ad

ad

Twite, Mustapha wafunika Uturuki

KIRAKA wa Yanga, Kabange Twite na kipa Ally Mustapha wamemkolea kocha Ernest Brandts baada ya kuwatumia katika kikosi cha kwanza kwenye michezo yote miwili waliyocheza nchini Uturuki.
Ukiacha mechi zingine Yanga ilizocheza mchangani, katika mechi dhidi ya Tusker jijini Dar es Salaam, Mholanzi huyo amewatumia Kabange na Barthez katika mechi mbili alizocheza hapa Antalya dhidi ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani na Denizlispor ya Uturuki.

Kabange raia wa DR Congo mwenye uraia wa Rwanda amecheza kwenye vikosi vyote vya kwanza kwenye mechi hizo na hajabadilishwa kama wachezaji wengine.
Kabange amekuwa akionyesha uwezo wa juu akicheza nafasi za kiungo na ushambuliaji, ambapo kocha huyo amekuwa akimbadili anavyotaka kadiri mchezo unavyoendelea na aina ya mabadiliko anayokuwa akifanya ndani ya mchezo.

Uwezo wa kucheza namba zaidi ya moja umempa faida mchezaji huyo aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili, ingawa Shirikisho la Soka la Tanzania lilitangaza kwamba usajili wake una utata kutokana na FC Lupopo kushindwa kumwidhinisha kwa Yanga katika muda mwafaka wa usajili.

Mbali na Kabange, mchezaji mwingine aliyeko kwenye fomu na ambaye amekuwa na namba ya kudumu mpaka sasa ni kipa Mustapha Barthez ambaye amecheza mechi zote.
Katika mechi dhidi ya Arminia, timu ya Yanga ilitoka sare ya bao 1-1, kabla ya juzi Jumanne kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Denilzspor ambayo mwaka 2002 ilifuzu kucheza Europa Ligi na kuzifunga timu kama Sparta Prague na Lyon kabla ya kutolewa raundi ya nne na FC Porto.

Katika mchezo huo, mshambuliaji Jerryson Tegete alifunga bao la pili katika ziara hiyo ya Uturuki alipoifungia Yanga bao la kufutia machozi.
Tegete ambaye hakuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, alifunga bao lake la kwanza kwenye mchezo dhidi ya Arminia wakati walipotoka sare 1-1 na Wajerumani hao.
Yanga ipo mjini hapa kwa wiki ya pili sasa, ambapo itaondoka Jumapili kurejea Dar es Salaam itawasili usiku wa manane.
Powered by Blogger.