SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-13
NYEMO CHILONGANI
Hakukuwa na kupoteza muda mahali hapo, ilikuwa ni lazima kuondoka na kuendelea na safari mpaka kuhakikisha wanafika juu kabisa alipokuwa akikaa Lusifa. Japokuwa mzee Hamisi alikuwa akilia pale huku akiwa amelishika kapu lile, mzee Hamadi hakutaka kumuacha, geti lile lilipojifungua akamnyanyua na kuanza kuelekea naye ndani.
“Inaniuma sana,” alisema mzee Hamisi huku akijifuta machozi yake.
“Kumuona mkuu ni lazima ujiandae, kumuona Mungu kuna ugumu, mpaka utende mema mengi, na hata kumuona mkuu wetu ni hivyohivyo, haonekani kirahisi, ni lazima umwage damu nyingi” alisema mzee Hamadi.
“Hivi kweli nimemuua mama yangu?”
“Ndiyo! Umemuaa lakini kwa faida sana kwani hata usingemuua, bado angekufa siku nyingine,” alisema mzee Hamadi.
Walikuwa wamesimama sehemu wakizungumza, mzee Hamisi aliumia sana moyoni mwake lakini muda huo haukuwa wa kujuta na kujiuliza juu ya kile kilichokuwa kimetokea, walitakiwa kusonga mbele kwenda upande mwingine kabisa.
Wakati wamepandisha ngazi ndefu, wakalifikia geti jingine, hili lilikuwa kubwa na jekundu ambalo liliandikwa BARDHAZ tena kwa maandishi makubwa. Walipofika hapo, mzee Hamadi akamwambia mzee Hamisi asimame na afanye kile atakachokwenda kufanya.
“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamadi.
“Tunaingia kwa waziri mkuu wa huku,” alijibu mzee Hamadi.
“Kwa hiyo?”
“Inamisha kichwa chako chini kama ishara ya kuabudu,” alisema mzee Hamadi na mzee Hamisi kufanya hivyo.
Geti lile likajifungua, wa kwanza kutoka lilikuwa jitu kubwa lenye umbo mithili ya tembo mkubwa. Kichwa chake kilikuwa ni cha nyani, alikuwa na mapembe huku tumboni akiwa na manyoya mengi kama kondoo.
Meno yake yalifanana na ngiri huku masikio yake yakiwa makubwa kama sahani ya kuwekea chakula. Lilipofika hapo nje, likaanza kuwaangalia wazee hao kwa macho yaliyojaa chuki. Aliwaangalia kwa makini kisha kuwaruhusu kuingia ndani.
Hawakutakiwa kuingia kama kawaida, walichoambiwa ni kugeuka na kuingia kinyumenyume, wakafanya hivyo na kuingia ndani. Ndani ya chumba hicho kikubwa wakakutana na viumbe wengi ambao walikuwa kama yule waliyekutana naye mlangoni.
Hawakusalimia, kila mmoja akaonekana kuwa bize akifanya yake. Waliendelea kupiga hatua mpaka kufika katika sehemu iliyokuwa na ngazi fupi ambazo hazikupanda juu sana, mbele kabisa ya ngazi zile kulikuwa na kiti kimoja kikubwa kilichokuwa na mafuvu ya binadamu pembeni.
“Inamisheni vichwa vyenu,” ilisikika sauti, hawakujua ilikuwa ni sauti ya nani na ilitokea wapi ila walichokifanya ni kutii kile walichokuwa wameambiwa, wakainamisha vichwa vyao kama ishara ya kuabudu.
Mara wakaanza kusikia vishindo kutoka kule kulipokuwa na kiti, hawakujua ni nani lakini baada ya vishindo hivyo kuacha, wakaambiwa wanyanyue nyuso zao. Kiumbe mmoja mkubwa, mwenye umbo kubwa alikuwa amekalia kiti kile huku akiwa na mabawa yaliyoonekana kuharibiwa mno, sehemu nyingine yalikuwa yamechanikachanika sana.
“Mnataka nini?” aliuliza yule kiumbe wa kutisha.
“Tumekuja kumuona mkuu,” alijibu mzee Hamadi.
“Mna shida gani?”
“Ndugu yangu anataka kuwa na nguvu, awamiliki wengine wenye nguvu,” alijibu mzee Hamadi.
Hapohapo kikaanza kusikika kicheko kikubwa kutoka kwa kile kiumbe, alionekana kama amechkeshwa kwa kile alichokuwa ameambiwa. Akatoka pale kitini alipokuwa amekaa na kuanza kipga hatua kuwafuata wazee wale pale walipokuwa.
“Mbona mmekuja kunichekesha?” aliuliza kiumbe kile.
