Wawili wanaswa na maiti yenye dawa za kulevya..
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa
tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina
ya heroin tumboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo,
Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri
Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa
Kigogo Luhanga.
“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa
raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi
baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo”
alisema.
Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na
kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali
katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.
“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema
marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama
Mashaka Mabruki” alisema.
Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda
alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na
alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.
Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na
kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu,
ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi
33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya
fedha.
“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa
usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa
akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.
Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa
usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote
watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.
Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo
vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya
Ushelisheli.
Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba
raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara
makubwa kwa wananchi, hasa vijana. VIA HABARI LEO.

Post a Comment