ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU - 10


NYEMO CHILONGANI
0718069269
Hofu zilizidi kuongezeka mioyoni mwao, hawakuamini kile kilichokuwa kikija mbele yao, mawimbi makubwa mithili ya ghorofa nne yalikuwa yakiwafuata kule walipokuwa, hawakutaka kusubiri, wakaanza kutimua mbio kurudi nyuma.
Walikimbia kwa kasi kubwa lakini kila walivyogeuka nyuma, mawimbi yalikuwa yakija kwa kasi. Mbio zile ziliendelea kwa umbali fulani na ndipo waliposimama baada ya kusikia ukimya mkubwa nyuma yao, walipogeuka, hakukuwa na kitu chochote zaidi ya lile pori walilokuwa wakilifuata.
Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya zaidi ya kuondoka huku wakihesabia kwamba walishindwa kwa kile walichotaka kukifanya. Hawakuwa na sehemu nyingine ya kwenda zaidi ya kurudi nyumbani huku kila mmoja akionekana kuwa na mawazo.
“Umefikiria nini?” aliuliza mzee Hamisi, alionekana kuchanganyikiwa.
“Inabidi tuondoke hapa.”
“Kwenda wapi?”
“Tongoni.”
“Mmmh!”
“Usigune, huko ndiyo nuksi, hakuna sehemu iliyokuwa na wataalamu wa kuroga kama huko, ni balaa,” alisema mzee Majoka.
“Ila nasikia ni mbali, tutaweza kufika leoleo?”
“Haitowezekana, hapa kitu cha msingi tuondoke kesho asubuhi na mapema kwenda huko,” alisema mzee Majoka.
Hawakuwa na jinsi, kwa kuwa walikwenda Tanga kwa ajili ya kazi moja tu, hawakukubali kurudi kirahisi pasipo kukamilisha kile walichokuwa wakitaka kukamilisha. Usiku wa siku hiyo, walikuwa wakizungumza namna ya kukabiliana na Ramadhani ambaye alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.
“Huyu kijana ni balaa,” alisema mzee Hamisi.
“Kwani ilikuwajekuwaje mpaka ukataka kupambana naye?” aliuliza mzee Majoka na mzee Hamisi kuanza kuhadithia kile kilichokuwa kimetokea.
“Kuna watu balaa, usipende kuwaingilia kichwakichwa, utauawa,” alionya mzee Majoka.
Hakukuwa na mtu aliyelala mapema siku hiyo, kwa kuwa alikuwa amepata ugeni, mzee Majoka hakuondoka usiku kwenda kuwanga, walibaki mpaka saa nane ya usiku ndipo wakalala.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema wakaamka na kujiandaa kwa safari ya kuelekea Tongoni. Huko hakukuwa karibu, kutoka hapo Handeni mpaka huko ilikuwa ni zaidi ya masaa matano kwa gari la kawaida na kutokana na ubovu wa barabara, walitarajia kutumia masaa nane njiani.
Wakabeba mizigo yao, wakaikabidhi safari yao kwa majini yao na kisha kwenda huko Tongoni kwa mzee aliyekuwa nuksi kuliko wote, huyo alitwa mzee Hamadi, mzee aliyekuwa na mguu mbovu, akichechemea lakini kwenye suala zima la uchawi, hakuwa mtu wa kuchezewa.
Tongo kilikuwa moja ya vijiji vilivyojaa wachawi kuliko sehemu zote nchini Tanzania, huko kulikuwa na uchawi wa kila namna, watu wengi waliokuwa wakitafuta utajiri walikwenda huko na hata wale waliokuwa wakitaka kuwatoa watu kafara ya damu, sehemu ya kwanza kwenda ilikuwa Tongoni.
Uchawi wa Tongoni ulikuwa tofauti na uchawi wa sehemu nyingine, huko, kila mtu alionekana kuwa mtaalamu wa kuroga jambo lililowafanya uchawi wao mwingi kwenda kufanyia nje ya kijiji hicho.
Kutokana na umbali wa sehemu yenyewe, walichukua masaa saba mpaka kufika Tongoni ambapo huko wakapokelewa kwa ukarimu mkubwa kwani mzee Majoka alijulikana sana kutokana na uchawi aliokuwa akiufanya kutetemesha Handeni yote.
“Mnacheza na mtu hatari sana,.” Alisema mzee Hamadi hata kabla wageni wake hawajaelezea kile kilichokuwa kimewaleta.
“Umejuaje?”
