Zimbabwe waahidi burudani Uwanja wa Taifa leo
MSAFARA wa wachezaji na viongozi 30 wa timu ya taifa ya Zimbabwe ‘The
Warriors’ uliwasili kwa mafungu jana mchana kuikabili Tanzania ‘Taifa
Stars’ huku ukiahidi soka la uhakika leo.
Taifa
Stars mazoezini.
Awali Stars ilikuwa ishuke kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam saa 10 alasiri kuumana na Kenya ‘Harambee Stars’, kabla ya
Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kujitoa na hivyo Tanzania kuamua
kuwasaka Zimbabwe, ambapo kipute kinatarajiwa kuanza saa 11:00 jioni,
leo.
Kikosi cha Zimbabwe kiliwasili jana saa 8:05 mchana, kwa ajili ya
pambano hilo lililo ndani ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa), kikiwa na msafara wa watu 30 kwa ndege ya Kenya Airways kutoka
Zimbabwe kupitia Nairobi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Kocha wa Stars, Kim Poulsen,
alijinasibu kuwa kikosi chake kiko tayari kwa changamoto ya kuivaa
Zimbabwe, aliyoitaja kama kipimo kizuri zaidi kwake kuelekea michuano ya
Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Kikosi kiko imara na tuna kila sababu ya kushinda pambano hilo, hasa
baada ya nyota muhimu kuwasili kuungana nasi katika kambi ya
maandalizi,” alisema Poulsen akiwataja wakali hao kuwa ni
Thomas
Ulimwengu, Mbwana Samatta na Mwinyi Kazimoto.
Stars inacheza mechi hiyo kabla ya kuvunjwa ili nyota walioteuliwa
timu ya taifa ya Tanzania Bara
‘Kilimanjaro Stars’ na ile ya Zanzibar
‘Zanzibar Heroes’ kujiunga nazo tayari kwa Chalenji inayotarajiwa kuanza
Novemba 27 jijini Nairobi Kenya.
Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), Mkuu wa Msafara, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya
Chama cha Soka cha Zimbabwe (Zifa), John Phiri, alisema wako imara na
tayari kuwavaa Taifa Stars.
Phiri alisema kuwa vijana wake wako kamili kila idara na kwamba
mashabiki watarajie burudani nzuri kutoka kwa nyota wa The Warriors,
ingawa hawakuja na mchezaji yeyote anayecheza soka nje ya Zimbabwe.
“Tumewaacha nyota wanaocheza nje sio kwa kuidharau Taifa Stars, bali
tuko katika kukiimarisha kikosi kitakachoshiriki Fainali za Mataifa
Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN 2014), zitakazofanyika kuanzia Januari
11 hadi Februari 1 mwakani.
Katika fainali hizo zitakazofanyika katika miji mitatu nchini Afrika
Kusini, Zimbabwe imepangwa kundi B, ikiwa na Uganda, Burkina Faso na
Morocco, ambapo Phiri anaamini Stars itakuwa kipimo sahihi kuelekea
maandalizi yao ya mwisho wa mwaka.
Waamuzi wa mechi ya leo wanatoka Uganda, wakati Kamishna atakuwa
Leslie Liunda wa Dar es Salaam, huku mwamuzi ni Oden Mbaga pia wa Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
viingilio vya mechi ya leo vitakuwa ni sh 5,000 kwa viti vya rangi ya
bluu na kijani, viti vya rangi ya chungwa sh 10,000, VIP C sh 15,000,
VIP B 20,000 na VIP A sh 30,000.
Nyota wa Kilimanjaro Stars watakaochaguliwa baada ya mechi ya leo,
wataweka kambi jijini Arusha kujiandaa na michuano ya Chalenji jijini
Nairobi Kenya.
Arusha imechaguliwa kutokana na hali ya hewa kuwiana na ya Nairobi.
Post a Comment