Upinzani ‘wawasha moto’ Zanzibar,wataka Chikawe ajiuzulu.
Waziri wa
Sheria na Katiba Mathias Chikawe ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za
uongo kwamba Zanzibar ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya
Katiba kuwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa
Sheria na Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia
mkutano wa hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar
ilipokea taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada
wa Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo
yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya
mabadiliko ghafla viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar
kupewa nafasi ya kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa
katika kupata katiba bora.
"Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai," alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri
akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Bunge, William Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo
kwa siku moja jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
"Baada ya kuanza kupiga kelele,
wenzetu walikuja Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya
mswada,nikawaambia siwezi kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni
kuiuza nchi, siko tayari kufanya hilo," alisema.
Aboubakari alisema marekebisho
yaliyofanyika katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha
mabadiliko ya Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba
yanapaswa kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu
ambao ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa
Tanzania.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias
Chikawe kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana
kweupe kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu
ya muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi
muswada pia walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao
cha Bunge na kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka
kabla ya kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho
ya vifungu vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na
michango ya wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa
kisheria.
"Baada ya kamati ya Bunge kukaa,
Mbunge Halima Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa
utaratibu wa wingi wa kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba
kama hatua ya theluthi mbili itashindwa kufikia mwafaka," alisema
Chikawe.
Pia alisema mbunge kupitia Baraza la
Wawakilishi, Jaku Hashim Jaku yeye alitetea kwa nguvu ya hoja kuwa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imalize kazi yake baada ya kuwasilisha ripoti
yake kwa Rais na kwamba haikuwa ni uamuzi na matakwa ya Serikali kama
inavyodaiwa na vyama vya upinzani kuhusu nyongeza hiyo.
"Nyongeza ya vifungu ilitokana na
wabunge katika kamati na ndani ya Bunge lenyewe, Serikali haiwezi
kupuuzia ushauri wa wawakilishi wa wananchi na wabunge ambao
wanaisimamia Serikali," alisema Waziri Chikawe.
Aidha, Aboubakari alimshutumu Naibu
Spika wa Bunge,Job Ndugai kwa kulidanganya Bunge kwa kitendo chake cha
kutoa barua ikithibitishaZanzibar imeshiriki wakati kuna vifungu vya
ziada vimefanyiwa marekebisho bila ya kupata baraka ya Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo amevunja na
kukiuka kanuni za Bunge na wabunge wana haki ya kumshtaki kwa kutumia
kanuni zao kwa kupotosha Bunge na umma.
Hata hivyo, taarifa hizo za Aboubakari
kutokana na maelezo aliyotoa awali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad kwenye mkutano wa hadhara, alisema Zanzibar ilishirikishwa
katika kuvifanyia vifungu sita na SMZ ilitoa mapendekezo katika vifungu
vitatu na baadae vikaongezwa vinane kinyemela bila ya Zanzibar
kushirikishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kwa muda mrefu viongozi wa Zanzibar
walikuwa wakijitolea kupigania mabadiliko ya taifa lao na kukutwa na
vizingiti ikiwemo kuwekwa vizuizini na kupewa hongo ya madaraka.
Mbatia alisema miongoni mwa viongozi
waliojitoa muhanga kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano ni pamoja na
Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambaye aliondolewa
kibabe madarakani chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Frederick Werema na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias
Chikawe kwa madai kuwa hawana nia njema wakikusudia kuharibu nia njema
ya Rais ya kupata Katiba mpya.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema Katiba iliyopo sasa nchini haifai kwa kuwa imejaa
upungufu unaokwenda kinyume na misingi ya haki za raia.
Chanzo:Mwananchi

Post a Comment