Morocco Yatinga 32 Bora Licha ya Kushindwa Kileleni mwa Kundi C
Timu ya taifa ya Morocco imefuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Haiti katika mchezo wa mwisho wa Kundi C, lakini ikashindwa kutwaa nafasi ya kwanza ya kundi hilo kutokana na ushindi wa Brazil dhidi ya Scotland.
Atlas Lions walihitaji ushindi mkubwa huku wakitegemea Scotland kuizuia Brazil ili waweze kumaliza kileleni mwa kundi. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama walivyotarajia baada ya Haiti kuwashangaza mapema kupitia bao la kujifunga la kipa Yassine Bounou dakika ya tisa.
Morocco walisawazisha dakika ya 39 kupitia nahodha Achraf Hakimi, lakini Haiti walirejesha tena uongozi muda mfupi baadaye kupitia shuti kali la Wilson Isidor.
Dakika chache kabla ya mapumziko, Ismael Saibari aliifungia Morocco bao la kusawazisha na kuandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka nchi za Kiarabu kufunga katika mechi zote tatu za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Kipindi cha pili Morocco waliongeza kasi na kupata bao la tatu kupitia mchezaji wa akiba Soufiane Rahimi dakika ya 70, kabla ya Gessime Yassine kufunga bao la nne dakika ya 89 na kuhitimisha ushindi huo muhimu.
Wakati huo huo, Brazil waliendelea kuonyesha ubora wao kwa kuichapa Scotland mabao 3-0. Nyota VinÃcius Júnior alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza, huku Matheus Cunha akiongeza la tatu.
Mashabiki wa Brazil walipata furaha zaidi baada ya kuona Neymar akirejea uwanjani dakika ya 76 baada ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha.
Mwisho wa hatua ya makundi, Brazil na Morocco zote zilimaliza na pointi saba, lakini Brazil walitwaa nafasi ya kwanza kutokana na kuwa na tofauti bora ya mabao.
Msimamo wa Mwisho wa Kundi C
Brazil – Pointi 7
Morocco – Pointi 7
Scotland – Pointi 3
Haiti – Pointi 0

Post a Comment