MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO.
MARAFIKI na mpenzi wako ni nani bora? Kabla hujajibu fumba kwanza macho
kisha tafakari. Umeshapata jibu? Usijibu, hebu vuta picha kwa mara ya
pili, fanya tafakuri ya kina kisha lipime jawabu lako. Kile ambacho
umepata ndiyo muongozo wa kila siku katika maisha yako.
Hata
hivyo, naomba nikupe changamoto kupitia hilo jibu lako. Kuna kipindi
marafiki wanaweza kuwa muhimu kuliko mwenzi wako, vilevile zipo nyakati
zikifika, haitawezekana kumpa rafiki kipaumbele kuliko mpenzi wako. Hapa
inataka maarifa na akili tulivu kuchanganua.
Rafiki anaweza kuwa
muhimu kipindi unamsoma mwenzi wako. Hata hivyo, umuhimu wake una ukomo,
kwani hatakiwi kuchukua akili yako au kumpa hata asilimia 50 ya mawazo
juu ya kile ambacho unataka kukiamua. Asilimia 15 zinamtosha, kisha
zingatia; akili za kuambiwa changanya na zako.
Maisha yako yapo
ndani yako mwenyewe. Unachohitaji au kukitamani katika maisha yako ya
kimapenzi, unakijua wewe. Kama ndivyo, basi tambua kuwa ukimsikiliza
sana rafiki, anaweza kukupotosha. Matokeo yake anaweza kukufanya uishi
ndani ya matarajio yake.
Wewe na yeye, kila mmoja ana sifa zake
anazoziangalia kwenye mapenzi. Una sifa ambazo unadhani mwenzi wako
akiwa nazo maisha yako yatakuwa na furaha, naye anavyo vipengele ambavyo
anataraji ‘waubavu’ wake awe navyo ili amani na upendo vitawale.
Mathalan, unaamini kuwa mwenzi wako anapaswa kuwa mtanashati, mzuri wa
umbo na sura lakini mwenzako anaamini kwamba vyote hivyo ni sawa lakini
kama tabia yake siyo nzuri hafai. Hapo utakuwa umeshaona namna ambavyo
wewe na yeye mnatofautiana.
Unaamini katika mpenzi mwenye mapenzi
ya kweli, anayejali, mwelewa, asiye na gubu, mwaminifu, rafiki yako
kipaumbele chake ni kumpata mwenye fedha. Hapo ikupe picha kuwa wewe ni
wewe na yeye ni yeye. Ukizubaa, utapoteza matarajio yako kwa sababu ya
kushikiwa kichwa na rafiki yako.
Ni dhambi kubwa, tena ni usaliti wa
hali ya juu kuacha misingi ambayo wewe unaamini inaweza kukupa furaha,
utulivu na amani ya moyo na kufuata ushauri wa rafiki yako ambaye hana
uwezo wa kusoma hisia zako na kujua nini hasa unahitaji. Atadhani upo
kama yeye, kwa hiyo atakwambia ufuate anachopenda yeye.
Ipo mifano
ya watu wanaoteseka leo kwa sababu ya kupotoshwa na marafiki. Walikuwa
na wapenzi wazuri sana, waliokuwa wanasikilizana nao lakini wakaachana
baada ya kushauriwa ndivyo sivyo. Picha iliyo wazi kwa sasa, mapenzi
kuwa na vurugu nyingi, ikufanye uelewe mantiki ya hoja ambayo naijenga.
Kama marafiki wenyewe wanachukuliana wapenzi, ni kwa nini isikupe
sababu ya kuamini kwamba wewe upo sahihi zaidi kwenye uamuzi wako kuliko
mshauri? Pengine akakujaza maneno ya chuki kwa mwenzi wako, mwisho
ukamwona hafai, baada ya majuma mawili unagundua yupo naye.
Ukiweka
pembeni hoja ya kuchukuliana wapenzi, ukweli mwingine ni kwamba rafiki
anaweza kukufanya uachane na mwenzi wako mnayependana na kuelewana
vizuri ili ukajiweke kwa mwenye fedha. Mwisho wa hilo siku zote kuna
majuto, kwa maana pesa itakuwezesha kutatua mambo mengi lakini haziwezi
kukupa penzi linalokidhi moyo.
Kama ambavyo umewahi kushuhudia
mateso ya mtu kulazimishwa kuoa au kuolewa na yule asiyempenda kwa
sababu mbalimbali, hususan kichocheo cha shinikizo la wazazi, ndivyo
hutokea pale uhusiano unapojengwa na fedha. Shika neno hili kuwa
binadamu ni rahisi sana kuzizoea fedha pale anapokuwa anazipata.
Anapozoea maisha ya fedha, moja kwa moja humuona wa kawaida sana, yule
mwenzi wake aliyemkubali kwa sababu ya mali. Ni hapo ndipo humsaka yule
atakayempa tulizo la kweli la moyo. Vitendo vya wenye fedha wengi
kusalitiwa, ikupe sababu ya kuyazingatia haya.
Kwa nini baadaye uje
kuvuna aibu ya kuonekana msaliti? Amua leo kwamba pamoja na hali yoyote
ya kimaisha uliyonayo na mwenzi wako, mtalindana kwa shida na raha. Yote
yanawezekana, endapo kwa maelewano yenu na nia ya dhati, mtajitolea
kusaka maisha bora zaidi, yatapatikana tu.
Itaendelea wiki ijayo.

Post a Comment