ad

ad

Mhasibu OUT apandishwa kizimbani

MHASIBU wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Engles Mrikaria (42), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kughushi mishahara hewa na kujipatia Sh milioni 578.5 kwa njia ya udanganyifu.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani jana, mbele ya Hakimu Mkazi Agnes Mchome, akasomewa mashitaka na kuunganishwa katika kesi inayomkabili Katibu Muhtasi wa Chuo cha Biashara Tanzania (CBE), Rose Maungu.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa, alidai Mrikaria anakabiliwa na mashitaka matatu ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kosa la kutakatisha fedha haramu ambalo kisheria halina dhamana.

“Mrikaria katika tarehe tofauti kati ya Julai 2009 na Aprili 2011, mkoani Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu alighushi orodha ya wapokea mishahara.

“Alionyesha kuwa Rose Maungu, Boniface Msofe, H. Kiungu na M. Mohammed ni waajiriwa wa OUT, hivyo wanastahili kulipwa mishahara ya mwezi ya Sh 578,501,001.

“Shitaka la pili linalomkabili Mrikaria ni la kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa katika kipindi hicho, mkoani Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu alijipatia fedha hizo kutoka katika akaunti namba 011103002560 ya OUT iliyoko Benki ya NBC, tawi la Corporate.”

Wakili huyo alisema kuwa mshitakiwa huyo alijipatia fedha hizo baada ya kudanganya kuwa fedha hizo zilikuwa mishahara ya kila mwezi kwa watumishi hao kwa kipindi cha Julai 2009 na Aprili 2011.

Mutakyawa alidai mshitakiwa Mrikaria anakabiliwa na shitaka jingine la kutakatisha fedha haramu, ambapo kwa njia ya udanganyifu alihamisha fedha hizo kutoka katika akaunti ya OUT kwenda katika akaunti zilizopo benki mbalimbali.

Mrikaria inadaiwa alihamishia fedha hizo katika akaunti zinazomilikiwa na Rose Maungu, East Africa Procurement Service, Judiana Stationery, S. M Mushi, B. J. Msofe, A. Mrakari, Pricila Mbwasi, huku akijua kwamba zimetokana na kosa la kughushi.

Shitaka la nne ambalo ni la kutakatisha fedha haramu, linamkabili Rose, ambapo anadaiwa kuwa kati ya Aprili 2010 na Mei 2011, mkoani Dar es Salaam, alijipatia Sh milioni 68 kutoka katika akaunti ya OUT iliyopo Benki ya NBC, tawi la Corporate, wakati akijua fedha hizo zimetokana na kosa la kughushi.

Powered by Blogger.