ad

ad

SIMBA HII SIO YA MCHEZOMCHEZO, YATUMA SALAMU KWA TIMU ZA LIGI KUU



JANA Jumanne, Klabu ya Simba SC ilitimiza miaka 81 tangu kuanzishwa kwake ikipitia majina mengi ikiwemo Sunderland, klabu hii yenye makazi yake Kariakoo, katika kuazimisha miaka hiyo walicheza mchezo na Rayon Sport ya Rwanda.
Timu hiyo inashikilia rekodi mbalimbali hapa nchini lakini Championi Jumatano, linakuletea baadhi ya rekodi ambazo zimewekwa na kikosi hicho kilichoshinda ubingwa wa FA msimu uliopita. 


WA KWANZA KUKWEA PIPA
Mwaka 1963, Simba ilipata mwaliko kutoka kwa Rais wa Ethiopia, Haile Selassie kipindi hicho hata Tanzania haikuwa imezaliwa, lakini nyota wa kikosi hicho walipanda ndege na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza Tanganyika kufanya tukio hilo ambalo leo hii wanajivunia mbele ya watani zao wa jadi Yanga.
UZI WA WACHEZAJI ULIANZA KWAO
Mwaka 1938, Simba iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuvaa jezi na hii ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Kombaini ya Mabaharia wa Meli zilizotia nanga kwenye Bandari ya Dar es salaam.
SOMA NA HII YA VIATU
Miaka 13 tangu kuanzishwa kwa Simba, mwaka 1949 timu hii ikaweka rekodi nyingine ya kuwa klabu ya kwanza kuvaa viatu vya kuchezea mpira. Hii ilikuwa walipokutana na Kombaini ya Jeshi la Majini (Navy) la Afrika Kusini.
WALIANZA KUMILIKI USAFIRI WAO KITAMBO
Ilipofika mwaka 1968, Simba ilitengeneza rekodi nyingine ya kuwa klabu ya kwanza kumiliki basi lao wenyewe hii ni moja ya rekodi ambayo mashabiki wa Simba wanajivunia mbele ya wapizani wao.
WALIMILIKI JENGO KABLA YA YANGA
Mwaka 1971, Simba walizindua jengo lao wenyewe na kuwafanya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kumiliki jengo lao wenyewe ambapo leo wanajivunia nalo.
UBINGWA WA LIGI WALIANZA KUBEBA WAO
Mwaka 1966, Simba ilitengeneza rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kuchukuwa kombe la ligi kuu baada ya kuanzishwa kwake.
TIMU YA KWANZA KUIPEPERUSHA NCHI KIMATAIFA
Mwaka 1967, timu ya Simba SC iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuipeperusha bendera ya taifa kwenye michuano ya kimataifa.
WA KWANZA KUTUA NJE YA NCHI
Simba ndiyo klabu ya kwanza kwenda katika nchi za Ulaya na walifanya hivyo mwaka 1974, walipokwenda Poland.
WA KWANZA KUTWAA UBINGWA WA KAGAME
Mwaka 1974, Simba ilibeba ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (maarufu kama Kagame, jina la rais wa Rwanda, Paul Kagame) baada ya kuanzishwa kwake na kuwafanya kuwa timu ya kwanza kuchukua kombe hilo.
MABINGWA WA KIHISTORIA WA KOMBE LA KAGAME
Simba ndiyo timu pekee iliyochukua ubingwa mara nyingi kuliko klabu yoyote Afrika Mashariki na Kati (Champs off all time).
TIMU PEKEE TANZANIA KUFIKA NUSU FAINALI YA KLABU BINGWA AFRIKA
Mwaka 1974, Simba iliweka rekodi ya kuwa klabu pekee ya Tanzania kufika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa wa Afrika ambapo mpaka leo rekodi yao haijafanikiwa kufikiwa na klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara.
TIMU PEKEE AFRIKA MASHARIKI KUFIKA FAINALI YA KOMBE LA CAF
Mwaka 1993 klabu ya Simba ilitengeneza rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kuwahi kufika fainali ya michuano ya Caf dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.


TIMU PEKEE TANZANIA KUIVUA UBINGWA ZAMALEK
Mwaka 2003, Simba ilifanikiwa kuivua ubingwa wa Mabingwa Afrika, timu ya Zamalek na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo kutoka Tanzania. Kabla ya hapo hakukuwa na timu iliyoweza kuwavua ubingwa timu kutoka Afrika Kaskazini.
Pia timu hiyo ilizifunga timu za mataifa ya kiarabu ambazo ni Al Ahly, Arab Contractors, Ismailia, Mehala, Al Kubra na nyingine mbalimbali.
Hii ndiyo rekodi ambayo leo hii klabu ya Simba imeendelea kushikilia mbele ya wapinzani wao kwa miaka 81 tangu kuanzishwa kwake.






CHANZO: CHAMPIONI

No comments

Powered by Blogger.