ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-12


 
 NYEMO CHILONGANI
“Tuondoke!” alisema mzee Hamadi.
“Inaniuma sana,” alisema mzee Hamisi huku akiwa pale chini akiiangalia maiti ya yule mwanamke.
“Tuondoke geti litafunga,” aliendelea kusisitiza mzee Hamadi ambapo hapohapo mzee Hamisi akanyanyuka na kuanza kuondoka mahali hapo.
Moyo wake bado uliendelea kuwa kwenye maumivu makali, hakuamini vile vilivyokuwa vikitokea kule kuzimu, vilimtisha, vilimhuzunisha na kumpa huzuni kubwa moyoni mwake, katika kila geti alilotakiwa kupita, ilikuwa ni lazima afanye mauaji, tena kwa mkono wake mwenyewe.
“Wewe mbona hutaki kuua?” aliuliza mzee Hamisi.
“Siwezi kuua kwa sababu nimeshaua sana nilipokuja kwa mara ya kwanza, huku nimekuleta wewe, unatakiwa kuwa makini sana, wakati mwingine unaweza kufa wewe,” alisema mzee Hamadi.
Wakati huo walikuwa wakipiga hatua kuelekea mbele zaidi, walikuwa wakilifuata geti jingine la tatu. Mzee Hamisi alikuwa akijifikiria juu ya geti la tatu, hakujua ni kitu gani ambacho angekikuta huko, akabaki kimya, hakutaka kujifikiria sana kwani aliamini kwamba angejisumbua tu.
Walipita katika jumba hilo, walikuwa wakielekea juu kabisa. Walipofika katika korido moja kubwa iliyokuwa na sakafu nyeusi, wakaingia katika chumba kimoja ambacho mzee Hamadi alimwambia kwamba kilikuwa chumba cha mapumziko, huko wangekula na kunywa.
Ndani ya chumba kile kulikuwa na meza kubwa, kuangalia juu yake, kulikuwa na chupa moja kubwa, ilikuwa ni kama ya soda, ndani kulikuwa na maji mekundu ambayo kwa harakaharaka mzee Hamisi akagundua kwamba ile ilikuwa damu.
Mbali na chupa ile, pia kulikuwa na mabakuli makubwa yaliyosheheni nyama iliyokuwa ikinukia vizuri kabisa. Wakaanza kupiga hatua kuifuata meza ile ndefu iliyozungukwa na viti zaidi ya ishirini na kisha kuchukua vikombe na kuanza kuimimina damu ile na kuanza kunywa.
Mzee Hamisi alikuwa mchawi, hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kunywa damu, alikwishawahi kunywa walipokuwa katika uwanja wa kichawi hivyo ile ilikuwa ni kama kujikumbushia tu.
Nyamza zile zilizokuwa zikionekana katika mabakuli hazikuwa nyama za ng’ombe au mbuzi, zilikuwa ni nyama za binadamu zilizokatwa vipandevipande, hapohapo wakaanza kuchukua na kuanza kula.
“Usiniangushe rafiki yangu,” alisema mzee Hamadi.
“Sitoweza kukuangusha.”
“Sasa kwa nini umekuwa na moyo wa huruma hivyo?”
“Huwa inatokea, ila nakuahidi kwamba sitokuangusha tena,” alisema mzee Hamisi huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Kama ni hivyo, sawa, tuendelee na safari,” alisema mzee Hamadi na safari kuanza tena.
Walitembea kwa mwendo wa harakaharaka kama watu wanaowahi sehemu fulani. Hawakuzungumza kitu chochote kile mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na geti jingine la kuingilia sehemu ya upande wa pili, kama yalivyokuwa mageti mengine yaliyopita, hata lile geti la tatu nalo lilikuwa limefungwa.
“Tunafanyaje? Ufunguo upo wapi?” aliuliza mzee Hamisi.
“Subiri kwanza.”
Mzee Hamisi ndiye aliyeonekana kuwa na presha sana kana kwamba hilo lilikuwa geti la mwisho ambapo baada ya kulifungua angekutana na shetani. Kila wakati alikuwa akimuuliza mzee Hamadi juu ya ufunguo wa kufungulia geti lile lakini mzee Hamadi hakusema kitu zaidi ya kumwambia kwamba anapaswa kusubiri.
“Hakuna kitu.”
“Subiri kwanza, wala usijali.”
Hawakukaa sana, ni ndani ya dakika chache tu, ghafla likatokea giza kubwa mahali hapo kiasi cha kutoweza kuonana. Mzee Hamisi aliogopa mno, alikuwa akiweweseka huku akihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao.
Akaanza kupapasa huku na kule ili hata aweze kumgusa mzee Hamadi lakini hakuweza kufahamu mahali alipokuwa hali iliyomfanya kuwa na hofu kubwa moyoni mwake kiasi cha kutetemeka mwili huku kijasho chembamba kikimtoka.
“Hamadi! Upo wapi?” aliita mzee Hamisi.
“Nipo hapa.”
“Wapi?”
“Hapana niliposimama.”
“Kuna nini tena? Mbona giza sana?” aliuliza mzee Hamisi huku akiwa na hofu kubwa.
“Ufunguo unakuja.”
“Upo wapi?”
“Nisikilize kwa makini. Nakupa maelekezo juu ya unachotakiwa kukifanya,” alisema mzee Hamadi.
“Sawa. Nipe maelekezo.”
“Hapo mbele yako kuna vikapu vitatu vyenye majina ya watu watatu.”
“Ndiyo!”
“Kikapu kimoja kina jina la mtoto wako wa mwisho, yule unayempenda sana, kikapu cha pili kina jina la mke wako na kikapu cha tatu kina jina la mama yako,” alisema mzee Hamadi.
“Nifanye nini sasa na hivyo vikapu?”
“Unatakiwa kuchagua kikapu kimoja, utakachokigusa, mtu mwenye jina lake ndani ya kikapu hicho atakufa muda huohuo,” alisema mzee Hamadi.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo. Sogea mbele, kuna mwanga utatokea na vikapu hivyo kuonekana mbele yako. Chaguakimoja tu, kisha mlango utajifungua,” alisema mzee Hamadi.
“Kwa nini yote yanatokea?”
“Ni kwa sababu huwezi kumuona Lusifa pasipo kutoa sadaka ya damu,” alisema mzee Hamadi.
Mzee Hamisi hakuwa na jinsi, kama ni maji, tayari aliyavulia nguo na wakati huo alitakiwa kuyaoga, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kwenda mbele, alipofika karibu na mlango ule, vikapu vitatu vikaonekana mbele yake na ndani vilikuwa na majina ya watu watatu ambao alikuwa akiwapenda sana.
Hakujua ni kikapu gani kilikuwa na jina gani, alichotakiwa ni kuchagua tu kikapu pasipo kujua ndani kulikuwa na jina gani. Mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda, alikuwa kwenye mtihani mgumu mno.
Watu wote watatu ambao alitajiwa alikuwa akiwapenda mno, ila hakuwa na jinsi kwa wakati huo, alitakiwa kuchagua kapu moja na mtu mmoja kufariki dunia, hivyo alitakiwa kufanya hivyo ili geti lifunguke.
Akakishika kikapu kimoja ambacho hakujua kulikuwa na jina gani, ghafla akahisi akianza kububujikwa na machozi ya uchungu, alipochungulia ndani, akakutana na jina la mama yake. Akajikuta akipiga magoti na kuanza kukipiga kifua chake kwa maumivu makali.
“Uwiiiiiiiiiiii.....” alijikuta akianza kulia kwa sauti kubwa.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.