ad

ad

Loga, Pluijm wafanyiana umafia mazoezini

YANGA ipo Bagamoyo ikijinoa kwa mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, Simba nayo ipo jijini Dar ikijinoa na ligi kuu, lakini habari ya kushangaza ni kuwa, makocha wa timu hizo ni kama wanaibiana mbinu, kwani kila kinachofanywa upande huu, mwingine naye anajibu.
Hali hiyo imekuwa ikitokea katika mazoezi ya timu hizo ambapo gazeti hili limeshuhudia mbinu zao zikifanana licha ya kuwa wapo kwenye viwanja tofauti.

Hali hiyo ilitokea juzi Jumatano, ambapo awali Championi Ijumaa lilipofika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers asubuhi, lilishuhudia Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, akiwafundisha wachezaji wake sawa na kitu ambacho Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic naye aliwafundisha wachezaji wake siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Kinesi jijini.

Kwenye mazoezi ya Yanga, Pluijm, raia wa Uholanzi, aliwatenga washambuliaji na mabeki na kuwapambanisha kila fowadi na beki wake huku akiwaelekeza mafowadi cha kufanya wanapokutana na mabeki wanaowakaba kila kona.

Pluijm alikuwa akiwapa mbinu mbalimbali jinsi ya kuwakaba washambuliaji hasa wenye chenga na spidi kali.
Upande wa Logarusic, naye aliwagawa kwa kuwatenganisha washambuliaji na mabeki kisha akaanza kuwaelekeza jinsi ya kukaba kama vile alivyokuwa akifanya Pluijm.
Tofauti iliyojitokeza ni kuwa, baadaye Loga aliamuru mafowadi waje wawili dhidi ya beki mmoja na kipa mmoja langoni.

“Tuna mechi ngumu kipindi hiki, ya kwanza ni dhidi ya Ruvu Shooting, halafu kubwa na ngumu ni dhidi ya Al Ahly, kwa hiyo maandalizi lazima tuanze mapema,” alisema Pluijm.
Upande wa Loga alisema: “Ni mazoezi mazuri yanayojenga mchezaji binafsi na timu kwa jumla, yanajenga zaidi umakini pale inapotokea wanakabana fowadi dhidi ya beki peke yao, itasaidia kwa aina ya wachezaji nilionao.”

CHANZO NI CHAMPIONI IJUMAA
Powered by Blogger.