ad

ad

Michirizi Ya Damu - 13

Michirizi Ya Damu - 13
Wakazungumza na madaktari na kumuonyeshea picha ya Fareed, kwa kuwa daktari huyo alikuwa akiwakumbuka watu aliokuwa amewapokea, hakukuwa na ugumu kugundua kwamba picha ya mtu aliyekuwa ameonyeshewa alikufikishwa ndani ya hospitali hiyo saa moja iliyopita.
“Where is him?” (yupo wapi?)
“Come with me,” (nifuateni) alisema daktari huyo na kuanza kumfuata.
Daktari yule akawapeleka mpaka katika wodi aliyolazwa Fareed ambapo akawakabidhi watu hao kwa nesi aliyekuwa akiwahudumia wagonjwa waliokuwa katika wodi hiyo. Alipoonyeshewa picha ya Fareed, alimgundua kwani alikuwa miongoni mwa wagonjwa waliokuwepo humo ndani.
“I know him,” (namfahamu)
“Where is he? (yupo wapi?)
Nesi yule akawachukua mpaka katika kitanda alicholazwa Fareed, walipofika, mwanaume huyo hakuwepo na alipomuuliza nesi mwenzake akamwambia kwamba Fareed alikuwa amekwenda chooni.
“Where is the toilet?” (choo kipo wapi?)
“Come with me,” (nifuateni) alisema na kuanza kumfuata nesi huyo kwenda huko chooni.
****
Maofisa wale wa FBI na nesi yule wakafika ndani ya choo kile, wakaangalia huku na kule, mtu waliyekuwa wakimtafuta hakuwepo humo. Nesi alishindwa kuelewa kwamba ilikuwaje Fareed asiwe humo na wakati alimuona akielekea chooni na hakuwa na uhakika kama mwanaume huyo alikuwa ametoka.
FBI hawakutaka kuridhika, walijua kwamba mwanaume huyo alikuwa ndani ya vyoo hivyo, wakaendelea kumtafuta kwenye kila choo lakini hawakuweza kumuona.
Hawakutaka kukata tamaa, waliamini kwamba kama mwanaume huyo hakuwa chooni humo basi atakuwa ametoka, na kama ni kipindi kifupi kilichopita waliamini kwamba hakuwa mbali kutoka mahali hapo.
Wakaelekea sehemu zingine ndani ya hospitali hiyo lakini hawakuweza kumuona Fareed, wakaelekea mpaka nje kabisa lakini kila kona waliyoangalia, mwanaume huyo hakuonekana machoni mwao.
“Where is he?” (yupo wapi?) aliuliza ofisa mmoja.
“I don’t know! He just went to the toilet,” (sijui! Alikwenda chooni) alijibu nesi.
****
Fareed alikuwa chooni, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, aliamini kwamba ilikuwa ni lazima kutafutwa kwani alikumbuka kwamba katika kituo kile cha treni kulikuwa na kamera ndogo za CCTV hivyo kugundulika lilikuwa suala jepesi sana.
Hakutaka kubaki humo, ilikuwa ni lazima kuondoka kuelekea popote pale lakini si kuona akikamatwa kwa kufanya jambo ambalo alilazimishwa kulifanya pasipo kujua kama lilikuwa kosa lolote lile.
Akaondoka na kuelekea nje ya choo kile, hakutaka kuonekana, aliondoka mpaka kufika nje huku akikutana na madaktari wengi ambao hawakumuuliza kitu chochote zaidi ya kumuacha tu.
Alijipekua mfukoni, alikuwa na kadi yake ya benki ambayo ilimuwezesha kuchukua kiasi chochote cha pesa sehemu yoyote ile. Akaelekea mpaka katikakibanda cha ATM na kutoa kiasi cha dola mia tano na kuondoka zake.
Safari yake iliishia katika hoteli ya kawaida ya Windows iliyokuwa hapohapo Pennyslvania, akachukua chumba ambacho alitakiwa kulipa dola mia mbili hamsini, zaidi ya laki tano kwa usiku mmoja tu.
Hilo halikuwa na tatizo, alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho angeweza kufanya jambo lolote lile, hivyo akaelekea katika chumba hicho. Hakulala, alibaki akifikiria namna alivyonusurika kuuawa kwa kulipukiwa na bomu.
