ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-06


 
NYEMO CHILONGANI

ILIPOISHIA
Kwa kuwa walikuwa wakiongea kwa sauti kubwa, watu waliokuwa pembeni waliposikia wakaanza kusogea kule walipokuwa wale watu na hatimaye vita vya maneno kuanza kuzuka mahali hapo, kila mtu aliyekuwa akimwambia mwenzake, walipeana vitisho vya kuua tu pasipo kujua tatizo lolote lile. Ghafla mzee yule akazidi kupandwa na hasira, nikajua kuna kitu kingetokea mahali hapo.
ENDELEA NAYO..

Watu walizidi kukusanyika mahali pale wakiwasikiliza watu hao waliokuwa wakipeana vitisho kwamba yeyote angeweza kumuua mwenzake. Hakukuwa na mtu aliyeingilia, labda kwa sababu wengi waliyafahamu maisha ya huyu mzee huyu aliyeitwa Hamisi tena huku wengine wakimsonta kidole kijana yule aachane naye lakini hakutaka kuacha, aliendelea kumwambia kwamba angeweza kumuua.
“Kijana anatafuta balaa, huyu mgeni nini?” aliuliza mzee mmoja.
“Si mgeni, ni mwenyeji kabisa.”
“Sasa kwa nini anampiga mkwara huyu mzee, hamjui nini?”
“Anamjua sana, si unajua hivi visifa vya vijana wetu,” alisema mzee mwingine.
Mzee Hamisi hakutaka kuzungumza kitu, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kuingia ndani huku akiwa amefura kwa hasira. Kijana yule hakutaka kuondoka, alijiona kuwa bingwa na kuona mpinzani wake ameshindwa.
Alitukana na kutukana huku mikwara ikiendelea kusikika mdomoni mwake lakini mzee Hamisi hakurudi nje, aliendelea kubaki mulemule ndani kwake. Nakumbuka kijana yule alichukua zaidi ya dakika tano zaidi kutukana na kisha kuondoka.
Usiku ulipoingia, nikaanza kumuona mzee Hamisi akiwa kwenye mti mmoja mkubwa uliokuwa katikati ya uwanja mmoja mkubwa wa mpira. Mahali hapo alisimama peke yake na baada ya dakika kadhaa, kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliofika uwanjani hapo.
Kila mtu alikuwa mtupu, haikujalisha kama ni mtu mzima, mtoto au kijana, uwe mwanaume au mwanamke, unapokuwa hapo ulitakiwa kuwa mtupu. Niliwaona wanawake wawili wakiwa wamebeba chungu kimoja kikubwa na kukipeleka mbele kabisa kisha mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa mtu mzima kusogea karibu na kile chungu.
“Leo ni siku ya kuleta mahitaji yenu na kufanyiwa kazi,” alisema mwanamke yule, sauti yake ni kama ililazimishwa iwe ya kutisha.
Ngoja nikwambie kitu. Miongoni mwa mambo mengi niliyoambiwa na Yusnath ni kuhusu siku maalumu ambayo hutumika kwa ajili ya kupeleka mahitaji yao kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Wachawi hutenga siku maalumu kwa ajili ya kufanyia kazi matatizo yao.
Siku hiyo, kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akiwasumbua, labda kuna mtu ambaye hakuwa akirogeka kirahisi basi siku hiyo jina lake lingetumbukizwa ndani ya chungu kile na kisha kufanyiwa kazi.
Kama mtu huyo hakuwa na nguvu zozote zile basi angepata kile walichokuwa wakitaka akipate, labda ugonjwa wa kudumu na mambo mengine mabaya ambayo mchawi anataka mtu huyo ayapate.
Baada ya kuambiwa hivyo, nikamuona mzee Hamisi akisogea karibu na chungu kile kisha kusimama huku akiwaangalia wachawi wengine waliokusanyika uwanjani hapo. Alionekana kuwa na hasira, alikuwa kama mtu aliyepagawa hivi, kila mtu akabaki kimya akimsikiliza.
“Nimekasirishwa sana mkuu,” alisema mzee Hamisi huku akiwa ameyageuzia macho yake kwa mwanamke yule aliyeonekana kuwa kiongozi mahali hapo.
“Sema chochote kile, tutalifanyia kazi,” alisema kiongozi.
“Kuna kijana amenikera sana,” alisema mzee Hamisi.
“Unataka tumfanye nini?”
“Awe kichaa tu ili iwe fundisho kwa kila mtu mtaani,” alisema mzee Hamisi.
“Anaitwa nani?”
“Ramadhani.”
“Sawa. Ombi lako limekubaliwa. Weka jina lake katika chungu hicho.”
Alichokifanya mzee Hamisi ni kukiingiza kikaratasi kilichokuwa na jina la kijana yule, Ramadhani katika chungu kile kilichokuwa kikitoa moshi mkubwa kisha kwenda kusimama na wenzake.
