SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-15
NYEMO CHILONGANI
Hakujua sababu iliyowafanya watu wote mahali hapo kuanza kucheka na wakati alijiona ameomba kitu cha msingi mno. Akabaki akiwa ameduwaa tu asijue la kufanya. Lusifa aliendelea kumwangalia huku akiendelea kucheka, kicheko kilichowafanya hata wale wengine kucheka zaidi.
“Mbona mnacheka?” aliuliza mzee Hamisi huku akionekana kushangaa.
“Hakuna anayeweza kuomba kitu kama hicho! Hicho ni kitu ambacho kinakuja moja kwa moja, umefikiria nini mpaka kuomba kitu kama hicho?” aliuliza kiumbe mmoja, alikuwa akimshangaa mzee Hamisi.
“Ninataka niwe na nguvu.”
“Kwa hiyo unataka uwe na nguvu au unataka kuwa na majini?”
“Nataka kuwa na vyotevyote,” alisema mzee Hamisi.
“Hahaha! Hakuna mtu mwenye majini duniani.”
“Unasemaje?”
“Hakuna mtu mwenye majini duniani, majini yote makazi yao ni kuzimu, duniani hakuna majini yanayofugwa na mtu,” alisema kiumbe yule, kidogo vicheko vikaanza kupungtua.
“Na wale wanaosema wana majini?”
“Hakuna mwenye majini, binadamu hawezi kufuga majini, hakuna mwanadamu mwenye nguvu kama majini,” alisema kiumbe yule.
“Nifafanulie juu ya hili.”
“Hakuna ufafanuzi, jua kwamba hakuna mwanadamu mwenye majini.”
“Na yale niliyokuwa nayo nyumbani.”
“Huna majini.”
“Wale ni wakina nani?”
“Nguvu zako!”
“Nguvu zangu?”
“Ndiyo!”
“Sijaelewa.”
“Utakwenda kuelewa tu, njoo hapa mbele tukupe nguvu ambazo unaamini ni majini,” alisema kiumbe yule.
Mzee Hamisi akaanza kupiga hatua kwenda pale mbele, ghafla akajikuta akianza kupata nguvu za ajabu ambazo hakuwahi kuzipata kabla. Hakujua kitu gani kilikuwa kinaendelea, mpaka alipofika pale mbele na kuambiwa kupiga magoti, akajisi kuwa mtu mpya kabisa.
Kiumbe yule akachukua kikombe kilichojaa damu, alimwambia kwamba hiyo ilikuwa damu yenye mchanganyiko wa watu tofauti, alimaanisha Wazungu, watu weusi, Wachina na wale wenye ulemavu wa ngozi, akampa kikombe kile na kumtaka kunywa.
Alipomaliza kunywa damu ile, akahisi akiongezeka nguvu fulani mwilini mwake, watu wote waliokuwa mahali pale wakapiga makofi ya shangwe kwani walijua kwamba kwa siku hiyo tayari aliongezeka mtu mwingine.
Kuanzia siku hiyo, mzee Hamisi akawa moto wa kuotea mbali, hakumuogopa kabisa Ramadhani kwa kuona kwamba tayari alikuwa na nguvu nyingi hivyo angeweza kumsambaratisha kwa dakika moja tu.
Aliporudi nyumbani, alikuta kukiwa kumetundikwa turubai na alipouliza kitu gani kilikuwa kikiendelea, aliambiwa kwamba binti yake alifariki dunia ghafla na alipoplekwa hospitalini majibu yalionyesha kwamba alikufa kwa shinikizo la damu.
Moyoni aliumia lakini hakuwa na jinsi kwani alijua kila kitu kilichokuwa kimetokea. Alihuzunika na majirani zake na maiti haikulala siku nyingi kwani kesho yake mazishi yakafanyika na kwenda kumzika.
Hawakukaa sana baada ya mazishi, taarifa zikaletwa na kusema kwamba mama yake alikuwa amefariki dunia. Mzee Hamisi aliumia zaidi lakini hakuwa na jinsi kwani yeye ndiye alihusika kwa kila kitu hivyo alijua kile kilichokuwa kikienda kutokea.
Familia nzima ililia, kilikuwa kipindi kigumu kuliko vyote ambavyo viliwahi kutokea katika familia hiyo, kuwapoteza watu wawili kwa mpigo kuliwaumiza mno. Hawakuwa na jinsi kwani kwa mawazo yao walijua kwamba Mungu ndiye aliamua hayo yote yatokee.