“Huyo mtu ni hatari sana, ni mkuu wa uchawi kule Magharibi, ana nguvu mno na anaweza kukuueni siku yoyote ile na mahali popote,” alisema mzee Hamadi.
“Ramadhani ni mkubwa wa wachawi Magharibi?”
“Ndiyo! Ni mtu wa kukaa mbali sana kwani anatisha.”
“Sawa. Ila sisi tumekuja utufanyie mambo, tunataka tumuondoe,” alisema mzee Hamisi.
“Jamani! Hivi nilivyowaambieni kuhusu yeye, mnafikiri mimi nitamuweza kweli?” aliuliza mzee Hamadi huku akiwashangaa.
“Kwa hiyo unashindwa?”
“Ndiyo!”
“Na hakuna njia ya kumpoteza?”
“Ipo.”
“Ipi hiyo?”
“Ni lazima ufuge majini,” alijibu mzee Hamadi.
“Nifuge majini? Mbona ninayo mengi tu!” alisema mzee Hamisi.
“Hayo majini ni machache sana, halafu majini yako hayana nguvu ya kutosha, mwenzako huyu ana majini yale makubwa ambayo yana roho mbaya na muda wote yapo yanamlinda, cha kufanya na wewe ni kutafuta majini makubwa na yenye nguvu ambayo yataweza kupambana na majini ya huyu,” alisema mzee Hamadi.
“Hayo majini nitayapata wapi?”
“Nyumbani.”
“Wapi?”
“Kuzimu. Huko ndipo utakapoyapata hayo majini mengine.”
“Kwa hiyo natakiwa kwenda huko? Nitakwendaje? Sijawahi kwenda huko kwani nasikia wote wanaokwenda huko huwa na vibali maalumu,” alisema mzee Hamadi.
“Nitakupeleka!”
“Nitashukuru sana.”
Kidogo moyo wa mzee Hamisi ukapoa, hakuamini kama naye angefanikiwa kwenda kuzimu. Ngoja niwaambie kitu kimoja. Katika suala la kwenda kuzimu halikuwa la kawaida hata kidogo, kwa kila mchawi alikuwa akitamani kwenda huko lakini si kila mtu aliyewwahi kufika.
Kuna mtu mwingine anakuwa mchawi tangu akiwa mdogo lakini mpaka anazeeka na kufariki, hajawahi kukanyaga huko. Hiyo ni sawa na mawaziri wetu. Unaweza kuwa waziri lakini katika miaka yote kumi, unaweza usikanyage ikulu, hivyo ndivyo ilivyokuwa hata kwa wachawi kuingia kuzimu.
Alipoambiwa hivyo, mzee Hamisi alifurahi sana, ni kweli alihitaji kwenda huko na ndiyo maana aliambiwa kwamba alipaswa kujiandaa na hakukuwa sehemu ya mchezomchezo. Hilo wala halikuwa tatizo, ilipofika usiku, akaambiwa kwamba safari hiyo ingefanyika baharini, hivyo walitakiwa kupanda ungo na kwenda huko sehemu ambayo ndiyo yalikuwa makazi makuu ya shetani. Safari ikaanza.
Mzee Hamisi alikuwa na hamu kubwa ya kufika kuzimu, kitu alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni kufuga majini tu, tena yale yenye nguvu kubwa ambayo aliambiwa kwamba ndiyo yangeweza kumuua Ramadhani kama alivyokuwa akitaka.
Usiku huohuo wakachukua ungo, ndani yake kulikuwa na tunguli nyingi na walikuwa wakienda kwa mwendo wa kasi mno. Kwa wakati huo, safari yao ilikuwa ni kuelekea katika Bahari ya Hindi ambapo huko ndipo wangepita na kuelekea kuzimu.
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika ufukweni ambapo moja kwa moja wakateremka na mzee Hamadi kuchukua mayai mawili na kuyatupa mule baharini kisha kumwambia mzee Hamisi waingie ndani ya yale maji.
Mara ya kwanza mzee huyo alikuwa akiogopa, alipopiga hatua ndani ya maji na kusogea mbele, aliona kwamba angeweza kuzama hivyo akaanza kwenye kwa machale sana. Kwa muonekano aliokuwa nao tu mahali hapo, ulitosha kukwambia kwama alikuwa na hofu kubwa ya kukumbana na kitu kibaya, alichokifikiria zaidi ni kuzama tu.
“Hatutoweza kuzama?” aliuliza huku akionekana kuwa na hofu.
“Hatuwezi, huku ndipo makao makuu, huku ndipo ilipo ikulu yetu,” alisema mzee Hamadi.
