TCRA yapiga marufuku matangazo kwenye miito ya simu
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepiga marufuku matangazo ya biashara
yanayowekwa mtumiaji anapopiga simu ili kutoa fursa kwa watumiaji kupata
mawasiliano bila usumbufu.
Mkurugenzi
wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema jana (Ijumaa) kuwa mamlaka hiyo
imepokea malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa simu wakilalamikia
matangazo hayo yanayotolewa na kampuni za simu.
Amesema
tayari TCRA imeshaziandikia barua kampuni zote za simu kusitisha
matangazo hayo na itakutana nazo kwa majadiliano ya kina Julai 6.
Amesema
mamlaka haitambui utaratibu huo na inauchukulia kama kero kwa watumiaji
wa simu ambao hutegemea kutumia njia hiyo ya mawasiliano kurahisisha
mambo.
“Tuna
imani mtu anapopiga simu ana shida ya haraka na anahitaji afanye
mawasiliano, unapomuwekea matangazo kwa dakika tatu au nne ni usumbufu,” amesema.
Katika
siku za karibuni imekuwa ni kawaida kwa mtu anayepiga simu kusikiliza
wimbo au matangazo ya biashara na baadaye kuambiwa namba anayopiga
haipatikani.
Post a Comment