KENYA Wapinzani: Serikali Ikubali Wachunguzi wa Nje Mauaji ya Msando
MUUNGANO wa upinzani nchini Kenya (NASA) umekubali nia ya serikali za Marekani na Uingereza kusaidia kuchunguza mauaji ya ofisa wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nchini humo, Chris Msando.
Mwili wa Msando ulikutwa chumba cha maiti cha jijini Nairobi jana siku moja baada ya kuripotiwa alikuwa amepotea. “Msimamo wetu ni serikali kukubaliana na Marekani na Uingereza kusaidia kuchunguza mauaji ya Chris Msando.
Tumefarijika kuona washirika wetu kuja kutusaidia katika suala hilo licha ya Mwanasheria Mkuu, Githu Muigai; Makamu wa Rais, William Ruto na Rais Uhuru Kenyatta kukaa kimya,” alisema Musalia Mudavadi wa NASA.
Marekani na Uingereza jana zilikubali kutoa maofisa wao wawili wa ngazi za juu kutoka mashirika ya upelelezi ya FBI na Scotland Yard baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Keriako Tobiko kutaka uchunguzi ufanywe kuhusu mauaji ya Msando. Aliitaka pia serikali kuhakikisha usalama wa maofisa wa IEBC ili uchaguzi ufanyike kwa usalama.
Polisi walisema mwili wa Msando uligunduliwa katika msitu wa Kikuyu na kumbukumbu za mochwari zinaonyesha kwamba ulipelekwa hapo Jumapili asubuhi pamoja na mwili wa mwanamke mmoja asiyefahamika uliopatikana sehemu hiyohiyo.
Marehemu Msando ameelezewa na marafiki zake kuwa mwalidifu na mcheshi, ambapo wafanyakazi wenzake katika IEBC wakiwemo Andrew Limo, Tabitha Mutemi na Ronnel Onchagwa wakisema alikuwa na utaalam mkubwa wa teknolojia, mwadilifu na mcheshi. Kabla ya kupatikana kwake, gari lake lilikutwa likiwa halina mtu eneo la Roysambu, Nairobi.
Post a Comment