Siku hiyo ilitumiwa vilivyo, kila mmoja alikuwa na kazi ya kuchukua kikaratasi kilichokuwa na jina la mtu aliyekuwa akitaka kumfanyia jambo na kukiweka katika chungu kile. Ndugu yangu, asikwambie mtu kwamba unapokuwa mchawi basi utakuwa na maisha yenye uhakika kwamba kila kitu utakachokitaka basi kitafanikiwa.
Kuna wachawi wanakutana na vitu vya kutisha mno, kuna wengine kazi zao zinashindwa na hivyo kujikuta wakikamatwa. Mchawi yeyote yule anayekamatwa kwa uzembe wake basi ni lazima apewe adhabu kule kuzimu.
Hii ndiyo sababu inayowafanya wengi kupeleka majina ya wabaya wao. Kulikuwa na watu wagumu kurogeka, kuna wengine wana kinga kali, mchawi anaposhindwa kumroga, basi huenda kwenye uwanja wao wa makutanio na kueleza kile kilichotokea.
Anachokifanya mchawi mkuu ni kuchukua lile jina na kuliweka kwenye kile chungu kisha kumpa mtu huyo nguvu na kurudi. Anaporudi, huwa na nguvu ya ziada, atakaposhindwa kwa mara nyingine, hapo ndipo wanapoongeza nguvu, yaani haendi mmoja, wanakwenda na wengine hata watano, wanaposhindwa hapo ndipo wanapotafuta njia nyingine.
Kuna wachawi wengine huwa wanakufa kazini, wengine wanapata misukosuko mingi, yote hiyo wanaita ajali kazini na mara nyingi hutokea kwani si kila mtu huwa rahisi kurogeka.
Mara baada ya mzee Hamisi kuliweka lile jina katika chungu kile, akawa na uhakika kwamba kile alichokuwa akikitaka ni lazima kingefanyika tu kwani aliamini kwamba kijana yule hakuwa na nguvu kubwa, hata kama alijiamini kwa kumpiga mikwara, bado alijiona kuweza kumfanya kijana yule kuwa kichaa.
Uchawi ukatumwa!
*****
Niliuona uchawi ukianza safari kumfuata kijana yule aliyeitwa kwa jina la Ramadhani ili uweze kumdhuru na kuwa kichaa. Katika upande wa pili nilimuona Ramadhani akiwa amekaa chumbani kwake, alionekana kuwa na mawazo mno, alionekana kama mtu aliyekata tamaa kwa jambo fulani.
Nikauona ule uchawi unaingia ndani. Ndugu yangu, huwezi kuuona huu uchawi kama hauna nguvu fulani. Sikuwa kwenye ulimwengu wa kibinadamu bali nilikuwa kwenye ulimwengu wa kijini. Ule uchawi ulipofika mlangoni, ukaingia ndani kwa ajili ya kumvaa kijana yule.
Sikujua nini kilitokea, nilimuona Ramadhani akishtuka, akasimama harakaharaka na kukunja ngumi mikono yake, kitu cha kushangaza, uchawi ule nao ukasimama. Sijajua kama Ramadhani alikuwa akiuona au la, alichokifanya ni kufungua droo yake ndogo ya kitanda na kuchukua kikaratasi kimoja kilichoandikwa maneno mengi kwa Lugha ya Kiarabu na kisha kuanza kukisoma kwa harakaharaka.
Ule uchawi ukamfuata na kumvamia, nikasikia sauti kubwa ya radi ikipiga, ule uchawi nikauona ukishindwa kumuingia na hapohapo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Mmmh!” nilijikuta nikiguna.”
Usiku huohuo nikauona uchawi ule ukirudi mpaka kule ulipotumwa. Hakukuwa na hali ya kawaida, kila mtu alipouona ukija, akakimbia mahali pale na kusimama pembeni kabisa ya uwanja ule, ule uchawi, kutokana na nguvu kubwa iliyokuwa nao, ukakivunja kile chungu hivyo wachawi wote kujua kwamba ule uchawi ulikuwa umeshindwa.
“Ni lazima tuungane, mtu mmoja hawezi kututisha,” nilimsikia mzee mmoja akizungumza maneno hayo, alikuwa mbali kabisa na aliogopa kusogea kule kilipokuwa chungu kile.
Baada ya dakika tano tena walipoona hali imetulia, walichokifanya ni kusogea mpaka pale kulipokuwa na chungu kile kilichokuwa kimevunjika na kuanza kuangalia kwa ndani, hakukuwa na kitu chochote zaidi ya manyoya ya kuku tu.
Kila mmoja akashangaa, japokuwa walijua kwamba kulikuwa na wakati wachawi walikuwa wakishindwa kufanya jambo fulani, lakini kwao hawakuwahi kushindwa hata mara moja, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza.
