Kiza kinene kesi ya Lwakatare..
HABARI NA TANZANIA DAIMA
Mbowe asema huo ni mtiririko wa mabavu ya dola
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimfutia
kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph,
kisha kuwakamata tena na kuwafungulia kesi mpya yenye mashitaka
yaleyale.
Awali ilielezwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka ( DPP), Dk. Eliezer
Feleshi, aliwasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa sababu hana
haja ya kuendelea nayo.
Hata hivyo baada ya kuachiwa, Lwakatare na mwenzake walikamatwa tena
na kufikishwa mahakamani hapo kisha kufunguliwa kesi mpya namba 6/2013
ambayo imepangiwa kwa Hakimu mpya, Aloyce Katemana.
Katika kesi ya awali namba 37/2013 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya
Lwakatare na wenzake Machi 18, mwaka huu, jana ilikuwa imekuja kwa ajili
ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, kuitolea uamuzi wa ama kuwapatia
dhamana washitakiwa hao au la.
Lakini Hakimu Mchauru alijikuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwa
sababu mawakili viongozi wa serikali, Ponsian Lukosi, Prudence
Rweyongeza na Peter Mahugo, waliwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya
kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka
2002.
“Kwa kuwa kesi hii Na. 37/2013 ilifunguliwa na upande wa Jamhuri Machi
18, mwaka huu, na leo kesi hii ilikuja kwa ajili ya mahakama kutolea
uamuzi wa maombi ya washitakiwa kupatiwa dhamana au la, pamoja na maombi
mengine…mahakama hii inasema haitaweza kutoa uamuzi wake kwa sababu DPP
amewasilisha hati ya kutotaka kuendelea kuwashitaki, hivyo mahakama hii
inawafutia kesi washitakiwa wote,” alisema Hakimu Mchauru.
Baada ya Hakimu Mchauru kuwafutia kesi, askari kanzu waliwakamata tena
washitakiwa hao na kuwaweka chini ya ulinzi na ilipofika saa 4:20
asubuhi, waliingizwa tena katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo
mbele ya Hakimu Mkazi mwingine, Aloyce Katemana.
Mawakili wakuu wa serikali, Lukosi, Rweyongeza na Peter Mahugo walidai
kuwa kesi hiyo ni mpya na imepewa Na. 6 ya mwaka huu, ambapo
washitakiwa ni Lwakatare na Ludovick wanaotetewa na mawakili wa
kujitegemea Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatara.
Walisema kuwa hati hiyo ina mashitaka manne, ambapo shitaka la kwanza
linaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na makosa
matatu yote yanaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Wakili Rweyongeza alilitaja kosa la kwanza ambalo linawakabili
washitakiwa wote kuwa ni kula njama kutenda kosa la jinai kinyume cha
kifungu cha 284 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alidai kuwa mnamo Desemba 28, mwaka jana, huko Kimara
King’ong’o Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka
kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Dennis Msacky, ambaye ni Mhariri
Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.
Alilitaja kosa la pili kuwa ni la kula njama ambalo pia ni kwa ajili
ya washitakiwa wote, ikiwa ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha Sheria
ya Kuzuia Ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002, kwamba washitakiwa hao walitenda
kosa la ugaidi la kutaka kumteka Msacky.
Shitaka la tatu ambalo pia linawakabili wote wawili ni kupanga kufanya
makosa ya ugaidi kinyume cha kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia
ugaidi, kwamba Desemba 28, mwaka jana, walishiriki katika mkutano wa
kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msacky.
Rweyongeza alidai kuwa shitaka la nne linamkabili Lwakatare peke
yake, ambalo ni kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume cha
kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.
Kwamba, Desemba 28, mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki wa nyumba
hiyo iliyopo Kimara King’ong’o kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa
kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka
kumteka nyara Msacky.
Washitakiwa wote walikanusha mashitaka hayo na Hakimu Katemana alisema
hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya
kusikiliza kesi hiyo, hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3, mwaka
huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa utetezi Kibatara, aliomba mahakama isikilize ombi lake
alilokuwa akitaka kuliwasilisha, lakini Hakimu Katemana alisema yeye
ndiye kiongozi na mawakili wa utetezi na Jamhuri wapo chini yake na
kwamba ana majukumu mengine hivyo hayupo tayari kusikiliza ombi hilo
wala lile la upande wa Jamhuri.
Jamhuri iliomba mahakama imruhusu Ludovick aende kushikiliwa na Jeshi
la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kipelelezi lakini hakimu huyo
akaamuru washitakiwa wapelekwe gerezani.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wafuasi wa CHADEMA ambao baadhi yao
walikuwa wamevalia sare walipaza sauti na kusema: “People’s Power.
Hakuna kulala hadi kwanza walale wao.”
Mbowe anena
Akizungumza nje ya viwanja vya mahakama baada ya kesi kuahirishwa,
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kwanza asingependa
kuingilia mtiririko wa mahakama.
Hata hivyo alizungumza kwa kifupi akisema kuwa wao wanafanya kazi za
mageuzi kwa ajili ya kuwatetea raia wanyonge na maskini na kwamba
kilichompata Lwakatare si kigeni, bali ni mtiririko wa mabavu ya dola
dhidi ya wanamageuzi.
Lissu ang’aka
Akizungumza kwa simu, Wakili maarufu, Tundu Lissu, ambaye alikuwa
miongoni mwa wanajopo wa utetezi wa Lwakatare katika kesi ya kwanza,
alisema kitendo cha kumfutia kesi mshitakiwa kabla hajajibu mashitaka na
kumfungulia mashitaka yaleyale, kinaonesha ni matumizi mabaya ya
taratibu za kimahakama.
Alisema ni kitendo cha kutumia vibaya mahakama ili hakimu asitoe
majibu kwa mambo ambayo yalikuwa yanatarajiwa kutolewa uamuzi jana.
“Leo tulitarajia kuwa tunakuja kujadili kama Lwakatare anapata dhamana
au hapana, na pia kuja kuzungumzia kama mashitaka ambayo yaliletwa
mahakamani yalikuwa na hati ya ridhaa ya DPP. Tulijiandaa kwa hayo, wala
si mengine, sasa wamefika mahakamani wakamfutia mashitaka na
kumfungulia mengine,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa, mashitaka ya Lwakatare pamoja na kutajwa kuwa ni
ya kigaidi, yapo katika kanuni za adhabu kama makosa ya kawaida kwa
mujibu wa sheria kifungu cha 384, hivyo ni makosa yanayodhaminika.



Post a Comment