ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-07


 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
Mwanamke yule ambaye watoto wake walikuwa ndani ya nyumba ile akaanza kulia, tayari alikwishajua kile kilichokuwa kimetokea ndani ya nyumba ile kwamba watoto wake walikuwa wamenasa na hivyo ilimaanisha kwamba wangekutwa asubuhi au wangekufa usiku huohuo.
Hilo likamkosesha amani, akajaribu kuwaambia wenzake kwamba walitakiwa kuelekea ndani kwa ajili ya kuwanasua lakini kila mmoja akaonekana kuogopa kwani Ramadhani hakuonekana kuwa mtu wa kutania.
Walijaribu kukaa pale huku wakifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya kwani nao muda haukuwasubiri, uliendelea kusonga mbele jambo lililowafanya kuwa na wasiwasi zaidi.
“Tuingieni....” alisema mwanamke yule mwenye watoto wake.
“Hapana! Hatuwezi kuingia, huyu mtu anaonekana kuwa hatari,” alijibu kiongozi.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, Ramadhani hakuonekana kuwa mtu wa masihara, kila mtu aliogopa kuingia ndani. Mwanamke yule alibaki akilia lakini kilio chake hakikubadilisha matokeo yoyote yale, watoto wake walinaswa ndani.
Siku iliyofuata, taarifa zikaanza kusambaa kwamba watoto wa mwanamke yule hawakuamka kitandani, walikuwa wamefariki dunia. Kilikuwa kifo cha kushtukiza sana, hakukuwa na mtu aliyejua kama kulikuwa na ushirikina kati yao na ndiyo kitu kilichopelekea kufa kwani walikwenda kumroga mtu aliyekuwa na nguvu zaidi yao.
Watu wakaanza kukusanyika msibani pale, wachawi waliofika mahali hapo wakaanza kuangaliana kwa macho ya mashaka kwani walijua kile kilichokuwa kimetokea kwamba watoto hawakufa duniani bali walichukuliwa misukule na Ramadhani.
“Hivi watu wanaweza kugundua kweli?” aliuliza mzee mmoja, alikuwa na upara kichwani, alivalia msuli mrefu.
“Hawawezi kujua, tusubiri tukazike tu.”
Ingawa wale waliokuwa wakiosha maiti walijua kwamba zile zilikuwa maiti lakini ukweli ulikuwa ni kwamba hawakuwa wakiosha maiti kama walivyoona bali ilikuwa ni migomba.
Wakati jeneza likiwa limeletwa nje tayari kwa kuswaliwa na maziko, ghafla mwanaume mmoja akaanza kuja kwa kasi msibani pale, alionekana kuwa na jambo la muhimu sana alitaka kuwaambia, alipowafikia, akaanza kumwangalia kila mtu aliyekuwa mahali pale, mwanaume yule hakuwa mwingine bali alikuwa Ramadhani.
Macho yake yalikuwa ya chuki mno, kila alipowaangalia wachawi wale, alikuwa akikunja uso wake huku akisonya kwa hasira kitendo kilichotafsiriwa kuwa dharau na hakikutakiwa kuonyeshwa msibani pale.
“Hebu nyie wachawi inukeni muwaambie wenzenu ukweli,” alisema Ramdahani kwa dharau kubwa.
Hakukuwa na mtu aliyesimama, hata mama yao na marehemu ambaye alijifanyisha kulia, akanyamaza na kuona kwamba tayari walikuwa wakienda kuumbuka. Mtu aliyekuwa akiongoza mazishi yale, shekhe mmoja aliyeonekana kuwa na heshima kubwa akamwangalia Ramadhani na kumwambia aondoke.
“Shekhe, hamuendi kuzika maiti, mnakwenda kuzika migomba,” alisema Ramadhani, watu wote wakashtuka.
“Unasemaje?” shekhe aliuliza kwa mshtuko.
“Hao watoto wapo nyumbani, nimewahifadhi,” alisema Ramdhani maneno yaliyomshtua kila mtu mahali pale.
