benedict na Bi Meriana na kisha kuendelea.
   “Mlisema aliondoka toka saa kumi na mbili kuelekea uwanja wa ndege?” Polisi aliuliza.
   “Ndio”
   “Alirudi baada ya kuondoka?”
   “Hapana”
   Polisi hakutaka kuendelea kuuliza maswali, akainuka kutoka pale kaunta na kuanza kuelekea katika chumba kimojawapo kati ya vyumba ambavyo vilikuwa ndani ya kituo kile ambapo baada ya sekunde kadhaa, polisi mwingine ambaye alikuwa mahali pale nae kuingia ndani ya kile chumba.
   “Nini kinaendelea afande?” Benedict aliuliza mara baada ya polisi wale kurudi kaunta.
   “Jambo hili bado linafanyiwa uchunguzi”
   “Uchunguzi? Uchunguzi gani?”
   “Uchunguzi juu ya kifo chake” Polisi alijibu huku akionekana kuwa na wasiwasi.
   Jibu lile likaonekana kumchanganya kila mmoja, Bi Meriana akaanza kulia kwa uchungu. Neno ‘kifo’ ambalo lilitamkwa na polisi yule ndilo ambalo lilionekana kumuumiza. Wala hakuchukua hata dakika moja kuwa katika hali ile, macho yake yakaanza kuona giza ambapo baada ya sekunde chache akaanguka na kupoteza fahamu.
****
   Maturubai zaidi ya matano yalikuwa yamefungwa katika eneo la nyumba ya mzee Matimya. Idadi ya watu ambao walikuwa wamehudhuria msibani hapo wala haikuwa kubwa kama jinsi ambavyo ilitarajiwa. Ingawa wachungaji mbalimbali kutoka katika makanisa tofauti tofauti walikuwa wamehudhuria msiba huo lakini wala hakukuwa na zaidi ya washirika watano kutoka katika kanisa la Praise And Worship la Mwenge.
   Watu wengi ambao walikuwa wamehudhuria msibani pale walikuwa watu ambao wala hawakutoka mbali na eneo lile pamoja na waandishi wa habari. Kanisa likaonekana kupunguza ukaribu, kitendo cha waumini watano kuhudhuria katika msiba ule kilidhihirisha wazi kwamba mapenzi makubwa juu ya mzee Matimya hayakuwepo tena katika mioyo ya waumini wa kanisa lile.
   Vilio vya ndugu wa marehemu vilikuwa vikisikika kutoka kila kona msibani hapo. Sehemu kubwa ya mikeka iliyokuwa mahali hapo ilikuwa wazi jambo ambalo lilionekana kumshangaza kila mtu.
   “Mbona washirika wa kanisa la Praise and Worship hawaonekani hapa msibani?” Mchungaji Melek aliuliza kwa mshangao huku akiangalia katika kila kona msibani hapo kana kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani.
   “Wote walikasirishwa na kitendo kilichotokea. Mapenzi yao yakapotea. Mbaya zaidi, mzee Matimya alijinyonga” Kijana mmoja alimjibu mchungaji Melek.
   “Mungu wangu! Kumbe alijinyonga?”
   “Ndio. Nafikiri alijiona kuwa mkosaji mbele za Mungu wake” kijana yule alijibu.
   Benedict alikuwa ametulia pembeni kidogo mwa mchungaji Melek. Maneno yote aliyoyaongea mchungaji Melek na yule kijana yalionekana kumuumiza kupita kiasi. Hapo hapo akanyanyuka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba yao.
   Idadi kubwa ya wanawake ilikuwa ndani ya nyumba hiyo. Benedict hakutaka kuongea chochote kile, kitu alichokifanya ni kupiga hatua kuelekea chumbani kwake.
   Akajilaza kitandani huku macho yake yakiangalia juu, machozi yakaanza kumtoka. Benedict akazidi kushikwa na hasira juu ya washirika wa kanisa la Praise and Worship lililokuwa Mwenge. Kadri ambavyo alivyokuwa akilikumbuka kanisa hilo na ndivyo ambavyo hasira zake zilivyozidi kuongezeka zaidi.
   Huku Benedict akiwa katika hali hiyo chumbani, mara mlango ukafunguliwa na Angelina kuingia. Macho ya Angelina yalikuwa mekundu huku mashavuni akiwa na alama za michirizi ya machozi hali iliyoonyesha kwamba kipindi fulani kilichopita alikuwa akilia. Angelina akaanza kupiga hatua mpaka pale kitandani alipokuwa amejilaza Benedict.
   “Najiona kama tumetengwa” Angelina alimwambia Benedict kwa sauti ya chini iliyojaa majonzi.
   “Mapenzi yao yamepotea kabisa. Ukaribu wao hauonekani, ni lazima nifanye kitu juu ya kanisa hili” Benedict alimwambia Angelina huku akionekana kuwa na hasira.
   “Kitu gani?”
   “Niwaue. Ni lazima niwaue washirika wote wa kanisa lile. Hasa Judith” Benedict alisema.
   “Usifanye hivyo Benedict”
   “Haina jinsi, nataka kurudisha furaha yangu iiyopotea” Benedict alisema huku akichukua kitambaa chake cha mkononi na kujifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
   Ukimya mrefu ukatawala mahali hapo huku kila mtu akionekana kufikiria lake. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira za Benedict zilivyozidi kumkamata. Hakulipenda kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge, hakumpenda mshirika yeyote ndani ya kanisa lile, kila mtu alionekana kuwa adui namba moja katika maisha yake.
   Huku kila mmoja akifikiria lake, mara simu ya mkononi ya Benedict ikaanza kuita, akaitoa kutoka mfukoni. Kabla hajapokea, akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile, macho yake yakatua katika namba ambayo ilikuwa ngeni machoni mwake. Akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka sikioni.
   “Upo wapi Benedict? Mbona sikuoni hapa nje?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza.
   “Wewe nani?” Benedict aliuliza.
   “Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi”
   Benedict hakutaka kuongea kitu chochote kile, akakata simu, akainuka kitandani na kuanza kuelekea nje. Alipofika nje, akaanza kuangalia katika kila upande. Macho yake yakatua katika uso wa mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi ambaye alimuonyeshea ishara ya kumuita. Benedict akaanza kupiga hatua kumfuata mwaname yule.
   “Hebu tusogee pembeni kidogo” Mwanaume yule alimwambia Benedict na kuanza kusogea pembeni. Hata kabla mzee yule hakuongea chochote, akatoa kitambulisho chake na kumuonyeshea Benedict.
   “Uchunguzi wenu umeishia wapi?” Benedict aliuliza.
   “Kwamba baba yako hakujinyonga”
   “Unasemaje?”
   “Huo ndio ukweli. Hakujinyonga bali alinyongwa”
   “Umejuaje?”


 Unataka niwe nakutumia CHOMEZO watu 200 wa kwanza kulike PAGE YA 2JIACHIE Mtatumiwa imbox chomezo LIKE PAGE YETU HAPA ==>www.facebook.com/2jiachie

ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

No comments

Powered by Blogger.