“Hapana mkuu! Anahitaji nguvu.”
“Huyu wa kulialia?”
“Ndiyo mkuu!”
“Nguvu hapewi mtu mwenye moyo wa kike, nguvu anapewa mtu mwenye moyo wa kishujaa na si kama yeye,” alisema kiumbe yule huku akimwangalia mzee Hamisi aliyekuwa akiogopa mno kwani sura ya kiumbe kile, kuiangalia ilitaka moyo mno.
“Mkuu! Naomba umsaidie,” alisema mzee Hamadi.
“Ni muoga, hawezi kufanya maamuzi!”
“Natumaini hatokuwa muoga tena, natumaini hilo.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mkuu!” alisema mzee Hamadi.
Alichokifanya kiumbe yule ni kurudi kule kulipokuwa na kiti chake na kisha kuchukua kisu kisha kuwarudia pale walipokuwa na kumkabidhi mzee Hamisi kisu kile.
“Ninataka niuone ujasiri ambao mwenzako ameusema juu yako,” alisema jitu lile.
“Ujasiri gani?”
“Ninataka umuue mtoto wako mahali hapa. Wakati unamuua, sitaki ulie wala kuhuzunika, ukifanikiwa katika hilo, nitakupa ruhusa ya kumuona mkuu, tena mageti mengine hautopita kama wengine,” alisema kiumbe lile na kisha hapohapo katika hali isiyotegemewa, picha ya binti yake mmoja ikatokea, hakukuwa na kioo, ilitokea kwa mbele na kutakiwa kumchoma kisu mpaka afe.
Alipomwangalia binti yake, moyo wake uliumia mno lakini hakuwa na cha kufanya, alimuua mama yake, hapo, tayari aliandaliwa kwa ajili ya kumuua mtoto wake, ilimuuma mno lakini hakuwa na cha kufanya.
“Yaani ninafanya yote haya kwa ajili ya Ramadhani?” aliujiuliza moyoni pasipo kupata jibu lolote lile.
“Haina jinsi. Nitalipiza kisasi kwa Ramadhani,” alisema na kisha kuchoma pale kulipokuwa na taswira ya binti yake, hapohapo akamuona akianguka chini, akianza kurusha miguu yake huku na kule, damu zikaanza kumtoka puani na mdomoni, watu wote waliokuwa pembeni ya binti yake wakashtuka, hata kabla hawajafanya chochote, palepale akakauka.
Kumbuka.....hakutakiwa kulia wala kuhuzunika, akapokonywa kisu kile.
****
Moyo wake ulimuuma lakini hakuwa na cha kufanya, hakuruhusiwa kuhuzunika hivyo maumivu yale aliyoyapata, yalikuwa moyoni mwake tu. Alipopokonywa kisu kile, wakaambiwa waende katika mlango mmoja wa chumba, huo ulikuwa na jina kubwa lililosomeka Lusifa mlangoni.
Walipofika, mlango ukajifungua na kisha kuingia ndani. Sehemu hiyo ilionekana kuwa tofauti na vyumba vingine, pale kulikuwa na uwanja mkubwa zaidi ya wa mpira wa miguu, mbele kabisa kulikuwa na jumba moja kubwa na la kifahari.
Sehemu hiyo ilikuwa na msisimko wa ajabu, hawakuona kitu chochote kile cha kutisha lakini kila walipokuwa wakilisogelea jumba lile, walikuwa wakisisimka mno. Mbele kabisa wakakutana na watu wengi warefu, urefu wao unaweza kufikia ule wa twiga, walikuwa na mapembe kama ya ng’ombe, chini walikuwa na kwato za kondoo.
Walikuwa wakitisha sana, walipowaangalia vizuri wakagundua kwamba hao walikuwa majini, yale yaliyokuwa yakija duniani huku wakiwa na maumbo hayo na kuwatisha watu.
Hawakuonekana kujali, wakazidi kupiga hatua kuelekea mbele zaidi, huko, wakakutana na sehemu iliyokuwa na bwawa kubwa kama haya yaliyokuwepo duniani (swimming pool), bwawa lile halikuwa la maji bali lilikuwa ni la damu tu.
Pembeni ya bwana hilo kulikuwa na mabomba makubwa kadhaa, mabomba hayo yalikuwa na kazi ya kumimina damu ndani ya bwawa lile. Katika mabomba yale kulikuwa na maneno yaliyokuwa yameandikwa, moja liliandikwa magari, hilo lilikuwa bomba pekee lililokuwa na kazi ya kukusanya damu kutoka kwa watu waliopata ajali za magari duniani.