Moyo wake ukawa na ghadhabu, akawa na hasira na Waarabu kwani aliamini kwamba watu hao hawakuangalia utu, hawakujua ni watu wangapi waliwakosea, katika kuua, waliua kila mtu hata kama hawakuwa na hatia kama alivyokuwa.
Hakutaka kuwafikiria sana Waarabu, alichokitaka ni kusonga mbele na kutekeleza kile alichokuwa akikitaka. Aliingia nchini MArekani kwa lengo la kumuua Bilionea Belleck ambaye aliamini kwamba alikuwa nchini humo.
Akaanza kufuatilia, alikuwa na marafiki wachache nchini humo ambao wangekuwa na data zote kuhusu bilionea huyo na kwa jinsi gani angeweza kumpata. Kwa kuwa bilionea Belleck alikuwa na maadui wengi akiwemo bilionea mwenzake, Peter Williams, alichokifanya ni kumpigia simu.
“Unanikumbuka?” alimuuliza bilionea huyo ambaye aliwahi kutambulishwa na Bilionea Belleck kabla ya wawili hao kutofautiana kwenye mambo ya kibiashara.
“Hapana!”
“Kwa hiyo namba yangu uliifuta?” aliuliza Fareed.
“Mmh! Sina uhakika! Wewe nani?”
“Naitwa Farida!”
“Yupi?”
“Yule wa Belleck!”
“Ooh! Yule wa mpumbavu?”
“Ndiyo!”
Kwa sababu watu hao walikuwa wakichukiana, Fareed aliamini kwamba angeweza kufanya naye kazi kwa ajili ya kukamilisha kile alichokuwa akikihitaji. Akamwambia mwanaume huyo kwamba walitakiwa kuonana na hivyo kama hatojali basi aende kuzungumza naye kitu ambacho kwa bilionea huyo hakukuwa na tatizo lolote lile.
Ndani ya saa moja tayari Bilionea William alikuwa mbele ya Fareed. Alimwangalia kwa umakini sana, alionekana kuwa mtu tofauti kabisa, hakuwa kama kipindi kilichopita, mwanaume mwenye muonekano wa kike, kwa kipindi hicho alikuwa mwanaume shupavu, mwenye mwili uliojazia.
Williams alibaki akimkodolea macho, hakuamini kama mwanaume aliyesimama mbele yake ndiye mwanaume yule aliyefahamiana naye kitambo. Fareed akamwambia bilionea huyo kile kilichomleta Marekani, hakuja kula starehe bali alitaka kufanya kazi moja, kumuua Bilionea Belleck.
“Kwa nini tena?”
Akamwambia sababu kwamba aliamua kufanya hivyo kwa kuwa mwanaume huyo naye alitaka kumuua ila kwa msaada wa Mungu aliweza kumtoroka na watu wake.
Williams akafurahia, chuki aliyokuwa nayo kwa Belleck ilikuwa kubwa kiasi kwamba kwa kitendo cha kuambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa tayari kumuua halikuwa tatizo kabisa.
“Kwanza hayupo Marekani,” alisema William.
“Yupo wapi?”
“Paris nchini Ufaransa,” alijibu Williams.
“Ni lazima niende huko. Utanisaidiaje kufika?” aliuliza Fareed.
Ili apate msaada wa kufika Ufaransa ilikuwa ni lazima amwambie Williams ukweli kwamba alikuwa akitafutwa kila kona. Mwanaume huyo alibaki kimya, alitaka muda wa kujifikiria ni kwa jinsi gani angemtorosha Fareed kuelekea nchini Ufaransa.
Alikaa na kuwaza sana, jibu alilokuja nalo ilikuwa ni lazima kwa mwanaume huyo asafiri kwa kutumia ndege yake binafsi ambayo ingempeleka mpaka huko.
“You will take my flight,” (utachukua ndege yangu) alisema Williams.
Hakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya huo na safari ilitakiwa kufanyika usiku. Fareed akajiandaa na baada ya siku mbili, magari mawili ya kifahari yakafika hotelini hapo na kumchukua kisha kumpeleka uwanja wa ndege.
