Loga apiga marufuku chenga za Messi
Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic.
Hans Mloli na Ibrahim MussaKOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amemnyooshea kidole kiungo wake machachari, Ramadhani Singano ‘Messi’ akimtaka kuachana na ‘show game’ na badala yake aangalie anacheza vipi na wenzake kulifikia goli la wapinzani na kufunga mabao.
Kocha huyo raia wa Croatia alisema kuwa ameanza kuwapa mazoezi maalum wachezaji wake ya kutokaa na mipira muda mrefu ili waweze kuwa na mbinu nyingi za kuomba mipira na kusonga nayo mbele.
Alisema kuwa inapotokea mchezaji anakaa na mpira muda mrefu na kupiga chenga kama anavyofanya Messi huwa inaigharimu timu kwani wachezaji wengine wanapokaa wanausubiri mpira huwa wanaishiwa na morali ya kuupokea mpira wanaoutaka muda ule.
“Sawa, unapiga chenga lakini unaangalia kwa muda huo unaopiga chenga timu inahitaji nini kwanza, nimekuwa nikimuona Messi anamsubiri mtu ampige chenga badala ya kupasiana na wenzake waupeleke mpira mbele wakafunge mabao,” alisema Loga na kuongeza:
“Kwa hiyo sasa nitakazania zaidi kuona pasi za haraka kwenye kikosi changu bila ya chenga zisizo na msingi.”
Wakati huohuo, kwenye mazoezi yaliyofanyika juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar, Messi aliagizwa na kocha wake huyo kufanya mazoezi ya peke yake pembeni mwa uwanja baada ya kumaliza mazoezi ya awali na wenzake.
Loga alisema: “Nimemwambia Messi ajifue mwenyewe sababu sitamtumia kwenye mechi inayokuja dhidi ya JKT Ruvu, ana kadi tatu za njano.”
Post a Comment