ad

ad

Simba SC Wamwandikia Barua Waziri Kudai Penalti


KLABU ya Simba imemuandikia barua Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kwa madai kuwa wamekuwa wakinyimwa penalti kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. 


Msemaji wa Simba, Haji Manara, amesema kuwa wamenyimwa penalti za wazi katika michezo mitatu jambo ambalo wanaona siyo sawa kwani waamuzi wamekuwa hawawatendei haki.
Aidha, barua hizo pia zimepelekwa katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi na Kamati ya Waamuzi ili kuwasilisha malalamiko yao. 


Mechi ambazo Simba walizilalamikia ni dhidi ya Mbao FC ya Mwanza katika mchezo uliopigwa CCM Kirumba, Stand United katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na ule dhidi ya Yanga uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar. 


“Waamuzi wamekuwa wakiidhulumu Simba kwa makusudi, hivyo tumemua kuchukua hatua kwa kupeleka malalamiko yetu kwa vyombo husika ambavyo ni wizara ya michezo, TFF, Bodi ya Ligi na kamati ya waamuzi. 


“Mechi ambazo tumefanyiwa ndivyo sivyo ni dhidi ya Mbao FC tulipocheza Mwanza, Bocco (John) aliangushwa mara mbili lakini mwamuzi alipotezea, Stand United ilipewa penalti ambayo siyo halali. 


“Pia katika mchezo wa watani wa jadi, Yondani alionekana kushika mpira kwenye eneo la hatari na katika tukio lingine Papy Tshishimbi alionekana kuukumbatia mpira ndani ya boksi lakini hatukupewa penalti, mwamuzi aliwabeba Yanga na tutatumia video hizo kuweza kuwasilisha malalamiko yetu,” alisema Manara.

No comments

Powered by Blogger.