“Haya yote amesababisha Ramadhani,” alisema pasipo kujua kwamba pembeni alikuwa amekaa mtu.
“Unasemaje?”
“Hapana! Hakuna kitu.”
Hasira zake zikawa kwa Ramadhani tu kwani bila yeye asingekwenda kule kuzimu na kusababisha mama yake na mtoto wake kufariki dunia. Moyoni alikuwa na hasira mno, hakutaka kuona kile kilichotokea kinakwenda hivihivi tu, alichokuwa akikitaka ni kumuua Ramdahani kama kisasi.
“Huyu atakuwa Ramadhani tu,” alimwambia mke wake.
“Kwa nini?”
“Yeye si ndiyo mwenye ugomvi na mimi!”
“Mume wangu! Usifikirie hivyo!”
“Hivi kweli kupoteza watu wawili kwa siku mbili tu, hapana, kuna kitu,” alisema mzee Hamisi.
“Usifikirie hivyo mume wangu!”
“Hapana! Hapa kuna kitu. Haiwezekani, leo namfuata na kumuondoa duniani, siwezi kukubali,” alisema mzee Hamisi huku akionekana kuumia mno. Akapanga usiku huo ndiyo aanze kupambana na Ramdahani, hivyo akajipanga.
*****
Usiku wa siku hiyo ndiyo ulikuwa usiku wa kazi, mzee Hamisi alimchukia mno Ramadhani, na hakupenda hata kidogo. Aliamini kwamba mtu huyo ndiye aliyesababisha vyote vilivyotokea katika maisha yake vikiwemo vifo vya watu aliowapenda mno maishani mwake.
Usiku wa siku hiyo alitulia chumbani kwake, hakutaka kuwasha taa yenye mwanga mkali, ilikuwa ni taa iliyokuwa na mwanga hafifu sana wa rangi nyekundu, alijifunika shuka jeusi tii huku ndani yake akiwa na karatasi iliyokuwa na maneno ambayo aliweza kuyatamka yeye tu kwa kuyasoma.
Chumba kizima kilinukia udi tu, sauti yake ilikuwa ikisikika kwa chini sana. Ulikuwa ni usiku wa manane ambapo alitaka kufanya kazi yake ili kummaliza Ramadhani aliyeonekana kuwa nuksi kwa kile akitu alichokuwa akikifanya.
Kelele zikaanza kusikika ndani ya chumba hicho, hakutaka kunyamaza aliendelea kuyazungumza maneno yale mpaka akajiona akianza kupaa juu chumbani mule na kuelea angani kitu ambacho hakikuwahi kutokea kabla.
Harufu ya udi ule ikaongezeka zaidi, akaongeza kasi ya kuzungumza maneno yale, mara zile tunguli zilizokuwa ndani ya chumba kile zikaanza kuvunjikavunjika kuonyesha kwamba yale aliyokuwa akiyafanya chumbani mule yalikuwa na nguvu zaidi.
Ghafla, akajikuta akipotea, alipokuja kuibuka, akajikuta ndani ya chumba cha Ramadhani, wakabaki wakiangaliana tu kwani naye Ramadhani alijua kwamba mtu huyo angefika nyumbani hapo usiku huo.
Hakukuwa na mtu aliyeongea kitu chochote kile, kilichofuata ni kuanza kupimana nguvu za kichawi. Walibaki wakiangalia huku kila mmoja akianza kuzungumza maneno yake yenye nguvu tena kwa haraka mno kwani ndiyo yalikuwa maneno yenye nguvu ambayo mara nyingi huyatumia.
Ghafla, taa iliyokuwa ikiwaka, ikapasuka, vyombo vilivyokuwa kabatini vikaanza kuanguka kutokana na tetemeka la ardhi lililotokea ndani ya chumba hicho tu. Hawakuacha kuzungumza maneno hayo ya ajabu, ghafla, Ramadhani akaanza kuzidiwa, akaanza kuzunguka huku na kule chumbani mule.
Mzee Hamisi hakutaka kunyamaza, tayari aliona kwamba huo ulikuwa nusu ya ushindi wake na alitaka kupambana mpaka pale atakapouona ushindi wenyewe.
Alizidi kuyatamka maneno yale, alipoona kwamba hayatoshi tu, akaanza kuchukua karatasi zenye maneno yale, akachukua na unga fulani kisha kuuweka katika karatasi ile na kuanza kumpulizia Ramadhani kitu kilichomchanganya vilivyo, hapohapo akaanguka chini na mapovu kuanza kumtoka mdomoni na puani.
