ad

ad

Rais Magufuli Apigilia Msumari Umiliki Wa Kampuni Ya Airtel



Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango kufuatilia umiliki wa kampuni ya mawasiliano ya simu ya Airtel akisema kwa taarifa alizonazo hiyo ni mali ya Serikali.


Ametaka ufuatiliaji huo ufanywe haraka iwezekanavyo na mpaka kufikia Januari, ripoti iwe imekamilika.

Dk Magufuli amesema hayo siku ambayo Mwananchi liliripoti kuhusu mpango wa Serikali kutaka kumiliki hisa zote za kampuni hiyo kutokana na uwekezaji mkubwa ilioufanya wakati wa kuanzishwa kwake, takriban miongo miwili iliyopita.

Wakati wasomaji wa Mwananchi wakiendelea kupata undani wa suala hilo, jana asubuhi wakati akiweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma, Rais alisema kwa taarifa alizonazo, Airtel ni mali ya Serikali chini ya umiliki wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

“Palifanyika mchezo wa ovyo, sasa sitaki kuzungumza mengi, fuatilia hilo. Nchi hii ilikuwa ya maajabu sana, unachukua share (hisa) leo, kesho inauzwa kwa Dola moja, maajabu,” alisema.
Rais Magufuli alimtaka Dk Mpango kuhakikisha mchezo huo unamalizika na kwamba kwa namna hiyo lazima vyuma vitabana tu.
“Tumeamua kubana vyuma vilivyolegea, vilivyokuwa vya ajabu ambavyo vilikuwa vikihatarisha maisha ya Watanzania hasa maskini,” alisema.
Uhamishaji hisa

Utata unaoelezwa na Rais Magufuli kwenye kampuni hii ambayo inahudumia zaidi ya wateja milioni 10.57 kwa mujibu wa takwimu za Septemba za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivyo kuifanya kuwa ya tatu yenye wateja wengi zaidi nchini, ulianza Novemba 3, 1998.
Mwaka huo, TTCL ilianzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote. Mtaji wa Dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Sh11 bilioni sasa) uliwekezwa.
Lakini, Januari 31, 2002 Celtel ikiendelea kuwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa Dola 82 milioni (zaidi ya Sh180.4 bilioni) ili kukuza mtaji wake.

Wakati mkopo huo unachukuliwa, TTCL ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International Cellular Investments Tanzania (MSIT) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.
Miaka mitatu baadaye, Agosti 5, 2005 mabadiliko yalifanywa kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel na kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikitenganishwa na TTCL.

Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Zain ambayo nayo, baada ya miaka mitatu, iliziuza kwa Bharti Airtel, Juni 8, 2010.

Madai yanayoibuka hivi sasa yanatokana na Serikali kutoridhishwa na namna umiliki ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL huku yenyewe ikipewa hisa chache tofauti na ilivyostahili.

Kwa agizo la Rais, mpaka Januari mwakani, Waziri Mpango anatakiwa kujiridhisha na kukamilisha taratibu za kudai umiliki huo utakaoiweka Airtel chini ya TTCL na kuifanya Serikali iimiliki Airtel kwa asilimia 100.

Kwa sasa, Serikali inamiliki asilimia 40 ya hisa za Airtel huku zinazobaki zikiwa za Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010.

Msimamo wa Rais Magufuli kutaka TTCl imiliki hisa zote za Airtel unatokana na madai ya udanganyifu na upindishaji wa taratibu uliofanywa mwaka 2005.
Nyaraka zilizoifikia Mwananchi, ambazo leo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL, Omar Nundu atazitolea ufafanuzi, zinaonyesha mkutano uliofanywa kwa saa mbili mfululizo, Agosti 2005, ndio uliobadili kila kitu kuhusu umiliki wa Celtel.

Kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe sita wa bodi ya TTCL, mwanasheria na mkurugenzi mtendaji, uliidhinisha uwekezaji wa Dola 82 milioni kwenye kampuni ya awali, Celtel.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa kati ya fedha hizo, TTCL ilitoa Dola 40 milioni (zaidi ya Sh88 bilioni) kama mtaji hivyo kumiliki asilimia 65 ya hisa za Celtel na Dola 42 milioni (zaidi ya Sh92.4 bilioni) zikiwa ni mkopo ambao ungerejeshwa ndani ya miezi sita kwa riba ya asilimia 4.75 kwa mwaka.

Licha ya kubadili sehemu ya mkopo huo kuwa mtaji, mkutano huo uliofanyika kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa sita mchana, ulihamisha hisa zote kutoka TTCL kwenda Airtel hivyo kuhitimisha uhusiano uliokuwapo kati ya kampuni hizo mbili. TTCL ilipokuwa inaimiliki Celtel.
Kufanikisha uendeshaji wa kampuni hiyo mpya (Celtel Tanzania) kwa umiliki, wajumbe wa mkutano huo, kwa pamoja, waliidhinisha asilimia 65 ya hisa za TTCL zipelekwe kwa Msajili wa Hazina ambaye ndiye aliyekuwa mwakilishi wa Serikali kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel.

Kuvunjwa kwa Celtel iliyokuwa chini ya TTCL kwenye mkutano huo kulifanya pawepo na mkutano mwingine wa dharura wa Celtel mpya ili kufanikisha uhamishaji wa hisa kati ya pande husika, wajumbe hao walitekeleza jukumu hilo. Mwisho wa mkutano huo, wajumbe walijiuzulu na wakapendekeza majina ya wajumbe wa bodi mpya.
Ndani ya majadiliano katika mkutano huo, haijulikani ni kwa nini wajumbe hao waliridhia kuhamisha asilimia 35 ya hisa za Celtel kwenda MSIT.

Kwa hali ilivyo, mtaji wa TTCL ulitolewa kuiendesha Celtel lakini, uongozi wa sasa unasema haujapata faida ya uwekezaji huo. Chanzo chetu cha kuaminika kinasema si mkopo uliotolewa wala riba yake vilivyolipwa mpaka leo tofauti na makubaliano yaliyofanywa miaka 12 iliyopita.
“TTCL ililazimika kukopa kutoka serikalini kufanikisha uwekezaji huo kama mkataba ulivyokuwa unaelekeza lakini mpaka leo hakuna ajuaye ilikuwaje Msajili wa Hazina alipokwa asilimia 65 alizokuwa anamiliki,” kilisema chanzo hichokutoka Wizara ya Mawasiliano.

Taarifa za kuaminika zinabainisha kwamba, kwenye kikao hicho, wajumbe waliandaa waraka wa uendeshaji wa kampuni (articles of association) ambao haukuipa nafasi TTCL kufanya uamuzi wowote wala kuuliza chochote kuhusu uwekezaji wake Celtel.

CHANZO; MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.