“Wewe kijana hebu tuondolee uchizi.”
“Kama mnaniona chizi, angalieni maiti hizo,” alisema Ramdhani.
Walichokifanya mashekhe wawili ni kusimama na kuyafuata majeneza yale yaliyokuwa na maiti zilizofungwa mikekani kwa lengo za kuzifungua. Kila mtu msibani pale alibaki kimya, alitaka kushuhudia kile kilichozungumzwa na kijana yule.
Wale watu walikuwa mbali, wakasogea karibu, walitaka kuona kama kweli mule hakukuwa na maiti kama walivyojua au Ramadhani alikuwa akiwadanganya. Wachawi wale ambao walikuwa wamekwenda kuroga nyumbani kwake, wakaanza kuondoka kwa kujifichajificha kwani tayari walijua kwamba mambo yaliharibika.
Mashekhe wale walipoyafikia majeneza yale, wakazitoa maiti zile kutoka ndani na kuziweka mkekani, watu wakakodoa macho zaidi kwa kutaka kushuhudia kile kilichokuwa ndani ya mikeka ile.
Kwa kuwa hawakuwa na uhakika na hawakutaka kumuamini sana Ramadhani, wakaanza kuchungulia wao wenyewe kuona kama kulikuwa na maiti au migomba kama alivyosema Ramadhani.
“Mtumeee! Migomba! “ alisema shekhe mmoja na hivyo kufungua mikeka ile.
Watu wakapigwa na bumbuwazi, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, ndani ya mikeka ile hakukuwa na maiti yoyote ile zaidi ya migomba miwili ambayo wao ndiyo walitakiwa kwenda kuizika.
Mama wa marehemu akaanza kulia kwa uchungu, hakulia kwa kuwa watoto wake walikuwa wamefichwa ila alilia kwa kuwa alijua fika kwamba huo ulikuwa wakati wa kuumbuliwa.
“Hawa watoto walikuja kuroga nyumbani kwangu usiku,” alisema Ramadhani na kuendelea:
“Nilichokifanya ni kuwasimamisha na ndiyo maana mnaona kwamba wamekufa lakini ukweli ni kwamba hawajafa bali walikuja kuroga nyumbani kwangu,” alisema Ramdhani,
Minong’ono ikaanza kuibuka msibani hapo, kila mtu aliyeyasikia maneno yale alipigwa na butwaa, watu ambao hawakuamini kama uchawi ulikuwepo, hapo wakaamuni kwa asilimia mia moja,.
“Huyu mama yao alikuja nao akiwa na wenzake, wakawaacha na kuwasakizia waingie ndani na wakati wanajua kwamba hawakuwa na uwezo wa kuroga,” alisema Ramadhani, watu wote wakamwangalia mwanamke yule, kilio cha unafiki kikakata, akainama chini kwa aibu.
“Sikutaka kuwaua mabinti hawa kwa kuwa hawajui chochote kile, waliingia kwa kushinikizwa tu. Twendeni mkawachukue,” alisema Ramadhni na kuanza kuondoka mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyetaka kubaki, wote wakaanza kumfuata Ramdahani ambaye alikuwa akitembea kwa mikogo mikubwa. Mkononi alishika hirizi kubwa nyekundu, alitembea kwa hatua ndefundefu ila kwa mwendo wa taratibu.
Walipofika nyumbani, akawaambia watu wale wasubiri na kisha kupulizia dawa fulani na kuwaita wasichana wale ambapo mlango ukafunguliwa na wasichana hao kutoka wakiwa kama walivyozaliwa, huku wakiwa wanatisha kwani bado walikuwa kwenye hali ya kichawi. Watu waliotangulizana na Ramadhani walipowaona wasichana wale, wakaanza kukimbia kwa hofu.
*****
Kwa muonekano, walitisha mno, hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kubaki mahali hapo na kuwaangalia mabinti wale, walikuwa na muonekano wa kichawi ambao ulizidi kuwaogopesha watu zaidi.
