ad

ad

Mashine za TRA majanga eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam

WAFANYABIASHARA wa maduka eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam wametangaza mgomo kwa muda usiojulikana hadi pale serikali itakapofanyia mabadiliko njia mpya za ukusanyaji kodi zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), za kutumia mashine za kielektroniki (EFD).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam mshauri wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Johnson Minja, alisema kuwa walikuwa wakitafuta mawasiliano ya Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda kuweza kukaa meza moja ili kutafuta njia bora ya muafaka wa ukusanyaji kodi kwa njia nyingine badala ya kutumia mashine hizo.

Minja alisema kuwa njia iliyotumiwa na TRA ya kutumia mashine hizo imeonekana kuwa mwiba kwa wafanyabiashara wengi wa eneo hilo kutokana na wengi wao kukosa uwezo wa kununua mashine hizo.

Alisema kuwa serikali imekuwa ikiwabana zaidi wamiliki wa maduka pekee huku wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) wakiachwa na kuendelea na biashara pasipo kulipa kodi.

Mshauri huyo alisema kuwa hawailaumu TRA kwa kuwa jambo hilo ni la kisera na viongozi ndiyo watekelezaji ila aliiomba serikali kuwasikiliza na kukutana na wafanyabiashara hao ili kujadiliana kuhusiana na matumizi ya mashine hizo.

“Tatizo hilo lisingefikia hapo kwa kuwa tumekuwa tukiandika barua tangu Septemba mwaka huu na kuzipeleka kwa Waziri wa Viwanda na Biashara ili tukae meza ya majadiliano lakini hatukufanikiwa kuonana naye kutokana na kubanwa na kazi,” alisema.
Powered by Blogger.