UCHAGUZI TFF KUFANYIKA SEPTEMBA 29 MWAKA HUU.

Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka
huu baada ya ule wa Dharura wa marekebisho ya Katiba ulipangwa kufanyika
Julai 13 mwaka huu.
Tarehe hizo zimepangwa na kikao cha
dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo (Mei 9 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais wake Leodegar Tenga
ambacho kupokea rasmi maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) na kupanga utekelezaji wake.
“Kamati
ya Utendaji ya TFF imepokea rasmi barua ya FIFA na kupanga utekelezaji
wake. Tumepokea maagizo ya FIFA yanayotuelekeza cha kufanya, si TFF wala
mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Maagizo
ni undeni Kamati ya Maadili, Kamati ya Rufani ya Maadili, fanyeni
marekebisho ya Katiba, anzeni tena uchaguzi, waliokuwepo na wengine
wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe kabla ya Oktoba
30 mwaka huu kama FIFA walivyotuagiza,” amesema Rais Tenga wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha
kanuni hizo, kwani Kamati za Maadili lazima ziwe na kanuni zake na
kuhakikisha kuwa hakuna mgongano kati ya Kanuni za Nidhamu na Kanuni za
Maadili.
Pia Rais Tenga amesema kuna kazi ya
kuangalia jinsi zitakavyoingia katika uchaguzi ambapo maana yake muda wa
mchakato wa uchaguzi utakuwa zaidi ya siku 40 za sasa, hivyo mabadiliko
hayo yatagusa vilevile Kanuni za Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji,
rasmu ya mwanzo ya Kanuni hizo inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30
mwaka huu ambapo itapelekwa FIFA kwa ajili ya kupata mawazo yao kabla ya
kuendelea na hatua inayofuata.
Juni
15 mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana kupokea mapendekezo
hayo ambapo baada ya kuyapitisha itayapeleka tena FIFA. Taarifa (notice)
ya Mkutano Mkuu wa Dharura ambayo kikatiba ni siku 30 itatolewa Juni 12
au 13 mwaka huu.
Baada
ya Mkutano Mkuu wa Dharura wa marekebisho ya Katiba, Kamati ya Utendaji
itakutana kati ya Julai 14 na 15 mwaka huu kuunda Kamati ya Maadili na
Kamati ya Rufani ya Maadili ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi uanze.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment