ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-11

 

NYEMO CHILONGANI

Moyo wake ulikuwa na hofu tele, uso wa mwanamke yule mzee bado uliendelea kumtia huruma kubwa kiasi kwamba aliona kulikuwa na ugumu mkubwa wa kuweza kufanya kile alichokuwa ameambiwa.
“Muue haraka mlango ufunguke,” alisema mzee Hamadi kwa sauti kubwa.
Kwa mzee Hamisi, lile likaonekana kuwa jambo gumu, kilichompa ugumu wa kumuua mwanamke yule ni sura ya kipole aliyokuwa nayo. Hakuwa radhi kuona akimuua mwanamke huyo na wakati hata muonekano wake ulionyesha kwamba alikuwa na shida mno katika maisha yake.
Pamoja na kukataa huko lakini bado mzee Hamadi alikuwa akimsisitiza kwamba alitakiwa kumuua ili waendelee mbele kwani mlango ule wa kwanza usingeweza kufunguka pasipo kumuua mwanamke yule.
“Kama hautaki sema turudi na usimuone Lusifa,” alisema mzee Hamisi.
Kitendo cha kulitaja jina la Lusifa tu, mzee Hamisi akajikuta moyo wake ukipata nguvu, huruma aliyokuwa nayo ikaanza kupungua, akajikuta akichukua panga lile lililokuwa pembeni na kisha bila kumwangalia usoni mwanamke yule akaanza kumshambulia na panga lile, alikuwa akimkatakata kichwani na maeneo mengine ya mwili wake.
Damu zilitapakaa sehemu hiyo yote, japokuwa sauti ya mwanamke yule ilisikika masikioni mwake akiomba msamaha lakini mzee Hamisi hakujali hilo, alichokifanya ni kuendelea kumkatakata na panga lile mpaka pale alipokufa, hapohapo geti lile kubwa likafunguka.
“Tuondoke. Hongera sana, umefanikiwa,” alisema mzee Hamadi huku akionekana kurufahia.
Wakaingia ndani, wakaanza kupiga hatua na kuelekea sehemu ambayo aliambiwa kwamba kulikuwa na geti la pili.
Walitembea kwa harakaharaka, hakukuwa na mtu yeyote ambaye walipishana naye njiani lakini kwa hali halisi ni kwamba walipishana na majini pasipo kufahamu hilo. Walitembea mpaka walipofika katika geti moja kubwa ambalo hilo lilikuwa ni geti la pili kuelekea kule kwa Lusifa, hivyo walitakiwa kupita.
Walichokifanya ni kulifuata geti hilo na kutaka kulifungua, kama lilivyokuwa lile la mwanzo, hata hilo lilikuwa gumu kufunguka. Huku wakijifikiria nini cha kufanya, mara kukatokea mwanamke mmoja akiwa mjauzito, alionekana kuwa kwenye nyakati za mwisho kujifungua na alipowaona tu, alihitaji msaada wa kusaidiwa kwani hakukuwa na watu wengine wa kuwaomba msaada zaidi yao.
“Kwanza tungemsaidia huyu mwanamke,” alisema mzee Hamisi.
“Hakuna kumsaidia.”
“Kwa nini na wakati anahitaji msaada?” aliuliza mzee Hamisi.
“Ukimsaidia, unakufa wewe.”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo!”
“Hapana! Mimi nataka nimsaidie, ni mwanamke mjauzito, anahitaji sana msaada,” alisema mzee Hamisi huku akimwangalia mwanamke yule kwa macho yaliyojaa huruma tele.
“Hamisi! Nisikilize kwa makini. Nikwambie.”
“Kitu gani.”
“Unataka kumuona Lusifa?”
“Ndiyo! Tena nina hamu kubwa.”
“Basi muue huyu mwanamke!”
“Unasemaje?”
“Muue huyu mwanamke kwa kumpiga ngumi za tumbo, tena mfululizo,” alisema mzee Hamadi huku akimaanisha kile alichokuwa akikisema.
Mwanamke yule mjauzito ambaye alikuwa akiomba msaada ndiye aliyekuwa ufunguo wa geti lile la pilii kuelekea kwa Lusifa. Hilo lilionekana kuwa gumu mno kwa mzee Hamisi kwani kila alipokuwa akimwangalia mwanamke yule, hakika alitia huruma sana.
Alipoambiwa kwamba ndiye aliyekuwa ufunguo wa geti lile, kwanza akabisha kwani muonekano wa mwanamke yule ulionyesha kwamba alihitaji msaada wa hali na mali.
“Ukimsaidia utakufa,” yalijirudia maneno yale aliyosema mzee Hamdai, maneno ambayo yalimfanya kuwa na hofu kubwa moyoni mwake.
“Muue haraka tuendelee na safari,” alisema mzee Hamadi.
Hiyo ndiyo ilikuwa njia ya kuweza kupita katika geti lile, mwanamke yule hakunyamaza, bado aliendelea kulia huku akiomba msaada wa kusaidiwa pale alipokuwa kwani alionekana kuwa katika kipindi cha kutaka kujifungua.
Huku wakiendelea kumwangalia, mara damu zikaanza kumtoka mwanamke yule sehemu za siri, alionekana kuzidiwa na kama asingepewa msaada mahali pale basi angeweza kufariki dunia. Kama walivyokuwa binadamu wengine, mzee Hamisi alishikwa na huruma ya kiwango cha juu kabisa, kile kilichokuwa kikitokea, alihisi isingekuwa roho nzuri kama angemwacha mwanamke yule akiendelea kuteseka.
“Anakaribia kujifungua, fanya haraka, mpige ngumi, mtoto akitoka tu tutakufa,” alisema mzee Hamadi huku akimshikashika mzee Hamisi kama kumsisitiza juu ya kile alichotakiwa kukifanya mahali pale.
Hakukuwa na la kufanya, kwa kuwa ndiyo ilikuwa moja ya masharti aliyokuwa amepewa ya kufungua geti lile, hapohapo akaanza kumpiga mwanamke yule ngumi za tumbo. Moyo ulimuuma mno, alijiona kuwa mtu katili lakini hakutaka kuona akishindwa kumuona Lusifa na wakati kumuona huko aliamini kwamba angepata nguvu kubwa na hata kumiliki majini yaliyokuwa na uwezo mkubwa.
Ngumi zile zikampeleka mwanamke yule chini, alikuwa akiugulia kwa maumivu makali, damu ziliendelea kumtoka huku mtoto akianza kutoka katika njia ya kujifungulia.
“Nimeua...” alisema mzee Hamisi, machozi yalikuwa yakimtoka.
“Usijali! Ni sehemu ya kumuona mkuu wetu, tuondoke,” alisema mzee Hamadi.
Mzee Hamisi hakutaka kuondoka, kwanza akapiga magoti chini na kumwangalia mwanamke yule, machozi yalikuwa yakimbubujika tu. Hapohapo, mwanamke yule na mtoto wake, wakafariki dunia. Geti likafunguka.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.