Zuku kutoa tuzo za filamu ZIFF
KAMPUNI ya Wananchi Group kupitia king’amuzi chake cha Zuku
inatarajiwa kutoa tuzo na fedha katika vipengele vitano vipya vya filamu
katika Tamasha la Nchi za Majahazi (ZIFF), linalofanyika Zanzibar.
Akizungumza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa hivi
karibuni, Mkurugenzi wa Wananchi Group, Hanellie Bekker, alisema tuzo
hizo zinazotarajiwa kutolewa Julai 6, mwaka huu ni maalumu kwa ajili ya
filamu za Kiswahili.
Bekker alisema filamu hizo zitahusisha muigizaji bora wa kike,
muigizaji bora wa kiume, filamu bora na muongozaji bora wa filamu
ambapo kila mmoja ataondoka na sh 500,000 pamoja na tuzo, huku kipengele
cha filamu bora mshindi ataondoka na kitita cha sh milioni moja.
Alisema filamu zitakazoshindanishwa ni Laptop, Maduhu, Bikira Kidawa, Woman of Principles, Nakwenda kwa Mwanangu, Room No.13,
Crush/Husuda, C.I.D, Network, Mdundiko, Fungate, Lovers Island, Changu na Chips Kuku.
“Tunafurahi kwamba katika mwaka wetu wa pili wa udhamini ZIFF tumeweza
kujumuisha tuzo maalumu za Zuku kwenye tamasha la ZIFF. Tuzo hizi
hazitoi mwanya tu kwa washindi kupata zawadi bali pia kuboresha kazi zao
na kuzifanya ziwe na viwango vya kimataifa.
“Tunafanya jitahada za kuwazawadia filamu za Kiswahili na pia
kutambua jitihada za wasimuliaji wazuri wa hadithi wazawa kupitia sanaa
ya filamu, tunaamini kuwa tuzo zetu zitachangia ukuaji wa sekta hii,”
alisema.
Alisema vigezo vitakavyotumika katika kupata filamu bora vitahusisha
ubora wa kazi, simulizi na mchezaji, uigizaji na uelekezaji wa filamu.
Katika kutafuta muigizaji bora wa kike na kiume, vigezo
vitakavyotumiwa ni pamoja na uelewa wa ‘script’, kujituma, kujenga
hisia, kutoa utendaji ambayo ni mzuri kwa ufanisi wa uzalishaji wa jumla
wa utendaji.

Post a Comment