Moyo wake ulikuwa na hofu, hakuamini kama angefika salama huko kwani kila kona alikuwa akitafutwa na FBI ambao hawakutaka kuzisambaza picha zake, walimtafuta kimyakimya ili asishtukie kama anatafutwa kumbe mwenzao alikwishajua hilo kitambo.
Uwanja wa ndege, hakupitishwa mlango wa kawaida, ndege ilikuwa ni ya binafsi tena ya bilionea mkubwa duniani, hivyo hata mlango aliopitishwa ulikuwa ni wa VIP na ilikuwa vigumu kumgundua kwamba alikuwa yeye.
Mpaka anakaa katika kiti ndani ya ndege hiyo, akashusha pumzi ndefu, hakutegemea kama ingekuwa kazi nyepesi namna hiyo. Huku nyuma, bilionea Williams alikuwa akifanya mawasiliano na watu wake waliokuwa Ufaransa, alitaka kupata data zote kuhusu bilionea huyo, kwamba alikuwa akiishi katika hoteli gani na ratiba yake ya siku ilikuwaje. Hilo halikuwa tatizo kwa vijana wake, kwa kuwa walikuwa huko na mtu huyo alikuwa maarufu, wakapata data zote na kumtumia na hivyo na yeye kumtumia Fareed ambaye baada ya kuzipokea, akamshukuru Mungu.
“Sasa kazi itafanyika,” alimwambia Williams kwenye simu.
“Ukikamilisha! Nakuahidi kukupa dola milioni kumi. Huyu mpumbavu ananinyima sana usingizi,” alisema William huku akiwa na uhakika kwamba ilikuwa ni lazima mwanaume huyo ammalize Bilionea Belleck. Ila la zaidi, alitaka kuona bilionea huyo akifa na yeye kumuua Fareed kwani kama angemuacha, siri ingeweza kuvuja. Ili siri itunzwe ilikuwa ni lazima hata naye Fareed afe.
****
Fareed hakujua mahali mwanaume huyo alipokuwa, ila aliambiwa kwamba angepewa maelezo yote kwani yale aliyopewa mara ya kwanza, yalibadilika kwani mtu huyo aliondoka Paris na hakukuwa na aliyejua kama alikwenda Monaco au Marseille.
Baada ya dakika hamsini akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa hapo Paris bali alikuwa jijini Marseille katika Hoteli ya Melkizedeki ambapo alikuwa akilala huku kila siku akishiriki katika kikao cha matajiri.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akaondoka hotelini alipokuwa, akachukua ndege na kuelekea Marseille ambapo ndipo aliambiwa mwanaume huyo alipokuwa. Njiani, alikuwa akimuomba Mungu afike salama kwani alikuwa na hasira kali, asingeweza kumuacha mwanaume huyo akaishi kwani alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kumuua kwa nguvu zote.
Walichukua dakika arobaini na tano tu mpaka kufika jiji humo ambapo akateremka na kuchukuliwa kwa gari mpaka katika hoteli moja na kutulia huko. Ilipofika saa mbili usiku, wanaume wawili wakafika hotelini hapo na kuomba kuzungumza naye.
Hilo halikuwa tatizo, alipewa taarifa na Williams kwamba watu hao wangefika mahali hapo, na wao ndiyo ambao wangemwambia kuhusu Belleck ambaye hakujua alikuwa katika hoteli gani.
“Belleck yupo anakula raha, hivi tunavyoongea, keshokutwa anaondoka kurudi Marekani,” alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kwa jina la De Leux.
“Sawa. Kingine?”
“Huwa anapenda sana kununua malaya mitaani! Tunajua sehemu ambayo hupenda kununua na pia tunajua hoteli anayokaa mpaka chumba alichokuwepo,” alisema De Leux.
“Haina shida! Ningependa nikutane naye na kufanya kazi yangu,” alisema Fareed.
Hakwenda huko kufanya jambo lolote zaidi ya kumuua bilionea huyo na kuondoka zake. Wanaume hao wawili ndiyo walikuwa wachora ramani wakubwa, walikuwa wakienda hotelini hapo, wanaonana na wahudumu wa hapo, wakatengeneza urafiki wa kizushi kwa ajili ya kuwasaidia hapo baadaye.
