WAZIRI NCHEMBA AWATUHUMU WANASHERIA WAKUU WA SERIKALI SAKATA LA MCHANGA WA MADINI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaka wanasheria
wakuu wa Serikali wastaafu waeleze hadharani maslahi waliyonayo kwenye
kampuni za madini zinazosafirisha mchanga nje ya nchi.
Hatua hiyo ya waziri imekuja siku chache baada ya wanasheria wakuu
wastaafu waliofanya kazi kwa nyakati tofauti wakati nchi ikiingia kwenye
mikataba ya madini ‘kujivua lawama’ kuhusu udanganyifu uliogunduliwa
kuhusa sakata la usafirishaji wa mchanga.
Wanasheria hao wakuu wa Serikali wastaafu ni Andrew Chenge na Jaji
Frederick Werema na amewataka wamwache Rais Dk. Magufuli aendelee
kulinda rasilimali za umma zisiliwe na watu wachache.
Mwigulu amesema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Ndago, Jimbo la Iramba.
Alisema Chenge na Werema kwa nyakati tofauti wakiwa wanasheria wakuu wa
serikali, pamoja na majukumu yao mengine, wameshiriki kusaini mikataba
mikubwa mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya kuchimba madini.
“Kwa
akili ya kawaida tu, baadhi ya mikataba mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya
madini, haikuwa sawa… ndiyo maana imelalamikiwa kwa muda mrefu.” alifafanua Mwigulu, Mbunge wa Jimbo la Iramba.
Alisema juzi juzi magazeti yameeleza kuwa akina Chenge na Werema wamedai
kuwa Rais wetu Magufuli amedanganywa na tume maalumu ya Profesa Mruma.
“Wao
ndio waliosaini mikataba ambayo imechangia Taifa kupoteza mabilioni ya
fedha kupitia usafirishaji wa michanga nje ya nchi. Sasa wamegeuka na
kuwa upande wa pili wa watu waliosaini pamoja mikataba hiyo mibovu.
Nawashauri watoke hadharani…. waeleze wana maslahi gani na kampuni
wanazozitetea,” alifafanua zaidi.
Aidha, Mwigulu amesema Chenge na Werema wakishindwa kuweka wazi maslahi
waliyonayo, basi ni vema wakakaa kimya na kumwacha Rais wa vitendo
aendelee kuinyoosha nchi.
“Hivi
ukimpa mtu kazi ya kuuza duka, halafu kila siku awe anakuambia hajauza
kitu na huku akilalamika kuwa kila siku anapata hasara. Unamshauri
aachane na biashara inayompatia hasara, haachi…anaendelea kuwepo tu,
utamwalewaje. Si atakuwa si mkweli, mwongo ananufaika na hilo duka,” alisema.
Akiijengea nguvu hoja yake, alisema Chenge na Werema wanaishi Masaki,
jijini Dar es Salaam, hawa hawawezi au watakuwa wamesahau maisha ya
Watanzania wengi maskini waliopo vijijini. Hivyo wamwache Rais Magufuli
ambaye ameonyesha uzalendo wa kweli, aendelee kulinda rasilimali za
umma.
Alisema kwa wao wanaomfahamu Rais Magufuli, kwa hili la kuchokonoa
kwenye madini na kubaini upotevu mkubwa wa fedha za umma, ni mwanzo tu,
kazi bado ipo mbele ya kuchokonoa zaidi ubadhirifu na wizi wa mali ya
umma katika sehemu mbalimbali.
Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wazalendo wa madhehebu
ya dini mbalimbali waendelee kumwomba Mungu ampe Rais Magufuli afya
njema na ujasiri wa kuziba mwinya yote inayotia hasara Taifa letu.
-Chanzo: Mwananchi
Post a Comment