Yanga, Azam kutimuana kileleni leo
Vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanashuka Uwanja wa
CCM Kirumba Mwanza leo kucheza na Toto African, huku Azam FC wanaoshika
nafasi ya pili, nao wakiisubiri nyumbani Chamazi, Polisi Morogoro.
Mechi hizo zina ushindani mkali hasa ukizingatia
kuwa, timu hizo zinashika nafasi ya kwanza na pili, hivyo mshindi
atazidi kujiongezea matumaini ya kutwaa ubingwa.
Lakini kwa upande mwingine, wapinzani wa Yanga na
Azam nao wana kibarua kigumu cha kujaribu kujinusuru na janga la
kuporomoka daraja, hivyo ili kuepuka hali hiyo ushindi ni lazima.
Yanga iko kileleni na pointi 42 baada ya mechi 18 ikifutiwa na Azam yenye pointi 36. Polisi Moro ya tutu kutoka mikiani ikiwa na pointi 16, wakati Toto African iliyoshinda mechi mbili tangu Septemba 15 mwaka jana, inashika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 14.
Katika mechi ya kwanza msimu huu kati ya Yanga na
Toto zinazoelezwa kuwa 'ndugu', Wanajangwani waliibuka na ushindi wa
mabao 3-1 yaliyofungwa na Jerryson Tegete, Mbuyu Titwe na Didier
Kavumbagu.
Hivyo basi, Toto watashusha kikosi cha kutaka kulipa kisasi hasa ukizingatia watakuwa Uwanja wa nyumbani na vilevile kuepuka kushuka daraja.
Kocha wa Yangam, Ernest Brandts amesema mchezo huo
utakuwa mgumu kwa vile Toto wamepata nguvu zaidi baada ya kuwa na
uhakika wa huduma kutoka serikali ya mkoa tofauti na awali.
Hofu kubwa ya Yanga ni kumkosa kipa namba moja, Ally Mustapha ëBarthezà aliyekuwa mgonjwa, lakini jana aliweza kufanya mazoezi mepesi na bado haijajulikana kama ataweza kucheza
Kocha wa Toto Africans, John Tegete amesema amekiandaa vizuri kikosi chake kupata ushindi kwenye mechi ya leo.
"Tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na vijana wangu wataingia uwanjani kwa kazi moja tu ya kusaka ushindi kwa nguvu zote bila ya kujali uhusiano wetu na Yanga," alisema Tegete.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mechi moja
itikayopigwa Uwanja wa Taifa kati ya Mabingwa watetezi, Simba dhidi ya
Coastal Union ya Tanga.

Post a Comment