Wazee wamkaanga Lulu mahakamani, atoka nduki
MAHAKAMA Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ mnamo Novemba 13, mwaka huu baada ya Wazee wa Baraza kutoa maoni yao katika kesi hiyo.
Kesi inayosikilizwa na Jaji Sam Rumanyika ambapo jana Alhamisi alitoa nafasi ya wazee watatu wa Baraza la Mahakama hiyo kutoa ushauri wao mbele ya mahakama ambapo wote walisema kuwa msanii huyo ameua bila kukusudia.
Jaji Rumanyika alisema kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka umejikita zaidi kwenye mazingira kwa kuwa Lulu ndiye mtu wa mwisho kuwa na marehemu Kanumba.
Akitoa maoni yake, mzee wa kwanza wa baraza hilo, alisema kuwa Lulu ameua bila kukusudia kutokana na ushahidi wa mdogo wake Kanumba (Seth) ambaye alielezea ugomvi uliotokea kati ya watu hao wawili.
“Maoni yangu naona marehemu alikufa kutokana na kuteleza maana ilikuwa ni usiku na kulikuwa na giza ingawa sababu ya kutekeleza kwake ni ugomvi wake na Lulu,” alisema.
Kwa upande wa mzee wa pili alisema kuwa Kanumba alikufa kutokana na ugomvi na ushahidi umewaeleza kulikuwa na giza hivyo anaamini msanii huyo hakuua kwa makusudi bali ilikuwa bila kukusudia.
Hata hivyo, mzee wa tatu, Rajabu Mlawa, yeye alisema kuwa hakuna ubishi kuwa msanii huyo ana kosa la kuua bila kukusudia kutokana na Kanumba kuwa na mwili mkubwa huku akiwa amelewa hali iliyosababisha Lulu kutumia nguvu kujiokoa kwa kumsukuma Kanumba na kudondoka chini.
Kufuatia wazee hao kutoa maoni yao, Jaji Rumanyika alisema kuwa anatarajia kutoa hukumu ya kesi hiyo Novemba 13, mwaka huu mbele ya mahakama hiyo lakini kwa upande wa msanii huyo alitoka akiwa anatembea kwa kasi kubwa akiwa amejifunga ‘ninja’ usoni pamoja na kujifunika khanga kwa lengo la kukwepa kamera za waandishi huku akikingwa na watu wanne.
Post a Comment