Hawakujua kama lengo la watu hao ni kumpata mwanaume aliyekuwa ndani ya hoteli hiyo. Wakati mwingine walikuwa wakikaa mapokezini, Belleck alipokuwa akiingia ndani ya hoteli ile na machangudoa walikuwa wakimuona hivyo kuwa kazi nyepesi kwao kufanya kile walichokuwa wakikitaka.
“Cha kwanza ni kupata kadi ya kufungua vyumba vyote,” alisema De Leux.
Hilo ndilo lililotakiwa, kwa kutumia uzoefu mkubwa wa kuzungumza waliokuwa nao, wakajenga ukaribu zaidi na mhudumu aliyeitwa kwa jina la Natalie ambaye bila tatizo lolote lile, naye akaukaribisha ukaribu huo na mwisho wa siku De Leux kumtongoza.
“Acha masihara wewe! Mzuri mimi?” aliuliza Natalie huku akitabasamu, japokuwa alipinga kwamba hakuwa mzuri lakini sifa zile zilimfurahisha.
“Wewe ni mzuri sana. Una tabasamu pana, msichana mrembo sana! Umeumbinka kama Mona Liza,” alisema De Leux huku akimwangalia Natalie kwa macho ya nipe nikupe.
Akamsifia usiku mzima, msichana huyo akachanganyikiwa, kila wakati akawa anapandisha juu mpaka katika chumba alichokuwa akilala De Leux na kuingia ndani. Hakutaka kufanya mapenzi na msichana huyo, kitu muhimu kilikuwa ni kuweka ukaribu na mwisho wa siku kuichukua kadi ambayo alikuwa akiitaka mno.
Wakati walipokwenda kuonana na Fareed, walimwambia kabisa kile kilichokuwa kimetokea kwamba kulikuwa na kadi moja muhimu ambayo ingewawezesha wao kuingia ndani ya chumba chochote kile.
Fareed akafurahi kwani urahisi huo ndiyo aliokuwa akiutaka kwa hali na mali. Siku hiyo wakaondoka na kwenda katika hoteli hiyo. Wakachukua chumba kwa ajili ya Fareed ambaye akaingia bila tatizo na uzembe mkubwa ambao waliufanya wahudumu wa hoteli hiyo ni kutokuishikilia passport yake.
Akaingia mpaka chumbani, akajipumzisha na kuambiwa kwamba mtu aliyetakiwa kumuua alikuwa njiani kufika mahali hapo hivyo alitakiwa kusubiri.
De Leux na mwenzake wakarudi mapokezi, wakatulia kochini. Ilipofika saa sita usiku, wakamuona Belleck akirudi hotelini hapo huku akiwa na mwanamke ambaye alivalia hijabu ila kwa nyuma alijazia hasa kiasi kwamba hata wao walipokuwa wakimwangalia walimtamani kupita kawaida.
“Huyo hapo! Subiri!” alisema De Leux.
Wakati mwanaume huyo akiingia ndani na mwanamke huyo, De Leux akamuita Natalie na kuanza kuongea naye. Alimwambia wazi kwamba siku hiyo alitaka kukaa naye na kuzungumza naye mambo mengi lakini iwe baada ya kufanya usafi katika vyumba mbalimbali.
“Haina shida mpenzi! Nitakuja,” alisema Natalie huku akionekana kuwa na furaha tele.
De Leux akaondoka na mwenzake mpaka chumbani kwake, wakakaa huko na kuyapanga kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa mtu huyo ambaye alikuwa adui wa bosi wao kwa kipindi kirefu.
Wakamfuata Fareed na kumwambia kilichokuwa kikiendelea kwamba ni yeye tu ndiye aliyekuwa akisubiriwa kufanya mauaji hayo.
“Haina tatizo!”
“Sawa. Ngoja nimuite huyu msichana alete kadi,” alisema De Leux na hapohapo kuchukua simu ya mezani na kupiga mapokezi ambapo alimtaka Natalie aende huko kuchukua shuka kwenda kulifua.
ITAENDELEA KESHO

No comments

Powered by Blogger.