Waziri mwingine aihujumu CHADEMA
BAADA ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wassira kutajwa kuwa nyuma ya mkakati wa kukihujumu Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waziri mwingine ametajwa kufadhili
kundi la vijana wasaliti wa chama hicho.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumamosi, umebaini kuwa kigogo huyo wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni naibu waziri wa wizara moja nyeti,
juzi alifadhili kikao cha kutathimini athari za tamko la aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti wa wa Baraza la Vijana la
CHADEMA Taifa (BAVICHA)
aliyefukuzwa, Juliana Shonza.
Naibu huyo pia anadaiwa kutumia siasa za ukanda na ukabila kuwarubuni vijana waliofukuzwa uanachama wa BAVICHA.
Baadhi ya vijana hao waliofukuzwa uanachama na kuungwa mkono na naibu
waziri huyo, ni Shonza, Mtella Mwampamba aliyekuwa mgombea ubunge wa
Jimbo la Mbozi Mashariki 2010 na Habib Mchange aliyegombea Kibaha Mjini.
Vijana hao walivuliwa uanachama baada ya BAVICHA kujiridhisha kuwa
walikuwa wakitumiwa na CCM pamoja na baadhi ya viongozi wawili ndani ya
CHADEMA ili kutoa matusi kwa viongozi waandamizi wa chama na kuwazushia
uongo.
BAVICHA pia iliwataja Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM),
Martine Shigella na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba, kuwa
nyuma ya mkakati huo.
Mmoja wa wajumbe walioshiriki kikao hicho juzi usiku, alisema kuwa watatathmini kazi aliyokuwa amepewa Shonza.
Alisema kuwa Shonza alipewa kazi ya kutoa tamko la kuwatukana viongozi
wakuu wa CHADEMA, kukishambulia chama na kuwashambulia baadhi ya
viongozi wa BAVICHA, hasa mwenyekiti wake, John Heche.
“Tulikutana pale Mikocheni kwenye nyumba moja, tukajadili kwa mapana
mkutano wa Shonza na waandishi wa habari baada ya kufukuzwa. Sikujua
nyumba ni ya nani, lakini aliyekuwa mwenyeji zaidi ni Shigela,” alisema.
Aliwataja wengine waliohudhuria kikao hicho kuwa ni Mwampamba, Tambwe
Hiza, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, Salumu Hapi
pamoja na Katibu
Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, Wareni
Kamnyoge.
“Katika mkutano ule, Shigella alimuuliza Shonza anaendeleaje baada ya
kutoa tamko na athari zake kwa jamii. Shonza alijieleza na baadaye
wajumbe wakamsifu kwa kusema CHADEMA ni chama cha Wachaga na cha
ukanda,” aliongeza.
Aliongeza kuwa Shigella alisema kuwa; “Hapa kwenye ukanda na ukabila,
nakwambia Juliana umetufurahisha. Maana sasa, tutakuwa tumefanikiwa
sana. Tutatembea na agenda hii hadi mwaka 2015.”
Shigela hakupatikana kuthibitisha madai hayo, lakini Tambwe aliliambia
gazeti hili kwa ufupi kuwa; “Mikakati ya kuwatumia vijana wa CHADEMA
inaendelea vizuri.”
Akizungumza kwa kujiamini, Tambwe alisema juzi hakwenda Kinondoni hasa
Mikocheni, lakini akathibitisha kuwa; “unachokisema cha kuwatumia
vijana wa CHADEMA ni kweli maana mikakati ni ushindi katika uchaguzi
mkuu 2015.”
Kuhusu kuwapokea CCM vijana hao, Tambwe alisema hayo mengine ya
kutumika au kupokelewa waulizwe viongozi maana hao ndiyo wasemaji.
Shonza hakupatikana ili kuzungumzia madai hayo, ingawa kuna taarifa
kuwa wameahidiwa kazi kulingana na elimu zao. Shonza inadaiwa kuwa
ataajiriwa kwenye kazi za ustawi wa jamii, Mwampamba ameahidiwa ualimu.
Chanzo hicho kinaongeza kuwa, kwa mujibu wa mkakati huo, Shonza na
kundi lake, wamepanga kufanya ziara mikoani, wakianzia Mbeya, Iringa na
baaye Mwanza.
Naibu waziri anayedaiwa kuwafadhili inasemekana anatumia ukabila na
ukanda akisema kuwa waliofukuzwa ni vijana wa Mbeya, na hivyo anataka
kuwatumia kuivuruga CHADEMA mkoani humo hasa Jimbo la Mbeya Mjini
analojitapa kutaka kulirejesha CCM.

Post a Comment