ad

ad

AHSANTE NI NENO DOGO LAKINI, LINAMAANA KUBWA KATIKA MAPENZI

IJUMAA imewadia, siku nzuri ambayo mimi na wewe tunakutana kwenye ukurasa huu mzuri, kujuzana na kujadiliana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Hebu jaribu kukumbuka, mara ya mwisho kumshukuru mwenzi wako, iwe ni mkeo, mchumba au mpenzi wako ambaye mna ndoto za kuja kuishi pamoja kama mume ni mke ni lini? 

Leo nimeamua tujadiliane kuhusu mada hii kutokana na malalamiko mengi ninayoyapata kutoka kwa wasomaji wangu, wakiwalaumu wenzi wao kwa kutokuwa na shukrani katika mapenzi na ndiyo maana nimeanza kwa kukuuliza wewe msomaji wangu, mara ya mwisho ulimshukuru mwenzi wako lini? Tuchukulie wewe ni mwanaume, umeamka asubuhi, mpenzi wako anakuandalia maji ya kuoga, unakuta nguo tayari zilishafuliwa na kunyooshwa, viatu vimesafishwa, kifungua kinywa kipo tayari mezani, yaani kila kitu umeshafanyiwa. 

Unapotoka ukiwa umependeza na umeshiba, huwa unakumbuka kumshukuru kwa jinsi alivyokuandaa? Unarudi jioni au usiku, nyumba ipo safi, watoto kama mmejaliwa kuwa nao wameshakula na kupumzika, unawakuta wapo kwenye hali nzuri, chakula chako kimeshaandaliwa, unakula, unaoga, unapumzika na baadaye anakupunguzia uchovu wa pilikapilika za kutwa nzima kwa kukupa haki yako ya faragha! Huwa unakumbuka kumshukuru kwa haya yote anayokutendea? 

Na kwako mwanamke, mumeo, mchumba wako au mpenzi wako amesababisha uwe hivyo ulivyo, anakupa fedha kwa ajili ya kununua nguo nzuri, unaonekana mrembo kwa sababu umepewa fedha za kwenda saluni na kununua mafuta mazuri! Unapendeza na kunawiri kwa sababu anakuhudumia vya kutosha, una simu nzuri, unakula na kushiba vizuri, ukiwa na tatizo lolote yupo kwa ajili yako! Anakutunzia heshima yako na anakidhi vizuri haja zako za kimwili na kihisia. 

Amekupa heshima ya kuitwa mke wa mtu au mama fulani! Siku mojamoja anakuletea zawadi, anakutoa ‘out’ na kukufanyia mambo mengi ya kukufurahisha. Je, huwa unakumbuka kweli kumshukuru? Hakuna kitu kinachoweza kuimarisha mapenzi kama kumshukuru mwenzi wako, hata pale anapokufanyia jambo unaloliona dogo au lisilo na maana. 

Neno ‘ahsante’ ni dogo lakini huwa lina maana kubwa sana, hasa likitamkwa na yule umpendaye. Shukrani hukufanya ujisikie vizuri, hukupa hamasa ya kumfanyia mambo mengine makubwa ya kumfura hisha zaidi! Hukufanya ujihisi kuwa na amani ndani ya moyo wako kwa sababu unajua upo na mtu anayekujali na anayethamini kila unachomfanyia. 

Hebu jenga utaratibu kuanzia sasa, hata akishamaliza kukup a haki yako y a msingi, mpe pole na umshukuru kwa kazi nzuri, mweleze jinsi unavyofurahi kuwa naye! Utayaona mabadiliko ya waziwazi na hakika atazidi kukupenda. Jenga utaratibu wa kumshukuru kwa kila jambo analokufanyia, hata kama ni dogo. Unatoka kwenda kwenye mihangaiko yako, umependeza na kila mtu anakusifia, basi kama ulisahau kumshukuru ukiwa unatoka, ukirudi mpe pongezi zake kwa sababu umesifiwa kwa sababu yake, mshukuru kwa uso wa tabasamu, utashangaa atakavyoongeza mapenzi kwako.

 Maisha ya kukaa kwa mazoea na mwenzi wako, yaani kila kitu unachukulia kama cha kawaida tu, au ni wajibu wake kufanya kwa sababu wewe ni mkewe au mumewe, husababisha hisia za mapenzi kushuka au kuisha kabisa lakini neno ahsante, lina ‘uchawi’ wa kutosha wa kufufua furaha kwenye moyo wake, na akifurahi lazima atakupenda na kukuonesha mapenzi ya dhati! Sema ahsante kwa sababu haikugharimu chochote! Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

No comments

Powered by Blogger.