Alichokifanya Ramadhani ni kuwaweka chini kisha kuwapaka unga fulani, ulikuwa ni wa njano, aliyapaka macho yao na miguu yao, baada ya kufanya hivyo, akaanza kuiongea maneno yasiyoeleweka na hapohapo mabinti wale wakarudi katika hali ya kawaida.
Kwanza walishangaa walikuwa wapi, kwa mbali mbele yao kulikuwa na umati wa watu ukiwashangaa, walipojitazama, wakagundua kwamba walikuwa watupu jambo lililowafanya kuanza kuziziba sehemu zao za siri kwa kutumia viganja vya mikono yao.
Pasipo kutegemea, mabinti wale wakaanza kulia. Kwao iliwauma sana kuwa katika mazingira hayo, hawakuwa wakikumbuka kile kilichowafanya kuwa mahali hapo lakini baada ya kumuona Ramadhani, wakakumbuka kila kitu.
“Wachukueni muwapeleke kwao,” alisema Ramadhani, walichokifanya wanaume wenye moyo wa chuma ni kuwachukua na kuwapeleka nyumbani kwao huku kundi kubwa la watu likiwafuatilia kwa nyuma.
“Hao wachawi hao, waangalie wanavyotisha, kama vinyago.”
“Hao, watoto wadogo wanajifunza uchawi.”
Zilikuwa kelele kutoka kwa watu waliokuwa wakiwatazama mabinti wale. Walikuwa wasichana warembo wa sura waliokuwa na mamumbo mazuri lakini kitendo chao cha kujihusisha na uchawi kiliwashtua watu.
Walitembea kwa aibu mpaka walipofika nyumbani kwao na kuingia ndani, kwa kipindi cha wiki nzima, hawakutaka kutoka ndani kwani walikuwa wakijisikia aibu mno.
****
Nilimuona mzee Hamisi akiwa amechanganyikiwa, kile kilichokuwa kimetokea, kilimuuma sana. Alipagawa kwani aligundua kwamba Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo na ndiyo maana hata pale kwenye mikwara, na yeye alikuwa na moyo wa kumpiga mikwara kwamba angeweza kumuua.
Hakutaka kukaa jijini Dar es Salaam, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea Bagamoyo. Hapa subiri nikwambie kitu kimoja kwamba mchawi yeyote anapoona kwamba ameshindwa sehemu fulani, huwa hataki kukubali bali anachokifanya ni kutafuta hata msaada wa watu wengine kuhakikisha kwamba anafanikiwa mpaka kutimiza kile alichokuwa akikihitaji.
Huko Bagamoyo alikuwa akimfuata mzee mwingine ambaye alionekana kuwa nuksi sana, mzee ambaye alikuwa akimuaminia kwa kuwa na uchawi wenye nguvu, alipofika huko, akaenda kuonana na mzee huyo kisha kuanza kuzungumza naye.
“Anatumia uchawi wa wapi?” aliuliza mzee huyo, aliitwa mzee Maliki, alijulikana Bagamoyo nzima kwa uchawi.
“Wa Kanda ya Magharibi!”
“Kutoka Kigoma?”
“Ndiyo!”
“Daah! Hapo kuna kazi kubwa, ila tutafanikiwa.”
Wachawi walikuwa wamegawanyika, walikuwa wale kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi na Kanda nyingine nyingi. Kwenye kila kanda, kulikuwa na nguvu yake lakini wachawi wengi waliogopa uchawi kutoka Kanda ya Magharibi.
Huko Kigoma, asilimia kubwa ya uchawi wao ulikuwa ukichanganyikana na ule kutoka Kongo ambao ulijulikana kwa kuwa mkubwa na wenye nguvu kuliko ule wa Tanzania. Watanzania wengi walikuwa wakiuogopa uchawi huo na ndiyo maana mzee Hamisi aliposema kwamba uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani ulitoka Kanda ya Magharibi, mzee Maliki akaogopa.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kwangu sidhani kama nitaweza ila kama utahitaji sana, kesho tuelekee Tanga, kuna mtu ambaye anaweza akatusaidia,” alisema mzee Maliki.