Tayari maji yaliwafikia vifuani, mzee Hamisi aliendelea kuogopa zaidi lakini baada ya maji kuwafikia machoni, ghafla wakajikuta wakiwa katika ulimwengu mwingine kabisa, kulipokuwa na mji mwingine, kwa muonekano tungesema dunia nyingine kabisa.
Mzee Hamisi akabaki akiangalia huku na kule, kuzimu kulikuwa kama duniani, kama ambavyo huku tuna serikali yetu basi napo kule kuna serikali yao pia, kama huku watoto walikuwa wakielekea shuleni kusoma basi hata kule ilikuwa hivyohivyo.
Hakukuwa na mabadiliko makubwa japokuwa kule hakukuwa na binadamu, kulikuwa na viumbe vya ajabuajabu ambavyo kama ungekuwa nje ya ulimwengu ule ilikuwa ni lazima kuogopa sana.
Wakaanza kupiga hatua kuelekea sehemu iliyokuwa na njia nyembamba ambayo ilizungukwa na majani mengi. Moyo wa mzee Hamisi ulikuwa na mengi ya kuuliza lakini aliamua kukaa kimya mpaka pale ambapo angeruhusiwa kuuliza kitu chochote kile.
Wakafika katika nyumba moja, ilikuwa kubwa mno, nje ya nyumba ile kulikuwa na miti miwili iliyokuwa imesimikwa chini, juu ya miti ile kulikuwa na mafuvu ya watu yaliyoonekana kukauka mno. Wakaanza kupanda ngazi kueleka katika jumba lile.
“Ni wapi hapa?” aliuliza mzee Hamisi kwa sauti ya chini.
“Hapa ni kwa mkuu wa mkoa!”
“Mkuu wa mkoa?”
“Ndiyo!”
“Kivipi tena? Mbona unanichanganya?”
“Huku pia kuna serikali kama ilivyo duniani, kuna balozi wa nyumba kumi, wakuu wa wilaya, mikoa, bunge, mawaziri na hata rais,” alisema mzee Hamadi.
“Huwa nao wanazungumzia bajeti na mambo mengine?”
“Hapana! Huku watu wapo bize kuzungumzia mambo mengi kuhusu kuiteka dunia, watu wasiweze kwenda makanisani wala misikitini, hicho ndicho wanachokizungumzia sana huku, kuiangusha dunia,” alijibu mzee Hamadi.
Tayari walikuwa wamefika katika mlango wa kuingilia ndani ya jumba lile kubwa hasa mara baada ya kupandisha ngazi kadhaa. Wala hawakugonga mlango, wakaona ukijifungua na kuingia ndani.
Mandhari yaliyokuwa ndani, mzee Hamisi akajikuta akitamani japokuwa baadhi ya vitu havikuwa kama duniani. Kulikuwa na televisheni kubwa ikiwa imepachikwa ukutani, ilikuwa na ukubwa wa inchi 40.
Mbali na televisheni ile, pia kulikuwa na makochi makubwa, yalikuwa na rangi nyekundu na alipouliza, aliambiwa kwamba makochi yale hayakutengenezwa kwa kutumia vitambaa bali yalitengenezwa kwa kutumia ngozi za binadamu ambazo kule zilikuwa dili mno.
Juu ya meza ya kioo kulikuwa na birika moja kubwa na pembeni yake kulikuwa na jagi la jeupe. Mzee Hamisi alipoliangalia vizuri jagi lile, akagundua kwamba ndani yake kulikuwa na damu kwani ilikuwa nyekundu mno.
“Kuna kitu nataka nikuonyeshee,” alisema mzee Hamadi.
“Kitu gani?”
“Nataka nikuonyeshee maiti mbalimbali.”
“Maiti zipi?”
“Kila wiki zinaletwa maiti humu.”
“Kazi yake nini?”
“Kwa ajili ya nyama tu.”
Wakati wanazunguka ndani ya nyumba hiyo kubwa na ya kifahari, hawakuwa peke yao bali walikuwa wakipishana na viumbe vya ajabu ambavyo kwa kuviangalia tu, mzee Hamisi alijawa na hofu kubwa, wakati mwingine alitamani kukimbia, akajikuta akifumba macho tu.
Wakafika katika mlango mmoja ambao uliandikwa maneno ambayo wala hakuyaelewa, mzee Hamadi akagonga hodi na baada ya sekunde kadhaa, mlango ukafunguliwa na mwanamke mmoja mrembo wa sura, alimvutia hadi mzee Hamisi.
Alikuwa msichana mrefu, mweupe, nywele zake zilifika kiunoni, alipendeza kumwangalia na kila alipokuwa akitabasamu, uzuri wake uliongezeka zaidi.
