Dk. Willibrod Slaa: Mwakyembe fisadi.
WAZIRI wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe,
ametuhumiwa kuhusika na vitendo vya kifisadi, kinyume kabisa na msimamo
wake kabla hajapewa uwaziri.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk.
Willibrod Slaa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk.
Willibrod Slaa, ndiye aliyerusha tuhuma hizo juzi mjini hapa alipokuwa
akihutubia mamia ya wakazi wa wilaya hii katika mkutano wa hadhara.
Dk. Slaa aliwaeleza wana Kyela Dk. Mwakyembe ambaye awali
alionyesha umakini katika uchapaji kazi, amebadilika mara tu baada ya
kupewa uwaziri na kujiingiza katika vitendo vya kifisadi, ikiwemo hatua
yake ya kugawa eneo la wazi kwa Shirika la Sukita ambalo liko chini ya
CCM kinyume na taratibu.
Katibu huyo aliyeongozana na Mbuge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(Sugu), mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, na viongozi wengine
waandamizi alisema Dk. Mwakyembe mbali na utoaji wa zabuni hiyo kwa
Sukita pia anazo tuhuma zingine zaidi ya sita za vitendo vya ufisadi
vinavyodaiwa kufanywa na Mwakyembe na kwamba anajiandaa kuziweka
hadharani.
“Ndugu wananchi najisikia furaha jinsi mlivyojaa katika uwanja huu na
hii inanidhihirishia mmechoka na vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na
mbunge wenu pamoja na chama chake.
“Sisi kama wapinzani tunasikitika hasa pale alivyosema atawataja kwa
majina wauza unga, lakini hadi leo hajawataja kwa hali hiyo inaonyesha
wazi kuwa kiongozi huyo ni mbabaishaji,” alisema Dk. Slaa.
Pamoja na hayo aliwataka wananchi wa Kyela waungane na wananchi
wengine nchini kuunga mkono jitihada za umoja wa vyama vya CHADEMA,
NCCR Mageuzi na CUF ambao wameamua kuunganisha nguvu zao kwa pamoja
kuhakikisha katiba inapatikana bila ya uchakachuaji, ili itumike kwa
maslahi ya watanzania na si kwa maslahi ya wachache.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, aliwataka wananchi wa Kyela
kuwaunga mkono kwa jitihada wanazozifanya bungeni kwani wameamua
kufanya hivyo kwa maslahi ya taifa na hawatarudi nyuma mpaka kieleweke.

Post a Comment