KIBADENI KOCHA MPYA ASHANTI
KOCHA Mkongwe nchini Abdallah ‘King’ Kibadeni amekubali kutua na kuifundisha Ashanti United ambayo iko katika wakati mgumu.
Ashanti iko katika wakati mgumu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na
imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi ya 12 kati ya timu 14.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Ashanti zimeeleza, tayari
mazungumzo kati ya Kibadeni na kocha huyo yamefanyika, naye ameridhia
kutua huko.
“Tayari mazungumzo yamefanyika, naweza kusema ni asilimia 90 tuko
katika makubaliano na Kibadeni na amekubali kuja kuifundisha timu yetu.
Amesema lile agizo la Rage kumrudisha yeye amelikataa na hatabaki
Simba,” kilieleza chanzo.
“Kwa kuwa ametuhakikishia, basi tumeanza kuandaa kila anachotaka na
tunasubiri tu amalizane na Simba kuchukua haki yake ili aanze kazi hapa
Ashanti.”
Alipotafutwa Kibadeni, jana mchana, alikiri kufanya mazungumzo na Ashanti lakini akasisitiza suala hilo litabaki kuwa siri.
“Kweli siwezi kubaki Simba, huo ni ukweli. Lakini kuhusiana na Ashanti na mambo mengine yote ya Simba nitayazungumza Jumamosi.
“Nimeitisha mkutano na waandishi wa habari, nimewaomba waje kwangu
Madale, saa nne kamili asubuhi. Nitaeleza kila kitu kuhusiana na Simba
na hata Ashanti, hivyo leo siwezi kuzungumza zaidi,” alisema Kibadeni.
Kibadeni
na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walifukuzwa kazi na kamati ya
utendaji lakini mwenyekiti aliyesimamishwa, Ismail Aden Rage
akawarudisha na kujirudisha madarakani akisema kamati hiyo haikufuata
katiba.
CREDIT: GPL

Post a Comment