ad

ad

Rage awapanga mashabiki wamshangilie

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Rage, amewapanga mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa ajili ya kumshangilia.

 Tukio hilo la aina yake lilifanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Msimbazi jijini Dar es Salaam, mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari, jana.
 
Mwenyekiti huyo akisubiriwa na kundi kubwa la mashabiki hao nje ya ofisi hiyo ya Simba, alionekana na kusikika akiwapanga kwa ajili ya kumshangilia.
 
Rage alimuita pembeni mmoja wa makomandoo wa klabu hiyo na kumtaka ashuke kutoka ghorofani haraka na kwenda kuwaambia mashabiki wajiandae kwa ajili ya kumshangilia akiwa anatoka mjengoni hapo.
 
Mwenyekiti huyo alisikika akiwaambia waandishi wa habari: “Mnataka mnione nikiwa nashangiliwa na mashabiki, basi subirini muone nitakavyoshangiliwa.
 
“Anzeni nyie waandishi wa habari kuanza kushuka chini mkiwa na kamera zenu muone nitakavyoshangiliwa, ndiyo muamini kuwa napendwa.”
Waandishi bila kujali, haraka wakashuka chini na kukuta kundi la mashabiki waliokuwa wanamsubiri mwenyekiti kwa shauku kubwa kwa ajili ya kumshangilia.
 
Mara baada ya kushuka chini alipokewa na mashabiki hao kwa shangwe kwa kumpa mikono na wengine kumnyooshea wakimpongeza na kumtaka aendelee kukaa madarakani.
 
Aliposhuka chini alisimama kama dakika tano kwa ajili ya kuzungumza na mashabiki hao na baadaye kuelekea kwenye gari aina ya Toyota V6 Granvia lenye namba T 300 CPR.
 
Baada ya kuingia kwenye gari alifungua dirisha la juu la gari hilo na kusimama na kuwapungia mikono mashabiki hao wachache ambao walikuwa wakiimba Simba! Simba! Simba! Simbaaa! Kwa sauti kali hadi gari hilo lilipoondoka likisukumwa na kundi hilo.
Powered by Blogger.