RAPHAEL MTAMBO WA MABAO, YANGA WAMWAMINI ILA LAZIMA ATANUE MOYO WAKE
UTAKUWA umesikia mengi kuhusiana na Raphael Daud ingawa niliwahi kumuita kwa jina la Raphael Alpha kwa kipindi kirefu kabisa.
Baadaye
niliambiwa jina lake sahihi ni Raphael Alpha. Jina lake lilibadilishwa
baada ya kutokea makosa wakati wa usajili wa leseni katika Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF).
Raphael
Alpha hadi leo ni mchezaji kinda katika kikosi cha vijana cha Mbeya
City. Raphael John yeye alikuwa katika kikosi cha wakubwa lakini majina
yao yakachanganywa naye akalazimika kutumia jina hilo ili acheze ligi
hadi liliporekebishwa.
Leo
ninamzungumzia Raphael Daud kamili, kiungo ambaye alianza kuichezea
Mbeya City katika msimu wa 2014-15. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake
rahisi kwake baada ya kukaa benchi mzunguko wote wa kwanza, kocha akiwa
ni Juma Mwambusi.
Mechi
ya kirafiki dhidi ya Majimaji ikiivaa Mbeya City, Raphael alikuwa
katika benchi tena. Bahati mbaya mkongwe Steven Mazanda aliumia, akaenda
benchi na bahati nzuri kwa Raphael akaingia kuchukua namba.
Baada
ya mechi hiyo kwisha, kocha Mwambusi alichukua uamuzi wa kumrudisha
Mazanda kucheza namba sita na moja kwa moja akamkabidhi Raphael dimba la
juu.
Mzunguko wa pili wa ligi, alicheza mechi zote 15 za mzunguko wa pili na kufanikiwa kufunga mabao manne.
Msimu
uliofuata yaani wa 2015/16 alicheza mechi zote 25 akiwa fiti na kufunga
mabao sita. Kama hiyo haitoshi, msimu uliofuata au uliopita, Raphael
akaichezea Mbeya City mechi 27, akikosa tatu tu na kufunga mabao nane.
Kwa
taarifa yako, ingawa ni kiungo mchezeshaji hadi sasa tokea Mbeya City
imeingia Ligi Kuu Bara ndiye mfungaji bora, akiwa amefunga mabao 18 na
kufuatiwa na Patrick Mangungulu mwenye bao 17.
Kwa
rekodi chache nilizokupa, nataka kukuthibitishia kuwa kati ya usajili
bora kabisa walioufanya Yanga msimu huu, basi Raphael ni mmoja wao na
kama ni moja ya chaguo sahihi amelifanya kiungo huyo basi ni kujiunga na
Yanga, nitakuambia kwa nini.
Yanga
imeondokewa na Niyonzima ambaye ilimtegemea kama kiungo mchezeshaji.
Huenda ilipanga kumtumia Thabani Kamusoko, kama ikimalizana na Papy
Tshishimbi raia wa DR Congo kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.
Bado
naona itakuwa kosa kubwa kama Kocha George Lwandamina hatamuamini
kiungo huyo kinda ambaye kwa misimu mitatu mfululizo hajakosa hata mechi
sita.
Lwandamina
ni kocha mtaalamu sote tunajua, lakini nimeona makocha wengi wangependa
kuchagua wachezaji wa nje zaidi kwa ile imani mchezaji wa kimataifa
hapaswi kukaa benchi.
Vizuri
ampe nafasi na asimbeze au kuona umri wake bado ni mdogo. Ninaamini
atakuwa na msaada ingawa Raphael atakuwa na kazi ya kumshawishi kocha
kama kweli atakuwa msaada kwake.
Kama
Lwandamina angeniambia nimpangie kikosi, basi ningempa hiki kifuatacho.
1. Youthe Rostand 2. Juma Abdul 3. Haji Mwinyi 3. Kelvin Yondani 5.
Nadir Haroub 6. Papy Kambamba 7. Obrey Chirwa 8. Raphael Daud 9. Donald
Ngoma 10. Ibrahim Ajibu 11. Thabani Kamusoko.
Mchezaji
ambaye amekuwa na kiwango cha juu, nidhamu ya kuvutia na mshindani
sahihi ambaye lazima kukubali kumpa muda hata kidogo kwa kuwa anakwenda
katika timu kubwa yenye presha ya juu zaidi.
Huenda
akawa ana nafasi ya kujifunza na kupata nafasi kwa kuwa Mbeya City kwa
kuwa ni timu ya mashabiki wengi na wanachama, presha yake inaweza kuwa
imemsaidia kidogo kwenda kuungana na presha ya Yanga.
Kwake
Raphael nataka kumpa moyo kwa kuwa namuona ni hazina kubwa ya taifa
letu baadaye. Namuona ana sura ya wachezaji wenye nafasi ya kucheza nje
ya Tanzania na kuitangaza Yanga na nchi yetu pia kuwa msaada katika timu
yetu ya taifa.
Huenda
anaweza kushindwa kidogo wakati akijifunza kadhaa, lakini ana nafasi
kubwa ya kufanya vizuri zaidi na zaidi kutokana na mwenendo wake. Huenda
jambo jema zaidi itakuwa ni kujilinda na “madudu” ya Jiji la Dar es
Salaam kwa kuwa tumeona wengi wakitokea timu za mikoani na nidhamu zao,
lakini wakifika Dar es Salaam na kujiunga na timu kubwa au maarufu,
tunaanza kuona wanabadilika na hawashikiki tena kwa muonekano wa usiku
katika kumbi za starehe.
Kama
kweli Raphael anataka mpira, basi ninaamini ataweza na hakuna wa
kumzuia kufika mbali. Kama anataka mengine, Dar es Salaam yanapatikana
kirahisi zaidi na suala la kuchagua linaendelea kubaki ndani ya moyo na
ubongo wake.
Na Saleh Ally
Post a Comment