Obama akanyaga Tanzania • Ulinzi mkali kila kona, Tanzania yakosolewa.
HAYAWI hayawi sasa yamekuwa baada ya Rais wa Marekani, Barack
Obama, kuwasili nchini jana kuanza ziara yake ya kiserikali ya siku
mbili akitokea Afrika Kusini.
Rais Obama ambaye alipata mapokezi makubwa ya wananchi na viongozi
mbalimbali, walioongozwa na Rais Jakaya Kikwete, aliwasili katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere saa 8:36 akiongozana na mkewe
Michelle pamoja na watoto wao wawili, Sasha na Malia.
Mara baada ya kuteremka kwenye ndege yake ya Air Force One, Rais
Obama, alikumbatiana na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso E. Lenhardt
na mkewe, kisha akasalimiana na mwenyeji wake, Rais Kikwete na Mama
Salma.
Rais Obama alikwenda moja kwa moja kwenye jukwaa dogo kisha kupigiwa
nyimbo mbili za Tanzania na Marekani zilizoambatana na mizinga 21, kisha
akakagua gwaride na vikundi vya ngoma za asili.
Huku akishindwa kujizuia kutokana na burudani hiyo, Rais Obama
alijikuta akisakata ngoma na mwenyeji wake, Rais Kikwete na baadaye
alisalimiana na viongozi kadhaa wa kiserikali na mabalozi kisha viongozi
hao walielekea Ikulu kwa mazungumzo.
Wakati wote ulinzi mkali wa maofisa usalama wa Marekani kwa
kushirikiana na wale wa nchini uliimarishwa kila kona, ambako wananchi
wengi walifurika mitaani kumlaki kiongozi huyo.
Baada ya mazungumzo mafupi ya faragha, viongozi hao walikuja mbele ya
waandishi wa habari kwa ajili ya kuulizwa maswali mbalimbali.
Waandishi na maswali
Kinyume cha matarajio ya wengi, waandishi wa habari wa Tanzania
walionekana kutopewa nafasi ya kutosha kufanya kazi zao kwa uhuru
kutokana na kupangwa katika eneo moja wakati wote wa matukio.
Hata ilipofika mkutano wao na marais hao, waandishi walipigwa butwaa
kuona watu wanne pekee wakitajwa kuuliza maswali ambapo ni swali moja tu
liliruhusiwa kwa waandishi wa Tanzania.
Pia maswali yaliyoulizwa hayakuwa na manufaa sana kwa Tanzania, kwani
ukiachilia mbali swali la Mtanzania Peter Ambirikile wa gazeti la Jambo
Leo, aliyeuliza kama marais hao wanaridhika na misaada ya miradi ya MCC
inayotolewa na Marekani, waulizaji wengine walijikita kwenye migogoro ya
mataifa ya Afrika.
Katika hotuba yake Rais Obama alisema maendeleo katika nchi za Afrika
ikiwamo Tanzania yataletwa na Waafrika wenyewe, kwani Marekani
inachofanya ni kuchochea miradi ya maendeleo.
Pamoja na hayo, alipongeza Tanzania kuwa na utawala bora, Bunge bora na hata kuendesha siasa za upinzani kwa amani.
Pia alipongeza Tanzania kuingia katika mchakato wa kupata Katiba mpya
pamoja na kumpongeza Rais wa Zanzibar kwa kufanikisha kupata Katiba
mpya.
Alisema anafurahi kusikia kuwa misaada wanayotoa imekuwa na matokeo
chanya kwa
Watanzania kutokana na kupunguza vifo vinavyotokana na
ugonjwa wa malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto kupungua.
Pia alisema mradi wa MCC umefanikiwa kwa Tanzania na kwamba itaingia katika awamu ya pili ya mradi huo.
Kuhusu mradi wa umeme wa Power Africa, alisema nchi nne ndizo
zitafaidika na kwamba wametenga dola za Marekani bilioni saba
kufanikisha mradi huo.
Aidha, alisema wataongeza fedha katika nchi za Afrika katika kukabiliana na magendo na ujangili.
Alisema ingawa ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania, amefurahishwa na mapokezi maalumu aliyopata.
Rais Obama katika kujibu maswali ya migogoro hiyo ya Afrika katika
nchi za Congo (DRC) na Misri, aliwaasa watawala kuheshimu wapinzani na
kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Awali, Rais Kikwete, alisema Tanzania inaendelea kufurahia uhusiano
wake na Marekani na kwamba misaada inayopata katika sekta mbalimbali
imekuwa na faida kwa Watanzania.
Alitoa mfano kuwa misaada katika sekta ya afya imesaidia kupunguza
vifo na misaada katika sekta ya elimu imesaidia kuongeza idadi ya
wanafunzi shuleni.
“Misaada mingine tunayopata ni katika usalama wa chakula, umeme na maji,” alisema.
Alisema Marekani imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kulingana na
mahitaji ya Tanzania na kutoa mfano katika miradi ya barabara,
upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na umeme vijijini.
