KAJALA,WEMA HEBU NISIKILIZENI KIDOGO!
Mastaa wa filamu Bongo, Wema Sepetu na Kajala Masanja.
KWENU,Mastaa wa filamu Bongo, Kajala Masanja na Wema
Sepetu. Poleni kwa tifu linaloendelea kati yenu. Hongereni kwa kazi za
kila siku za kujipatia kipato. Tuweke mambo yote pembeni, mimi kama kaka
yenu, hebu tuzungumze kirafiki kidogo leo.Nimefuatilia kwa karibu ugomvi unaoendelea kati yenu, moyoni imeniuma na nimeona naweza kuwashauri mawili matatu, nanyi mkiona inafaa, muyachukue kama dira ya tatizo lililopo kati yenu.
Inawezekana wakati Kajala akifanya hivyo, alikuwa na nia njema tu, lakini Wema akahisi labda mwenzake anajisikia! Ni kawaida, hatuwezi kufanana mioyo na mawazo.
Tatizo ni pale wanapotokea watu wengine ambao wanakuza huo ugomvi. Kuna watu wanajiita Team Wema, hao nadhani hawana kazi. Wanakesha kwenye mitandao ya kijamii kuchochea huo ugomvi.
Jamani, thamani ya milioni 13 kwenye matatizo inafanana na kiasi kama hicho kwenye furaha? Siamini kama Wema anazitaka hizo fedha. Alizitoa kwa moyo kwa lengo la kumsaidia rafiki yake.
Niliona picha zilizopigwa mahakamani, wote mlikuwa mnamwagika machozi. Naamini hayakuwa ya kinafiki – ilikuwa furaha. Kwa nini leo mtofautiane kwa jambo dogo? Hata kama ni kubwa, maana inawezekana mna kitu kingine mnachogombania ambacho sikijui, lakini bado nasema kuna kila sababu ya kumaliza hizi tofauti.
Ninyi ni binadamu, najua mna mioyo, najua kila mmoja anaamini katika imani yake. Uadui umekatazwa kwenye vitabu vyote vitakatifu. Visasi vimezuiwa kabisa kwenye vitabu vyote. Hekima na busara ni sifa njema.
Kusameheana ni kitu kinachoonesha uungwana wa hali ya juu kwa binadamu mkamilifu. Bado mnayo nafasi ya kuzungumza. Hakika nawaambia, mnapoteza mambo mengi ya maana kwa kuendekeza hilo bifu.
Asitokee mtu akatumia kigezo hicho kuwagombanisha. Huu ugomvi unaweza kuwa na faida kwa watu wengine, siyo ninyi. Mlaanini shetani.
Nawapenda sana dada zangu. Ni furaha yangu kuwaona pamoja tena mkili songesha kwenye tasnia yenu. Ni wakati wenu wa kutafakari! Inawezekana.
Yuleyule,
Mkweli daima,
............................
Joseph Shaluwa

Post a Comment