“Usitabasamu,” alisema mzee Hemedi, alikuwa akimwambia mzee Hamisi.
“Kwa nini? Yeye si ndiye aliyeanza kutabasamu?”
“Hata kama! Ukitabasamu kama alivyotabasamu, huwa anakasirika sana,” alisema mzee Hamadi.
“Kwa nini? Kwani yule nani?”
“Unamjua jini Maimuna?”
“Namsikiasikia tu, si yule wa mapenzi?”
“Ndiyo!”
“Huwa ninamsikia tu.”
“Ndiye yule aliyetufungulia mlango!”
“Kumbe ni mzuri vile!”
“Ndiyo! Twende mbele kwanza, kuna mengi ya kukuonyesha.”
Wakaendelea kusonga mbele mpaka kwenye mlango mmoja mkubwa uliokuwa na rangi nyeusi, walipouangalia mlango ule, ulionekana kuwa tofauti na milango mingine. Mlangoni kulikuwa kumeandikwa maneno makubwa yaliyosomeka SONYITO, maneno ambayo mzee Hamisi hakuyaelewa kabisa.
“Sonyito ndiyo nini?”
“Maiti zinazozungumza.”
“Mmmh!”
“Ngoja tuingie, utaziona tu,” alisema mzee Hamadi na kisha kuanza kuugonga mlango ule, kwanza kwa mbali, wakaanza kusikia sauti ya vilio kutoka ndani ya chumba kile, mzee Hamisi akaanza kuogopa, alitamani kumwambia mzee Hamadi warudi walipotoka.
Mwili ukaanza kumtetemeka na kijasho chembamba kumtoka. Mlango ukafunguliwa, huyo aliyeufungua, hakuonekana kuwa jini wa kawaida, alikuwa ni wa tofauti sana na majini wengine.
“Mama yangu!” alijikuta akijisemea mzee Hamisi huku mapigo yake ya moyo yakianza kudunda kwa kasi. Hofu ikamjaa.
Aliyesimama mbele yao alikuwa jini makata, jini mkorofi aliyekuwa na kazi moja ya kuwatesa watu kule kuzimu. Ngoja nikwambie kitu kimoja, unapofika kuzimu huwa kunakuwa na yale majini ambayo yalipewa kazi ya kufanya lakini kwa bahati mbaya yakajikuta yakishindwa. Kule kuzimu hakuna kitu kinachoitwa kushindwa hivyo uadhibiwa.
Mbali na majini hayo, huwa kunakuwa na zile maiti za watu waliokufa lakini makazi yao huwa ni ya kuzimu milele. Maiti zile huwa zinachukuliwa na kupelekwa huko ambapo hupewa roho chafu na kisha kuanza kuadhibiwa kwani roho ile yenyewe inakuwa imekwishakwenda kwenye hukumu.
Huyo ndiye alikuwa jini makata, alitisha, alikuwa na kichwa kama cha paka, alikuwa na nywele nyingi kama simba, kila alipoongea, meno yake yaliyochongeka yalionekana vizuri. Kuna kipindi kingine hasa anapokuwa na hasira kali, kila anapoongea huwa anatoa cheche mdomoni mwake.
Jini yule alipowaona watu hao, hakuzungumza kitu chochote, aliwaruhusu kuingia ndani na kuona jinsi maiti zile zilivyokuwa zikiteswa kule kuzimu. Yalikuwa mateso makubwa na zilipiga kelele mno lakini hakuonekana kujali chochote kile, aliendelea kuzitesa kama kawaida yake.
Alichukua mikuki mikubwa iliyokuwa na ncha kali ambayo iliwekwa kwenye moto na kuwa nyekundu mno kisha kuanza kuzchoma kana kwamba alizichoma na miti ya mishikaki na kisha kuanza kuzipiga huku na kule.
Alipoona hiyo haitoshi, alikuwa akichukua rungu moja kubwa na kuanza kuzipiga kwa zamu. Hiyo ilikuwa ni kazi yake ya kila siku na wala hakuchoka kabisa. Yalikuwa ni mateso makali lakini hakuacha, hizo zilikuwa adhabu kwa kuwa walishindwa kufanya kile walichotaka kukifanya.
Mzee Hamisi alikuwa na hofu kubwa, ni kweli alifuga majini lakini hakuwahi kuona jini aliyekuwa na sura mbaya kama aliyokuwa nayo jini makata. Alitisha sana lakini akashindwa kukimbia.
