Waumini wamuaga Papa
Maelfu ya watu wamekusanyika katika uwanja wa kanisa la mtakatifu Petro
wakihudhuria tukio la mwisho la baba mtakatifu Benedict wa 16 la
kuwaombea waumini hadharani,
Hiyo ni ibada ya mwisho ya baba mtakatifu ya mwisho ya hadhara ya siku
ya Jumapili kabla ya kuachia kabisa nafasi hiyo ya kuliongoza kanisa
katoliki duniani.
Kimsingi misa hiyo ya mchana ya jumapili huwavutia watu wachache ikiwa
ni pamoja na watalii lakini mara hii wamejitokeza maelfu kwa maelfu ya
waumini katika uwanja huo kumshuhudia kwa mara yao ya mwisho papa
Benedict. Inasaidikiwa kwamba watu 150,000 wanahudhuria misa hiyo ya
wazi katika uwanja wa mtakatifu Petro.
Wamuaga
Baadhi ya watalii wamesikika kusema kwamba wamefika katika uwanja huo
kumuaga na kumtakia mema na zaidi ya yote, mtalii kama Amy Champion
aliyetokea Uingereza anasema inahitaji ujasiri kufanya kazi ya Papa na
vile vile wakati unapoamua kuachia ngazi.
Kuanzia Jumapili Jioni baba mtakatifu hatoweza kuonekana tena mbele ya
hadhara katika kipindi cha wiki nzima, ambacho kanisa mjini Vatican
linaanza kipindi maalum cha maombi na tafakari. Jumapili hii uongozi wa
mji wa Roma uliongeza usafiri wa mabasi na Treni za chini kwa chini ili
kusaidia kukabiliana na msongamano wa watu waliokuwa wanamiminika
kuelekea Vatican pamoja na kutowa usafiri wa bure wa mabasi madogo kwa
ajili ya wakongwe na walemavu.
Kujiuzulu kwake
Kiongozi wa kanisa Katoliki baba mtakatifu Benedict wa 16
aliushtuwa ulimwengu wiki iliyopita kwa kutangaza anajiuzulu kuanzia
Februari 28, kitendo ambacho hakijawahi kushuhudiwa na kanisa hilo kwa
kipindi cha miaka 600. Wakati Makadinali wakitazamiwa kumchagua mrithi
wake mpya katika kikao maalum cha siri, baba mtakatifu Benedict mwenye
umri wa miaka 85 atakuwa katika mapumziko na kufanya ibada katika makazi
ya kanisa huko Kusini mashariki mwa mji wa Roma.
Baada ya wiki kadhaa anatazamiwa kuhamia kwenye makaazi mengine yaliyoko
kwenye eneo la Vatican ambako ataishi maisha ya kitawa. Makao makuu ya
kanisa hilo Katoliki mjini Vatican hayajatangaza tarehe ya kuanza kwa
kiao cha siri cha kumchagua kiongozi mpya lakini yametangaza kwamba
kikao hicho huenda kikafanyika mapema kabla ya mwezi March 15 na tarehe
hiyo mpya inaweza kutangazwa chini sheria za sasa za kanisa.
Uchaguzi wa papa mpya
Papa atahitajika kutia saini juu ya tarehe hiyo kitendo ambacho
kitakamilisha kabisa kipindi chake cha takriban miaka 8 ya uongozi wa
kanisa. Wakati huohuo tayari makadinali wameshaanza kuwasili Roma kuanza
kipindi cha kujadiliana kwa mujibu wa sheria za kanisa kuamua ni kina
nani walio wagombea wenye nafasi nzuri ya kuchukua wadhifa huo wa papa.
Askofu mkuu Robert Sarah mzaliwa wa Guinea, ambaye ni kadinali
anayeongoza ofisi ya misaada ya Vatican amewaambia waandishi wa habari
kwamba viongozi wa kanisa watapaswa kumchagua papa mpya kwa utulivu na
kuaminiana.

Post a Comment