Vodacom Kuzipa Timu Za Ligi Kuu Vifaa Mbalimbali Wiki Hii
Timu
zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara(VPL), zinatarajiwa
kukabidhiwa vifaa mbalimbali wiki hii na mdhamini mkuu wa ligi hiyo
Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC, vyenye thamani ya zaidi
ya shilingi milioni 500/= .
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Meneja Uhusiano wa Vodacom
Tanzania PLC, Matina Nkurlu, alisema kuwa wameamua kutoa vifaa mapema
ili waweze kuzipa muda wa kutosha timu zitakazoshiriki VPL inayotarajiwa
kuanza Agosti 26, mwaka huu, ikiwa ni baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii
utakaopigwa Agosti 23.
Alisema
kwa mara nyingine katika kuhakikisha ligi ya soka nchini inaenda
vizuri, kampuni yao inakabidhi vifaa mbalimbali vya ligi ili kuwezesha
ushiriki wa timu katika msimu huu utakaoanza mwezi ujao bila
kipingamizi.
Alivitaja
vifaa vitakavyokabidhiwa kuwa ni jezi za mechi na mazoezi, viatu vya
mechi na mazoezi, soksi, vilinda ugoko, glovu, ‘bibs’, pampu’, kitambaa
cha nahodha, jezi na viatu vya waamuzi, sare za waokota mipira, mabegi
ya kusafiria na vinginevyo vinavyozihusu timu, waamuzi na mchezo kwa
ujumla.
“Tunajisikia
furaha kwani vifaa vipo tayari na tutavikabidhi rasmi wiki hii tukiwa
tunatekeleza matakwa ya mkataba wa udhamini, ni imani yetu kwamba timu
zitakazoshiriki ligi zimejiandaa vya kutosha kwa msimu mpya wa ligi wa
2017/2018,” alisema Nkurlu.
Aliongeza:
“Vodacom Tanzania inaendelea kudhamini ligi kuu kwasababu soka ni
mchezo unaopendwa sana hapa Tanzania na duniani kote kwa ujumla, ukiwa
na washabiki wengi, hivyo tunapenda kuona wananchi ambao baadhi yao ni
wateja wetu, wanapata burudani ya mchezo waupendao, ukizingatia michezo
ni ajira kubwa duniani, ikiendelezwa inaweza kubadilisha maisha ya watu
wengi na taifa kunufaika kwa mapato makubwa ya kodi kutoka katika sekta
hiyo.”
Aliwataka
wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi ya Tanzania na
kuongeza maslahi kwa wachezaji wanaoshiriki ligi hiyo ambayo
itashirikisha timu 16, zikiwamo tatu zilizopanda msimu huu.
“Tukiunganisha
nguvu timu zetu zinaweza kuwa na wachezaji wa kimataifa na kufuata
nyayo za Mtanzania Mbwana Samatta anayeipeperusha Bendera ya Tanzania
huko Ulaya katika klabu ya Genk ya Ubelgiji. Ni muhimu kwa wadau
mbalimbali kuanza kuwekeza katika timu za vijana chipukizi kwa kuwa
vipaji vinaanzia ngazi ya chini,” alisema Nkurlu.
Yanga
ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ambapo msimu huu inatarajiwa kutetea
ubingwa wake, huku ikitarajiwa kupata changamoto ya aina yake kutoka
kwa timu nyingine 15, wakiwamo watani wao wa jadi, Simba.
Mbali
ya wakongwe hao wa soka nchini, timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo
msimu huu ni Azam FC, Singida United, Kagera Sugar, Mbeya City, Njombe
Mji, Mtibwa Sugar, Ndanda FC, Mbao FC, Tanzania Prisons, Majimaji,
Mwadui, Ruvu Shooting, Lipuli na Stand United.
Post a Comment