Singano Anakwenda Yanga, Apotezewa na Difaa Al Jadida Akiwa Morocco
KIUNGO mshambuliaji Ramadhan Singano ambaye alikuwa akiichezea Azam FC, Alhamis mchana alirejea nchini akitokea Morocco alikokwenda kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya Difaa Al Jadida. Akiwa Morocco kwenye mipango yake hiyo inaelezwa kuwa wakala wake amechangia kukwama kwa dili la kujiunga katika kikosi hicho na ndiyo maana amerejea Dar ambapo moja kwa moja amekutana na ofa ya kusajiliwa na Yanga.
Singano aliondoka hapa nchini Julai 14, mwaka huu, alikwenda Morocco kwa makubaliano ya kusaini mkataba wa miaka mitatu katika timu hiyo, lakini alishangaa kufika huko na kutakiwa kufanya majaribio ambapo alicheza mechi sita.
Mtu wa karibu wa mchezaji huyo, alisema: “Singano amerejea baada ya wakala wake anayeitwa Khalid kuwa na tamaa ya fedha kutokana na kupandisha dau na kwenda kinyume na makubaliano kitendo ambacho ile timu imekasirika. “Sisi kama watu wake wa karibu, tumemwambia arudi awahi dirisha la usajili hapa nyumbani kabla halijafungwa na kama ikitokea anahitajika tena ataondoka,” alisema mtu huyo.
Aidha kaka yake Hamis Singano aliliambia gazeti hili kuwa, Singano alikuwa tayari amesaini mkataba wa awali na klabu hiyo, kilichobaki ni kwenda kumalizika kupimwa afya na masuala mengine ili awe mchezaji wao. Katika mkataba huo, inaonyesha kwamba kila mwezi Singano angekuwa akilipwa dola 2,000 (zaidi ya Sh 4.4m) kama sehemu ya mshahara kwa muda wa miaka mitatu, huku fedha ya usajili kwa kila mwaka ikiwa ni dola
56,000 (zaidi ya Sh 124m).
Kama dili hilo lingefanikiwa, basi Singano angecheza timu moja na kiungo wa zamani wa Yanga, Simon Msuva ambaye hivi karibuni alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.
Yanga yamfuata Taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni kuwa Yanga imeshamfuata mchezaji huyo kwa ajili ya kumsajili kwa kuwa mkataba wake na Azam FC ulimalizika mwezi uliopita.
Alipotafutwa Singano mwenyewe kuhusu suala hilo, alisema: “Kweli nipeshapata ofa kadhaa ikiwemo Yanga, kuhusu nitasaini au la nitakujulisha, nipe muda kwa kuwa ndiyo kwanza nimefika.” Kigogo mmoja wa Yanga, alisema: “Ndiyo tuna mpango huo wa kumsajili na ninadhani tutakamilisha dili hilo kabla ya kufungwa kwa usajili maana tumesikia Azam na Singida United nao wanamuwania.”
CHANZO: CHAMPIONI IJUMAA
Post a Comment