Walizunguka ndani ya kile chumba kwa dakika kadhaa kisha kuondoka na kuelekea katika jumba jingine kabisa, huko ndipo alipoambiwa kwamba rais wa kuzimu, shetani alipokuwa akiishi.
Aliwahi kuzisikia hadithi nyingi kuhusu shetani, siku hiyo alikuwa mahali hapo kwa ajili ya kumuona huyo shetani mwenyewe ambaye kila siku aliifanya kazi zake kama mfuasi wake duniani.
Walipiolifikia jumba hilo, wakaanza kupandisha ngazi na kuona kibao fulani kikubwa kilichoandikwa LUCIFER PARADISE. Hapo, akatakiwa kuinamisha kichwa chake kama kutoa ishara ya kumuabudu na kisha kuruhusiwa kuingia ndani ya jumba hilo kubwa.
“Hapa ndipo kwa mkuu wetu,” alisema mzee Hamadi.
“Umesemaje?”
“Hapa ndipo kwa mkuu wetu, chochote nitakachofanya, fanya,” alisema mzee Hamadi.
“Sawa mkuu.”
Mzee Hamisi alionekana kutokujiamini, hata hatua zake zikaanza kubadilika mahali pale, hakuamini kama katika maisha yake angeweza kumuona shetani ambaye kila siku alimuabudu kwa vitu vya kishirikina alivyokuwa akivifanya.
Kabla ya kumuona shetani, kulikuwa na mageti saba ambayo ulitakiwa kuvuka. Naomba niseme kitu kwamba hata naye shetani alijifanya Mungu. Kama ambavyo watu wanaposema kulikuwa na mbingu saba mpaka kufika kwa Mungu basi naye shetani alijiwekea mipaka kwamba ulitakiwa uvuke mageti saba ndiyo umfikie yeye.
Geti la kwanza kabisa ambalo walikutana nalo kulikuwa na mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa mzee sana, alitia huruma kwa kumwangalia tu, ni kama alikuwa akihitaji msaada wa fedha.
Alionekana kuwa na uhitaji mkubwa sana, mzee Hamisi na Hamadi walipofika getini hapo na kumwangalia mwanamke yule, walimuonea huruma sana, hasa mzee Hamisi ambaye hakutarajia kukutana na mwanamke aliyekuwa akitia huruma kama yule.
Huyo ndiye aliyekuwa ufunguo wa kuingilia geti la kwanza kabisa, ili uweze kuvuka hapo ulitakiwa kumuua tu. Haukutakiwa kumuonea huruma, ili uweze kupita kwa urahisi ilikuwa ni lazima kumuua.
Wengi waliotaka kwenda huko walishindwa mahali hapo. Kwa jinsi mwanamke yule alivyotia huruma, lilikuwa jambo gumu sana kumuua. Pembeni mwa mwanamke yule kulikuwa na panga moja kubwa lenye makali pande zote mbili.
“Huyu mwanamke anafanya nini hapa?” aliuliza mzee Hamisi.
“Amekaa tu.”
“Kwa nini aondoki?”
“Hawezi kuondoka kwani yeye ndiye ufunguo wa kusonga mbele,” alijibu mzee Hamadi.
“Unamaanisha nini?”
“Unatakiwa umuue ili uvuke geti la kwanza.”
“Nimuue huyu mwanamke?”
“Ndiyo!”
“Acha utani!”
“Basi turudi.”
“Turudi kabla ya kufanya kilichotuleta?”
“Sasa tutafikaje kama hutaki tuchukue ufunguo.”
“Kwa maana hiyo mwanamke huyu ndiye ufunguo?”
“Haswaaaa.”
Mzee Hamadi alivyoongea hivyo, mwanamke yule alizidi kutia huruma zaidi kiasi kwamba mzee Hamisi akajikuta akilengwa na machozi na baada ya sekunde chache machozi kuanza kumbubujika mashavuni mwake.
Ni kweli alikutana na ombaomba wengi mitaani lakini siku hiyo, mwanamke yule alitia huruma kuliko ombaomba wote aliowahi kukutana nao mitaani. Alimwangalia vizuri mwanamke yule, alijiona akishindwa kabisa kuchukua lile panga na kumuua.
“Basi turudi.”
“Ningependa niendelee mbele mpaka huko alipo lucifa,” alisema mzee Hamisi.
“Basi fanya kama nilivyokwambia,” alisema mzee Hamadi.
Mzee Hamisi hakujua afanye nini kwani kila alipomwangalia mwanamke yule, alizidi kutia huruma mno.

Je,nini kitaendelea?
Je, watamuona shetani?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.