Mzee Hamisi alikosa la kuongea, kila wakati alikuwa ameuachamisha mdomo wake, hakuonekana kuamini juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Kijana yule, Ramadhani alionekana kuwa na nguvu mno na hakuwa mtu wa kumchezea hata mara moja, alikuwa mwenye uwezo mkubwa kichawi hivyo hata kama kufuatwa, alitakiwa kufuatwa kimakini zaidi.
“Haiwezekani! Haiwezekani!” nilimsikia mzee Hamisi akisema kwa sauti kubwa.
“Huyu mtu ana kinga kubwa sana,” alisema kiongozi wao.
“Tufanye nini? Tuongeze nguvu kumfuata?” aliuliza mchawi mwingine.
“Hatuwezi kwenda kwa kukurupuka, ni lazima tujipange, vinginevyo tutaumbuka,” alisema kiongozi yule.
Hapohapo wakapangwa watu waliotakiwa kwenda kwa Ramadhani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kijana yule anamalizwa haraka iwezekanavyo kwani waliamini kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa na uchawi mkubwa zaidi yao.
Wachawi wengine waliochaguliwa kwa ajili ya kwenda huko, walionekana kuwa na wasiwasi mno, hawakupenda kwenda kwa kuwa walijua kwamba kazi huwa ngumu sana na hivyo wanaweza kushindwa na hata mwisho wa siku kukamatwa.
“Nitawapeni maelekezo juu ya nini cha kufanya,” alisema kiongozi yule na kuanza kuwapa maelekezo.
Hakuchukua muda mrefu kuwaelekeza nini cha kufanya, baada ya kumaliza, akawapa unga fulani na kuwataka kujipaka nyusoni mwao kisha kupotea, ghafla nikawaona wakiwa juu ya nyungo zao huku kiongozi wao akiwa mbele kabisa akiwaelekeza nini cha kufanya.
Nilikuwa nikiyaona yote, mzee Hamisi alikuwa ametulia kwenye ungo wake uliojaa tunguli nyingi, mkoni alikuwa ameshika usinga mmoja mkubwa na alikuwa akiupepea kila ungo wake ulipokwenda kwa umbali fulani.
Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamefika katika nyumba waliyotaka kuingia. Ilikuwa ni usiku sana, katika mtaa huo waliokuwepo, kulikuwa na watu wengine, hasa vijana ambao walikuwa wakinywa pombe na hata kucheza drafti lakini hakukuwa na yeyote aliyewaona mahali hapo.
“Nani anaanza kuingia?” aliuliza mchawi mmoja.
Kiongozi wao ndiye aliyekuwa akiamua ni nani wa kuingia na nani wa kubaki nje, alichokifanya ni kuwachagua wachawi wawili, walikuwa mabinti wadogo, kwa kuwaangalia kwa harakaharaka ungeweza kugundua kwamba walikuwa wakijifunza mambo ya kishirikina.
“Kwa nini waende wao?” aliuliza mwanamke mmoja, nahisi alikuwa mzazi wa watoto hao.
“Ni lazima wajifunze mengi, bila hivyo, hawatokua,” alijibu kiongozi.
Ngoja nikwambie kitu kimoja, kwenye suala zima la kuingia ndani ya nyumba ya mtu aliyeshindikana kichawi huwa linaogopwa sana, hakuna mtu anayependa kuingia humo kwani wengi wanaoingia hunaswa na mwisho wa siku kukutwa mpaka asubuhi wakiwa hapohapo wamenasa na mbaya zaidi, wakati mwingine hufariki dunia.
Kila mmoja aliogopa hivyo kuwasakizia wale mabinti ili waingie ndani. Mama yao alijua kwamba hiyo ilikuwa ni moja ya hatua kubwa na ngumu sana na ndiyo maana alilazimisha sana mabinti zake wasiingie ndani.
“Lakini ndiyo wanajifunza,” alisema mama yao.
“Hata kama! Ndiyo wajifunze jinsi ya kuroga watu kama hawa,” alisema kiongozi
Mwanamke yule hakuwa na jinsi, japokuwa alikuwa na mapenzi makubwa kwa mabinti zake lakini akakubaliana na kiongozi wake kwamba awaache mabinti zake waingie ndani kwa ajili ya kumroga Ramadhani.
Kilichofanyika ni kuupuruzia dawa mlango wa nyumba ile na pembe zote kisha mabinti wale wakaambiwa waingie ndani. Ghafla wakapotea na kuwaona wakiwa kwenye pembe moja ya nyumba ile na kuanza kuingia ndani.
Nilibaki kimya, nilikuwa nikifuatilia kila ktu tena kwa ukaribu, nilitaka kuona ni kitu gani kingetokea mahali hapo. Pale nje walipobaki, wale wachawi walikuwa wakiendelea kufanya mambo yao, walikuwa wakicheza utupu huku wakiendelea kupulizia unga fulani katika nyumba ile.
Huku kila mmoja akiwa bize, ghafla ukasikika uyowe mmoja mkubwa kutoka ndani. Kila mmoja akashtuka! Hawakujua nini kilitokea ndani.

Je, nini kiliendelea?

No comments

Powered by Blogger.