Huku duniani watu wanapopata ajali, na kama ile ajali ni ya kishetani, basi zile damu zao zinakwenda katika bwana lile kupitia bomba lile. Mbali na bomba hilo, pia kulikuwa na bomba jingine lililoandikwa ndege, hilo nalo lilikuwa na kazi hiyohiyo.
Haikuishia hapo, kulikuwa na megine yameandikwa treni, meli na pikipiki, yote hayo yalikuwa yakipitisha damu kuelekea katika bwana hilo. Mbali na mabomba yote hayo, kulikuwa na bomba jingine ambalo liliandikwa mhanga.
Hili lilikuwa bomba pekee ambalo lilipitisha damu za watu waliokuwa wakifariki duniani mara mtu fulani anapojitoa mhanga na kuwaua watu kadhaa katika mkusanyiko wa watu anapokwenda kujitolea mhanga.
Hapa ningependa niseme kitu ili watu wanielewe. Mtu unapomuona anakwenda sehemu fulani kujitoa mhanga, huwa anapewa elimu ya chuki. Anaweza akaambiwa bwana Waafrika ni watu wabaya mno, nenda kawaue kwani usipowaua, watakuua wewe na kukuolea dada yako.
Maneno yale hayaendi hivihivi, bali mtu yule huanza kupandikizwa chuki kali na watu waliokuwa na uwezo wa juu wa kupandikiza majini mioyoni mwa watu wale, na wanapoondoka pale, yale majini yanawatia nguvu na kuwaambia kweli Waafrika ni watu wabaya, kawaue, hawafai kabisa, watakuja kukuolea dada zako, yule mtu anakwenda na kujitoa mhanga na hatimaye watu wanaokufa, damu zinachukuliwa na kuingia ndani ya bwawa lile.
“Mmmh!”
“Usigune, huku kuna utajiri wa damu,” alisema mzee Hamadi, hapohapo damu zikaanza kumwagikia ndani ya bwawa lile kupitia katika bomba kubwa lililoandikwa magari kuonyesha kwamba tayari huko duniani kulikuwa na ajali mbaya ilitokea na watu kufariki.
Walikwenda mbele mpaka walipoanza kuziona ngazi na kuanza kupandisha, huko, wakakutana na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamevaa mavazi makubwa kama madela, yalikuwa na rangi nyeusi na juu yao kulikuwa na vitu kama vikofia ambavyo viliunganishwa kupitia mavazi yale.
Watu wale walikuwa wamepiga magoti katika jengo kubwa, walionekana kama kusubiria kitu fulani, hivyo mzee Hamadi na Hamisi wakaanza kupiga hatua kuelekea kule kwani nao walihitaji kushiriki hata kabla huyo kiongozi hajafika.
“Mnakwenda wapi?” walizuiwa na kuulizwa, yule aliyewazuia alikuwa kiumbe wa ajabu pia.
“Tunakwenda kuabudu, tunakwenda kumuabudu mkuu!”
“Na huyu ni nani?”
“Ni mgeni.”
“Mara yake ya kwanza kufika hapa?”
“Ndiyo!”
“Nendeni kule mkajiandae, hamtakiwi kuingia pale hivihivi,” alisema kiumbe kile cha ajabu huku akiwaonyesha sehemu iliyokuwa na damu nyingi.
Wakaelekea hapo, hawakuwa peke yao, kulikuwa na kundi la watu kama kumi na tano hivi waliokuwa wakinywa damu zilizokuwa kwenye bakuli kubwa, walionekana kufurahia uwepo wao mahali hapo.
Nilipokuwa nikiwaangalia watu wale, niliwaona watu maarufu nao wakiwa mahali pale, walikuwepo wanamuziki wakubwa duniani, wanasiasa, matajiri na watu wengine wengi ambao nisingependa kuwataja mahali hapa.
Nao wakaungana nao na kuanza kunywa zile damu, hayo ndiyo yalikuwa matakaso hata kabla ya kwenda kuonana na shetani ambaye alipenda kuitwa kwa jina la Lusifa.
Walipokunywa damu zile, nao wakapewa mavazi meusi kama waliyovaa watu wale na kisha kusogea kule walipokuwa wale watu wanaoabudu, walipofika, nao wakapiga magoti chini na kuinamisha vichwa vyao.
Ni ndani ya dakika chache tu wakaanza kusikia vishindo vya mtu akija mahali hapo, alikuwa shetani mwenyewe, hawakutaka kuviinua vichwa vyao, walitakiwa kuvituliza vilevile kama walivyokuwa, shetani huyo akakifuata kiti, akakikalia na kuwaambia watu wote wainue vichwa, kile alichokiona mzee Hamisi, ilikuwa bado kidogo tu azimie.
Je nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa
Post a Comment