ad

ad

SHOGA; Ukila na Kipofu Usimshike Mkono!


HEYA heya acha nicheke miye sidaiwi na mtu navuta hewa ya bure ya nini kujibana najiachia nitakavyo. Kama pumzi ingekuwa inauzwa mbona wengi tungepumua kwa mahesabu!
Ushaanza kusema nina maneno mengi kama nilibemendwa, aiiih weee! Jamani mbona hivyo kwani kucheka ni kwa wenye meno pekee, wenye mapengo na magego tusicheke, tuvumiliane basi mate yakiwarukia muone kama dawa ya mbu ya kupuliza! 


Leo nipo na nyie wadokozi wa waume za watu lazima mbadilike na muelewe kuwa ulacho si chenu hata kama utammiliki kwa asilimia mia. Siku zote matawi hayashindani na shina. Nasema haya nina maana gani? 


Siku hizi nyumba ndogo imekuwa si suna tena, hapo mwanzo ilikuwa mtu akiwa na nyumba ndogo ilikuwa siri, lakini siku hizi watu aibu imewatoka usoni na kujihalalishia na kuonekana nyumba ndogo imegeuka nyumba kubwa kwa kila kitu kuhamishiwa nyumba ndogo na nyumba kubwa kusahaulika.


Kwa vile wanadamu wengi tumekuwa hamnazo na akili tunazo, basi unajiona kuwa wewe unapeeeeeendwa kuliko mkewe. Weweeee unajidanganya ungekuwa unapendwa ungeolewa wewe. Japo najua nasi nyumba ndogo kwa kufusha mavumba hatujambo. 


Basi ndiyo unamteka mume wa mwenzio na kujisahau kama ana watoto na mke wanahitaji matunzo. Eeeh! Jamani kwa nini lakini tunafanya matangazo ya dawa za kulevya kwenye runinga hatuogopi? Wao wamelala au umemweka kwenye kiganja haoni hasikii kwa ulozi wako.
Hivi kama wewe mwizi umeweza kwenda kwa huyo mganga mwenye mali atashindwa vipi? Mbona tunajidanganya. Kumbuka unayemfanyia hivyo ni mwanamke mwenzako kibaya zaidi mume wake wa ndoa. Naye akishikwa masikio kuna kupona mtu, haki ya nani yeye akifika anafunika tu akifunua jina lako linabakia historia, upo?


Sasa leo nataka tuongee kidugu na ninyi mnaoitwa nyumba ndogo, ukipata bwana ambaye amekufa kwako haina haja ya kwenda kwa karumanzila muoneshe mapenzi ambayo kwa mkewe hayapati jitume bila kuchoka ili aone tofauti ya ndani na nje.


Siyo nyumba ndogo basi ina matatizo kuliko hiyo nyumba kubwa mwanaume abaki kwako amerogwa. Na wewe ambaye unayatenda yaliyomgandisha kwako kwa kutumia udhaifu wa nyumba kubwa. Basi kula kama unakula na kipofu, usimbane sana mume wa mtu mpaka mabadiliko ndani yaonekane. Jitahidi kuheshimu ndoa ya mtu kwa kula kama panya unakula huku unapuliza la sivyo waokota makopo wataongezeka si wajinga waliosema cha mtu sumu.


Siku zote ukila na kipofu shoga usimshike mkono, mshahara kama mia basi chukua 25 zingine muachie apeleke kwake. Siyo 75 wewe 25 nyumbani kwake lazima mkewe atatafuta sababu za mshahara kupotea pia muda wa kurudi nyumbani kubadilika. 


Wewe unajua kabisa upo na mume wa mtu unamng’ang’ania ili iweje? Unataka arudi saa sita za usiku wakati siku za nyuma alikuwa akirudi saa mbili usiku. Hivi ungekuwa wewe ungekubali mabadiliko hayo? Usifikiri utaendelea kuwa nyumba ndogo maisha yako yote, ipo siku utakuwa nyumba kubwa utakubali?


Siku zote unapopata raha ukumbuke na shida, acheni kuchokonoa watu waliotulia, cha mtu siku zote sumu.Kula chako kidogo kikubwa muachie mwenye mali siku zote utaishi kwa raha hata mwenye mali ataona kweli kampata mtu mwenye hekima atakayemsaidia siyo atakayemfilisi.
Yangu nimemaliza tukutane wiki ijayo ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

No comments

Powered by Blogger.