Chadema wasalimu amri kwa polisi, wasitisha maandamano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekubali kusitisha
maandamano yaliyokuwa yafanyike leo kushinikiza kujiuzulu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kutokana na matokeo
mabaya ya kidato cha nne ya 2012.
Makubaliano yalifikiwa baada ya kikao cha Mkuu wa
Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said
Mwema na viongozi wa Chadema walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kilichofanyika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Mwema na viongozi wa Chadema walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kilichofanyika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, IGP Mwema alikuwa na Kamishna
wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Suleimani Kova na maofisa wengine wa ngazi za juu wa jeshi
hilo.
Mbowe katika ujumbe wa Chadema aliambatana na Katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Deogratius Munishi na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Taarifa ya pamoja ya polisi na Chadema
iliyosainiwa na Makene na Msemaji wa Mkuu wa Polisi, Advera Senso
ilisema baada ya kushauriana, walikubaliana kusitisha maandamano hayo
ili kutoa nafasi ya wananchi kushiriki katika mapokezi ya ugeni wa Rais
wa Jamhuri wa Watu wa China, Xi Jinping.
“Pia katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema na IGP Mwema walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya siku 14 ili kuona utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana na kushirikiana pasipo migogoro kwa pande zote mbili, huku kila upande ukitimiza wajibu wake kwa masilahi ya taifa, “ ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Chadema waliingia katika mvutano mkali na
polisi kutokana na kuzuiwa kwa maandamano yao, ambapo kabla ya
makubaliano ya jana walikuwa wamesisitiza kwamba yangefanyika hata kama
polisi wangetumia nguvu kuyazuia.

Post a Comment