Simba yapigwa tena Oman
MABIGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom, Simba SC, wameendelea kufanya
vibaya katika michezo yao ya kirafiki nchini Oman, baada ya jana
kutandikwa mabao 3-1 na timu ya Qaboos kwenye Uwanja wa Qaboos nchini
humo.
Kwa mujibu wa kocha wa zamani wa Simba, mwenye makazi yake nchini
Oman, Talib Hilal, licha ya kipigo hicho, Simba ilionyesha kandanda safi
na ya kuvutia, huku bao la kufutia machozi likipachikwa na
mshambuliaji, Haruna Moshi ‘Boban’.
Simba ambayo iko huko tangu wiki iliyopita, kwa kambi maalumu ya
kujiandaa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na Ligi ya
Mabingwa Afrika, juzi ililala bao 1-0 kwa timu ya taifa ya Vijana ya
Oman chini ya miaka 23.
Aidha Simba inayonolewa na Patrick Liewig, inatarajiwa kucheza mechi
nyingine ya kirafiki na Fanja Fc, kabla ya kurejea nchini Januari 23,
tayari kwa kuanza mzunguko wa pili wa ligi unaotarajiwa kuanza kutimua
vumbi Januari 26.

Post a Comment