“Tunaridhika na misaada tunayopata kupitia mradi wa MCC…nikisema hatujaridhika rais atakataa maombi mengine,” alisema.
Alisema misaada ya Marekani kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha
maisha ya Watanzania na kumuomba ikiwa anaweza kuendelea kuisaidia
Tanzania afanye hivyo.
Kuhusu swali la ofisa wa ubalozi, Allan Mzengi, anayetuhumiwa
kumdhalilisha kijinsia msichana wa Kitanzania, hatua iliyoilazimu
Tanzania kulipa fidia alisema:
“Nalijua suala hilo, lilihusu msichana mdogo wa ofisa wetu wa
ubalozi, walimchukua vizuri kwa lengo la kumsaidia kielimu, lakini
kulitokea tofauti za kifamilia, yule msichana akashtaki akasema
anafanyiwa vitendo vya unyanyasaji.
“Nakubali kulikuwapo na suala hilo ila faini iliyotolewa ilikuwa ni
kubwa sana, hata kwa pensheni yangu ambayo nitalipwa baada ya kustaafu
urais isingetosha kumlipa huyo, hata hivyo sehemu ya malipo hayo
imekwisha kufanywa,” alisema Kikwete.
Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC One) ambacho pekee ndicho kilikuwa
kikirusha matangazo hayo, mawasiliano yake yalikuwa yakikatika mara kwa
mara, hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakifuatilia ziara
hiyo kupitia runinga hiyo au nyingine zilizokuwa zimejiunga na kituo
hicho.
Tanzania yakosolewa
Katika hatua nyingine, wakati Rais Obama akipokewa kwa bashasha,
gazeti maarufu nchini Marekani la The New York Times, limechapisha
habari za kuonesha matukio ya ukatili yanayofanyika Tanzania.
Habari hiyo iliyochapishwa katika toleo lake ya Juni 30, imeleza tukio
la kuteswa na kuumiza kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen
Ulimboka.
Mwandishi wa habari hiyo amejaribu kunukuu kauli ya Dk. Ulimboka
akieleza jinsi alivyotekwa na kuteswa kinyama kisha kutupwa kwenye Msitu
wa Mabwepande.
Anasema kuwa Tanzania inaheshimika nje ya nchi kama kisiwa cha amani ndani ya ukanda wenye machafuko wa Afrika Mashariki.
Kwamba kutokana na sifa hizo, Tanzania imejizolea sifa na ufadhili wa
fedha kutoka kwa mataifa mbalimbali yaliyoendelea, ikiwamo Marekani,
ambayo mwaka jana iliipatia zaidi ya dola milioni 480.
Alisema kuwa wakati Rais Obama akiwasili Tanzania makundi ya kutetea
haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wanasema matukio ya vitisho
na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa yanashika kasi. “Kuna woga, si
amani”.
Ananukuu kuwa waandishi wamekuwa wakishambuliwa na mmoja aliuawa akiwa anatekeleza kazi yake ya uandishi wa habari.
Aliongeza kuwa Julai mwaka jana, serikali ililifungia gazeti huru la
uchunguzi la kila wiki la
Mwanahalisi, ambalo lilikuwa likiandika kwa
undani kuhusu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, ambalo
lilihusisha uhalifu huo na serikali ya Rais Kikwete.
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari yenye makao makuu yake New York
nchini Marekani, wiki jana ilimtaka Rais Obama kuliibua suala la uhuru
wa vyombo vya habari atakapokutana na Rais Kikwete jijini Dar es Salaam.
Gazeti hilo pia limetaja vurugu za kisiasa kuwa zilichukua sura mpya
na ambayo haikutegemewa wakati bomu la kurushwa kwa mkono lilipolipuliwa
katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa madiwani wa CHADEMA
na kusababisha vifo vya watu wanne mkoani Arusha.
“Hivi ni vitisho” ananukuliwa Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa
CHADEMA. “Watu wataogopa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na wale
jasiri watakuwa wameuliwa”.
Kwamba viongozi wa CHADEMA wamesema wazi wazi kwamba mtu aliyerusha
bomu ni polisi au analindwa na polisi. Wamesema chama chao kipo tayari
kuutoa mkanda wa video kuthibitisha tuhuma hizo, lakini lazima iwe mbele
ya tume huru ya uchunguzi.
Lakini pia ananukuliwa kamishna wa Polisi anayehusika na operesheni,
Paul Chagonja akipuuza tuhuma hizo na kuziita kuwa hazina msingi wowote,
na alisema kuwa chama hicho kinapaswa kufikisha mikononi mwa polisi ili
ufanyiwe kazi.
“Kazi ya msingi ya polisi ni kulinda usalama wa watu, hatufungamani na chama chochote cha siasa,” alisema Chagonja.
Pia ziara hiyo ya Rais Obama imekosolewa na wakazi wengi jijini Dar es
Salaam, walidai kuwa imewaathiri katika shughuli zao za kiuchumi
kutokana na kuhamishwa kwa muda katika maeneo yao ya biashara.

Post a Comment