MTU
mmoja, Omar Mussa Makame (35), mkazi wa Mwanakwerekwe Zanzibar,
amekamatwa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kwa tuhuma za mauaji ya
aliyekuwa Padri wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Evaristus Mushi. Taarifa
hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Mussa
Ali Mussa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Kamishna Mussa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 13, mwaka
huu, katika Mtaa wa Kariakoo, Zanzibar na atafikishwa mahakamani baada
ya taratibu zote kukamilika.
“Huu ni mwanzo tu, kwani Jeshi la
Polisi linaendelea na upelelezi wa kitaalamu ili kuhakikisha watu wote
wanaohusika na matukio ya uhalifu hapa Zanzibar, wanakamatwa na
kufikishwa katika mkondo wa sheria.
“Jalada la mtuhumiwa huyu
tayari limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria
kwa sababu yeye ndiye atakayetupa mwongozo juu ya suala hili.
“Kabla mtuhumiwa hajakamatwa, tulifanya upelelezi kwa kutumia michoro na
alipokamatwa, watu waliokuwa eneo la tukio siku ambayo padri aliuawa,
walimtambua kwamba ndiye aliyekuwapo.
“Lakini, kwa kuwa
tulikuwa tumeahidi zawadi ya shilingi milioni kumi kwa atakayesaidia
kukamatwa kwa watuhumiwa na kwa kuwa mtuhumiwa huyu amekamatwa kwa
msaada wa wananchi, aliyesaidia kukamatwa, atakabidhiwa fedha zake
katika mazingira ya usiri kwa ajili ya kulinda usalama wake.
“Pamoja na kazi nzuri tunayoifanya kwa kushirikiana na wananchi, bado
tunahitaji msaada wao katika harakati zetu za kukabiliana na uhalifu,”
alisema Kamishna Mussa.
Padri Mushi aliuawa na watu
wasiojulikana kwa kupigwa risasi kichwani Februari mwaka huu, wakati
akiingia katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Mtakatifu Theresia,
Zanzibar.
Baada ya watu hao kufanya mauaji hayo, walitoweka kwa
kutumia pikipiki waliyokuwanayo wakati wanamsubiri padri huyo awasili
kanisani hapo.
Kutokana na uzito wa tukio hilo, Jeshi la Polisi
nchini, lilifanya upelelezi kwa kuwashirikisha wataalamu wa masuala ya
upelelezi kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ambao waliwasili
Kisiwani Zanzibar na kuchora michoro kuonyesha jinsi mauaji hayo
yalivyofanyika.
Juzi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu
la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuonyesha jinsi
asivyoridhishwa na ukimya wa upelelezi wa kuuawa Padri Mushi na
kujeruhiwa kwa risasi, Padri Ambrose Mkenda.
Post a Comment