“Sawa hakuna tatizo.”
Mzee Hamisi hakutaka kurudi Dar es Salaam, alichokifanya ni kusubiri hukohuko Bagamoyo ili kujiandaa na safari ya kwenda Tanga kwa mtu mwingine ambaye aliambiwa kwamba alikuwa na nguvu kubwa mno.
Usiku hakulala kwa raha, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Ramadhani aliyeonekana kuutetemesha ufalme wake. Alimchukia kijana huyo na alitaka kuhakikisha kwamba kila kitu atakachokifanya basi mwisho wa siku kijana huyo afe.
Asubuhi ilipofika, wakaamka na safari ya kuelekea Tanga kuanza. Kuna kitu huwa kinashangaza sana, unaweza kumkuta mchawi akiwa bize na mambo yake, tena ya msingi kabisa lakini linapokuja suala la kuroga, yaani yupo radhi aache mambo yake yote lakini mwisho wa siku afanye kile anachotakiwa kukipata.
Si kwamba mzee Maliki hakuwa bize na mambo yake, alikuwa bize mno lakini alipoambiwa suala la kutaka kumroga mtu fulani, mambo yake yote akayaacha pembeni na kutaka kufanya kile alichokuwa amewambiwa, yaani alikuwa akihusudu uchawi kuliko kitu chochote kile.
Baada ya sa moja wakawa ndani ya basi wakielekea Tanga. Walikuwa wakipiga stori tu njiani huku kila mmoja akionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. Basi lilipofika Segera, njia panda ya kwenda Moshi na Tanga, likasimama.
Kila mmoja akahisi kwamba inawezekana kuna abiria alikuwa akishuka au wengine wakiingia lakini kitu cha ajabu, basi likasimama kwa muda mrefu sana lakini dereva hakuliondoa jambo lililowakera abiria.
“Dereva unazingua, hakuna abiria anayepanda, sasa tunasubiri nini hapa? Au tunamsubiri mkeo?” aliuliza abiria mmoja, kwa muoenakano wake tu ulionyesha alikuwa kisirani.
“Gari haiondoki!” alijibu dereva.
“Haiondoki au haiwaki?”
“Kuwaka imewaka, wala sikuzima, ila kuondoka haiondoki, sijui tatizo nini,” alisema dereva yule.
Maneno ya dereva yule yalimshangaza kila mmoja, hakukuwa na aliyeamini kama kweli daladala lilishindwa kuondoka na wakati ilikuwa imewaka. Alichokifanya abiria mmoja aliyeonekana kuwa mtaalamu wa magari akasimama na kuelekea kule kwa derea ambaye akampisha na yeye kukalia kiti, akajaribu kukanyaga mafuta ili waondoke, gari haikuondoka.
“Mmmh!”
“Imekuwaje?”
“Ndiyo kwanza naona leo, imekuwaje gari haiondoki?” aliuliza dereva.
Minonong’ono ikaanza kusikika ndani ya basi lile, hakukuwa na mtu aliyejua kwamba kile kilichokuwa kikiendelea kilikuwa katika utawala wa nguvu za giza hivyo kwa akili ya kibinadamu jambo hilo lisingewezekana kabisa.
Mzee Hamisi na Maliki hawakuelewa chochote kile, ila waliposikia kwamba hali hiyo haikuwa ya kawaida kutokea duniani kwamba gari liwake lakini lishindwe kuondoka, wakaanza kuelekea kwa dereva ambaye bado alikuwa kwenye sintofahamu.
“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Hata kabla dereva hajajibu swali hilo, ghafla wingu kubwa likaanza kujikusanya, ndani ya sekunde kumi tu, tayari jua halikuonekana, hapohapo mvua kubwa ikaanza kuinyesha huku ikiambatana na radi kali iliyowafanya watu wote kuogopa.
“Mmmh!” aliguna mzee Maliki.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.