Jay amkumbuka mama yake ukumbini
Baada ya kufunga ndoa katika kanisa la St. Joseph jijini Dar es salaam
na mpenzi wake wa muda mrefu, Mbunge wa Mikumi na Mkongwe wa hip hop
bongo Joseph Haule 'Prof Jay' amesema ingawa ametimiza ndoto yake,
anasikitika mama yake hajaweza kushuhudia.
Prof Jay na mkewe Grace wakionyesha vyeti vyao baada ya kufunga ndoa.
"Namshukuru
Mungu kufikia siku ya leo ni ndoto niliyokuwa nayo muda mrefu. Hii ni
siku ya kipekee sana kwangu. Ningependa sana mama yangu awe shuhuda wa
tukio hili lakini nasikitika bahati mbaya alitangulia mbele ya haki
miaka minne iliyopita, naomba tuzidi kumuombea apumzike kwa amani" alisema Prof Jay
Aidha Prof Jay aliongeza kwamba furaha
aliyonayo ni kukamilisha ndoto zake kwa mpenzi wake huo ambaye tayari
walibahatika kupata mtoto wa kike na bado wakaendelea kudumu pamoja
kwenye mahusiano.
"Nimedumu na Grace kwa muda
mrefu sasa namshukuru Mungu kwa hii siku kutimia maana nilikuwa naiota
kila siku. Hata wimbo wa Kamili Gado ulikuwa maalumu kwake.....Mke wangu
ni mrembo sana yupo Kamili gado...." Prof Jay.
Mh. Joseph Mbilinyi ' Sugu' (kushoto) akiwa na maharusi
Kwa upande wa wahudhuriaji Mbunge wa Hai
na kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe alitoa
pongezi kwa Prof Jay huku akimuuita ni mbunge mjanja.
"Sisi tunakupongeza kwa
hatua nzuri uliyochukua, tunakutakia maisha mema wewe na familia yako.
Lakini unaona Wabunge wa vyama vyote wako hapa ni kwa sababu
wanakuthamini kwa kuwa na wewe unaheshima sana unyeyekevu japokuwa wewe
ni mbunge mjanja sana. Tunakutakia mafanikio katika Siasa yako, biashara
na sanaa" Mh. Mbowe.
Mjumbe wa kamati kuu Chadema na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akipunga Mkono ukumbini kwenye harusi ya Prof Jay.
Prof Jay aliungana katika tafrija ya
kusherehekea kuuaga ukapera jana usiku katika ukumbi wa Mlimani City
pamoja na Wabunge wenzake, Viongozi wa CHADEMA, Wasanii mbalimbali,
ndugu jamaa na marafiki pamoja na mashabiki zake.
Uongozi wa EATV LTD unampongeza Mh Joseph Haule kwa kupiga hatua nyingine katika maisha yake.
Post a Comment