CHADEMA YADINDA:YARUKA KIHUNZI CHA HUJUMA ZA CCM ‘KUMTUMIA’ ZITTO
JITIHADA
za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mzozo kati ya Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe, na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
zinaelekea kugonga mwamba.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya kutosha
katika hujuma dhidi ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani wa
chama hicho kuunda mgogoro na kukipasua.
Hata hivyo, licha ya misukosuko na kelele kutoka kwa baadhi ya
wanachama na wanaodhaniwa kuwa ‘mapandikizi’, CHADEMA kimeweza kupuuza
hujuma hizo na kujikita katika harakati za ujenzi wa ngazi za chini za
chama katika vijiji na vitongoji.
Kwa sasa viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika majimbo 103
nchi nzima kujenga chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu lililoketi
mwishoni mwa mwaka jana, kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko, na
ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi unaokuja.
Baadhi ya wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali wamekuwa
wanashirikiana na wana CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya
CHADEMA mtandaoni na mitaani. Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango
na kuyapeperusha katika mikutano inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama
hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk. Kitila
Mkumbo na Samson Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu,
Dk. Kitila amevuliwa wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba
amevuliwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za
‘usaliti’.
Katika kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama wamekuwa
wakitoa matamko, huku wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika
mikoa ya Lindi na Singida.
Huku wakitoa shinikizo kwa chama Zitto asichukuliwe hatua zaidi,
baadhi yao mkoani Kigoma walikwenda mbali wakitaka chama kiahirishe
ziara ya Dk. Slaa mkoani humo hadi baadaye, kwa kisingizio cha usalama.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisisitiza kuwa masuala ya usalama
yamezingatiwa barabara, na kwamba ziara
ziko pale pale, kwani hakuna
mkoa au wilaya ya mtu.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa uongozi wa CCM mkoani Kigoma, chini
ya Dk. Aman Walid Kabourou, umekuwa ukiratibu vitisho na fujo katika
mikutano au maeneo anayotembelea Dk. Slaa kwa lengo la kutisha wananchi.
Dk. Kabourou aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya
CHADEMA kabla ya kukimbilia CCM miaka kadhaa iliyopita. Alipohamia CCM
akapewa ubunge wa Afrika Mashariki. Sasa ndiye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kigoma.
Makundi ya vijana wa CCM na wana CHADEMA wenye matatizo na chama,
wamekuwa wakisambazwa kuelekea maeneo kadhaa kwa lengo la kuhujumu
mikutano ya Dk. Slaa.
Lengo ni kutumia fursa hii kujaribu kudhoofisha uwezo wa chama kinachohatarisha utawala wa CCM.
Miongoni mwa mikakati ya kuivuruga CHADEMA inayofadhiliwa kwa gharama
kubwa ni kuwapandikiza vijana kufanya fujo katika mikutano ya Dk. Slaa.
Katika mikutano hiyo vijana mbalimbali wamekuwa wakijitokeza na
mabango ya kupinga uamuzi wa kuondolewa kwa Zitto, kuzomea na kufanya
vituko vyenye lengo la kuharibu mikutano hiyo.
Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililotokea juzi katika Kijiji cha
Mabamba wilayani Kibondo, ambako zaidi ya vijana saba walikamatwa na
kufikishwa kwenye kituo cha polisi.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwapo eneo la tukio waliwatambua
kuwa wengi wao ni vijana wa CCM ambao wamekuwa wakizunguka katika
mikutano yote anayofanya Dk. Slaa.
Katika mikutano yake mkoani Shinyanga na Kigoma, Dk Slaa, alisema
propaganda za udini, ukabila na ugaidi zinazopandikizwa na CCM zimezidi
kuimarisha chama chake katika safari ya kuelekea Ikulu mwaka 2015.
Dk. Slaa alisema wanaosema CHADEMA itakufa hawajui kinachoendelea,
kwa sababu ya uamuzi wa kuwachukulia hatua au kuwaondolea nyadhifa watu
wasiotaka kufuata maadili, katiba na miongozo ni njia ya kukipa uhai
chama hicho.
“Mimi nilidhani CCM wangeshangilia chama chetu kufa, lakini hiki
ninachokiona kinanistaajabisha; yaani eti wanatuonea huruma sisi tusife?
Huu ni muujiza,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, limekuwa likidokezwa kuwa viongozi wa CCM
wamekuwa wakifadhili harakati za kuidhoofisha CHADEMA ili wasipate
upinzani mkali katika uchaguzi ujao.
Wiki iliyopita kupitia ukurasa wake wa facebook, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (bara), Mwigulu
Nchemba aliandika kuwa Mkurugenzi
wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila aliyekuwa Kigoma
alipigwa na wafuasi wa Zitto hadi kushindwa kusimama hadi aliposaidiwa
na polisi.
Wakati Mwigulu akituma maneno hayo kupitia ukurasa wake, Kigaila
amesema kuwa yeye yupo katika ziara ya kujenga chama mkoani Mbeya, na
aliondoka Tukuyu kwenda Njombe kwa kazi hiyo hiyo.
Wakati wana CCM wakishangilia kile kinachoitwa mpasuko ndani ya
CHADEMA, Dk. Slaa anasema wanazidi kuimarika na watafanya vizuri zaidi
katika chaguzi zijazo.
Katika mazungumzo yake na Tanzania Daima, wiki iliyopita, Dk. Slaa
aliwataka Watanzania wawe makini, kwani hao wanaotoa matamko ya kulaani
Kamati Kuu wanafanya kazi ya CCM, hata kama baadhi yao wana kadi za
CHADEMA.
“Wanaojitokeza kutoa matamko kulaani Kamati Kuu ya CHADEMA
hawazungumzi bei ya umeme kupanda, hawazungumzi hali mbaya ya elimu na
afya nchini, hawazungumzii suala la mishahara ya wafanyakazi, wamejikita
kumjadili Mbowe na Slaa.
“Niwahakikishie wanachama na Watanzania wanaotaka mabadiliko kuwa
tuna usalama uliokomaa tunajua hujuma zote, ndio maana jana Naibu Katibu
Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, aliwatangazia Watanzania kuwa Mkurugenzi
wetu wa Oganaizesheni na Mafunzo Benson Kigaila amepigwa na wafuasi wa
Zitto na amesaidiwa na polisi wala hajiwezi hata kusimama.”
Dk. Slaa alisema wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa chama hicho
wapo kwenye majimbo 103 nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa chama ngazi ya
msingi, kutekeleza uamuzi wa Baraza Kuu. Alisisitiza kuwa ziara hizo
hazina uhusiano na propaganda zinazosambazwa sasa kuhusu hatua ya chama
hicho kumvua vyeo Zitto.
CREDIT: TANZANIA DAIMA

Post a Comment