Huo ulikuwa ushindi mkubwa ambao hakutarajia kuupata kabla, mtu ambaye alimsumbua kwa kipindi klirefu, leo hii, tena usiku huu alikuwa hoi pale chini. Kwake, hiyo iliendelea kuwa furaha, kubwa, alichokifanya ni kupotea, na ghafla akaibukia katika uwanja wa wachawi wenzake, wote waliomuona, wakaanza kutetemeka akiwemo mkubwa wao.
Nguvu alizokuja nazo mzee Hamisi zilikuwa kubwa mno, uwanjani hapo walikuwa na kiongozi wao lakini alipomuona mzee Hamisi akiingia, naye akajikuta akitetemeka, hofu ikamjaa na mwisho wa siku, wote kwa pamoja akiwemo yeye kiongozi wakapiga magoti chini kama ishara ya kumpa heshima.
Huo nao ukawa ushindi mkubwa, kule kuzimu alipokuwa amekwenda, alipewa nguvu za ajabu ambazo hakuamini kama angeweza kuzipata katika maisha yake.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, mzee Hamisi alikuwa kiongozi wa wachawi lakini huyohuyo ndiye alikuwa hakosi msikitini. Alikuwa mtu wa swala tano, aliheshimika mno pasipo watu kujua kwamba mtu huyo alikuwa mkubwa wa wachawi na alikuwa na nguvu mno za kichawi.
Hiyo ndiyo stori ya mzee Hamisi niliyotaka kukupa, alikuwa miongoni mwa watu niliokutana nao kule kuzimu. Walikuwa watu wengi sana, wote hao walikuwa wakimuabudu shetani ambaye alikuwa mbele yao.
Ukiachana na mzee Hamisi, yule mchungaji na mwanasiasa ambao wote niliwapeni sifa zao, kulikuwa na msichana mmoja hivi, msichana mrembo kwa kumwangalia, aliyekuwa na figa matata sana, naye huo alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa humo.
Kwa kumwangalia, mwanaume yeyote aliye rijali asingeweza kumuacha, alivutia, alikuwa na umbo namba nane, sura nyembamba na kifuani alionekana kama msichana aliyetoka kuvunja ungo siku si nyingi.
Sikuwa nikimfahamu, sikuwahi kumuona kabla lakini Yusnath aliniambia kwamba msichana huyo aliitwa Esta.
Naweza kusema kwamba nchi ya Tanzania ilikuwa ikifanya mashindano ya walimbwende kila mwaka, niliwahi kuwaona wengi wakiwemo Wema Sepetu, Irena Uwoya na wengine wengi lakini kwa uzuri aliokuwa nao Esta ilikuwa ni balaa.
“Huyu msichana ni nani?” nilimuuliza Yusnath.
“Anaitwa Esta.”
“Anakaa wapi?”
“Anaishi Ilala.”
“Naye anaabudu hapa?”
“Ndiyo!”
“Yupo kitengo gani?”
“Huyu ni kwa ajili ya kuua tu na kuwalaghai watu. Huyu ni msichana mbaya sana ambaye ombea kukutana na simba lakini si msichana huyu,” alisema Yusnath.
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo!”
“Ooppss!”
“Nikwambie kingine?”
“Kipi?”
“Huyu msichana si binadamu!”
“Unasemaje?”
“Ni jini!”
“Hebu niambie vizuri kwanza,” nilimwambia Yusnath.
“Usijali, kuna mengi nitakwambia kuhusu Esta na namna anavyofanya kazi zake,” aliniambia Yusnath.
“Sawa. Ningependa kusikia mengi.”
“Usihofu! Ushawahi kusikia kuhusu jini Maimuna?”
“Ndiyo! Nasikia ni msichana mzuri mno!”
“Basi ndiye huyu!”
“Ndiye yule tuliyekutana naye kule mwanzo?”
“Unaposikia jini Maimuna, hayupo mmoja, wapo wengi, tena wote warembo!”
“Duuh! Hebu niambie kuhusu Maimuna, ningependa kusikia mengi sana!”
Wala usijali! Njoo huku,” aliniambia na kunipeleka pembeni, kulikuwa na viti kadhaa, nikatulia hapo, baadae akaniambia twende kwenye ule mlima mkubwa, tukapaa mpaka tulipofika huko. Kama kawaida ile televisheni kubwa ikawashwa, nilikuwa hapo kwa ajili ya kuona yale yaliyokuwa yakimhusu jini Maimuna tu. Akaanza kazi.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.
Post a Comment